Genesis 13

Abramu Na Loti Watengana

Hivyo Abramu akakwea kutoka Misri kwenda Negebu, yeye na mkewe na kila kitu alichokuwa nacho, pia Loti akaenda pamoja naye. Wakati huo Abramu alikuwa tajiri sana wa mifugo, fedha na dhahabu.

Kutoka Negebu, akapita mahali hadi mahali, hadi akafika Betheli, mahali hapo ambapo mwanzoni alipiga hema lake kati ya Betheli na Ai hapo ambapo alikuwa amejenga madhabahu ya kwanza. Huko Abramu akaliitia jina la BWANA.

Basi Loti, ambaye alikuwa anafuatana na Abramu, alikuwa pia na makundi ya mbuzi, kondoo, ng'ombe na mahema. Lakini nchi haikuwatosha kukaa pamoja kwa ajili ya wingi wa mali zao. Ukazuka ugomvi kati ya wachunga mifugo wa Abramu na wale wa Loti. Wakati huo, Wakanaani na Waperizi ndio waliokuwa wenyeji wa nchi hiyo.

Hivyo Abramu akamwambia Loti, “Pasiwe na ugomvi wo wote kati yangu na wewe, wala kati ya wachungaji wangu na wako, kwa kuwa sisi ni ndugu. Je, nchi yote haiko mbele yako? Tutengane. Kama ukielekea kushoto, nitakwenda kulia; kama ukielekea kulia, mimi nitakwenda kushoto.”

10 Loti akatazama akaona lile bonde lote la Yordani kuwa lilikuwa na maji tele, kama bustani ya BWANA, kama nchi ya Misri, kuelekea Soari. (Hii ilikuwa kabla BWANA hajaharibu Sodoma na Gomora.) 11 Hivyo Loti akajichagulia bonde lote la Yordani, akaelekea upande wa mashariki. Watu hao wawili wakatengana: 12 Abramu akaishi katika nchi ya Kanaani, wakati Loti aliishi miongoni mwa miji ya lile bonde na kupiga mahema yake karibu na Sodoma. 13 Basi watu wa Sodoma walikuwa waovu, wakifanya sana dhambi dhidi ya BWANA.

14 Baada ya Loti kuondoka BWANA akamwambia Abramu, “Ukiwa hapo ulipo, inua macho yako utazame kaskazini na kusini, mashariki na magharibi. 15 Nchi yote unayoiona nitakupa wewe na uzao wako hata milele. 16 Nitaufanya uzao wako uwe mwingi kama mavumbi ya nchi, hivyo kama kuna ye yote awezaye kuhesabu mavumbi, basi uzao wako utahesabika. 17 Ondoka, tembea katika marefu na mapana ya nchi, kwa maana ninakupa wewe.”

18 Basi Abramu akaondoa mahema yake, akaenda kuishi karibu na mialoni ya Mamre huko Hebroni, huko akamjengea BWANA madhabahu.

Copyright information for Neno