Genesis 15

Agano La Mungu Na Abramu

1Baada ya jambo hili, neno la BWANA likamjia Abramu katika maono: “Usiogope, Abramu.
Mimi ni ngao yako,
na thawabu yako kubwa sana.”2Lakini Abramu akasema, “Ee BWANA Mwenyezi, utanipa nini na mimi sina hata mtoto na atakayerithi nyumba yangu ni huyu Eliezeri Mdameski?” 3Abramu akasema, “Hukunipa watoto, hivyo mtumishi katika nyumba yangu ndiye atakuwa mrithi wangu.”

4Ndipo neno la BWANA lilipomjia: “Mtu huyu hatakuwa mrithi wako, bali mwana atakayetoka katika viuno vyako mwenyewe ndiye atakayekuwa mrithi wako.” 5Akamtoa nje na kusema, “Tazama juu kuelekea mbinguni na uhesabu nyota, kama hakika utaweza kuzihesabu.” Ndipo akamwambia, “Hivyo ndivyo uzao wako utakavyokuwa.”

6Abramu akamwamini BWANA, naye kwake hili likahesabiwa kuwa haki.

7Pia akamwambia, “Mimi ndimi BWANA, niliyekutoa toka Uru ya Wakaldayo nikupe nchi hii uimiliki.”

8Lakini Abramu akasema, “Ee BWANA Mwenyezi, nitawezaje kujua kwamba nitapata kuimiliki?”

9Ndipo BWANA akamwambia, “Niletee mtamba wa ng'ombe, mbuzi na kondoo dume, kila mmoja wa miaka mitatu, pamoja na hua na kinda la njiwa.”

10Abramu akamletea hivi vyote, akampasua kila mnyama vipande viwili, akavipanga kila kimoja kuelekea mwenzake, lakini hata hivyo ndege, hakuwapasua vipande viwili. 11Kisha ndege walao nyama wakatua juu ya mizoga, lakini Abramu akawafukuza.

12Wakati jua lilipokuwa linatua, Abramu akashikwa na usingizi mzito, giza nene na la kutisha likaja juu yake. 13Kisha BWANA akamwambia, “Ujue hakika kwamba wazao wako watakuwa wageni kwenye nchi ambayo si yao wenyewe, nao watakuwa watumwa na watateswa kwa miaka mia nne. 14Lakini nitaliadhibu taifa lile wanaolitumikia kama watumwa, hatimaye watatoka huko na mali nyingi. 15Wewe, hata hivyo utakwenda kwa baba zako kwa amani na kuzikwa katika uzee mwema. 16Katika kizazi cha nne wazao wako watarudi hapa, kwa maana dhambi ya Waamori bado haijafikia kipimo kilichojaa.”

17Wakati jua lilipokuwa limezama na giza limeingia, tanuru la moshi na mwali wa moto unaowaka vikatokea na kupita kati ya vile vipande vya nyama. 18Siku hiyo BWANA akafanya Agano na Abramu, na kumwambia, “Nitawapa wazao wako nchi hii, kuanzia mto wa Misri
15.18Mto wa Misri hapa ina maana "Wadi-el-Arish" kwenye mpaka wa kusini wa Yuda
hadi mto ule mkubwa, Eufrati,
19yaani nchi ya Wakeni, Wakenizi, Wakadmoni, 20Wahiti, Waperizi, Warefai, 21Waamori, Wakanaani, Wagirgashi na Wayebusi.”

Copyright information for Neno