Genesis 17

Agano La Tohara

Abramu alipokuwa na miaka tisini na tisa, BWANA akamtokea akamwambia, “Mimi ndimi Mungu Mwenyezi
17:1 Mungu Mwenyezi hapa ni Jina la Kiebrania, El-Shaddai (yaani Mungu Mwenye utoshelevu wote)
; enenda mbele zangu na uishi kwa unyofu.
Nami nitafanya Agano langu kati yangu na wewe, nami nitakuzidisha sana sana.”

Abramu akaanguka kifudifudi, naye Mungu akamwambia, “Kwa upande wangu, hili ndilo Agano langu na wewe: Wewe utakuwa baba wa mataifa mengi. Jina lako hutaitwa tena Abramu, bali jina lako litakuwa Abrahamu
17.5Abrahamu maana yake Baba wa watu wengi
, kwa maana nimekufanya wewe baba wa mataifa mengi.
Nitakufanya uwe na uzao mwingi sana, kwako yatatoka mataifa nao wafalme watatoka kwako. Nitalithibitisha Agano langu kama Agano la milele kati yangu na wewe na wazao wako baada yako na vizazi vijavyo niwe Mungu wako na Mungu wa wazao wako. Nchi yote ya Kanaani, unakoishi sasa kama mgeni, nitakupa kuwa milki yako milele, na uzao wako, nami nitakuwa Mungu wao.”

Ndipo Mungu akamwambia Abrahamu, “Kwa upande wako, lazima ushike Agano langu, wewe na wazao wako kwa ajili ya vizazi vijavyo. 10 Hili ni Agano langu na wewe pamoja na wazao wako baada yako, Agano mtakalolishika: Kila mwanaume miongoni mwenu atatahiriwa. 11 Mtafanyiwa tohara na hii itakuwa ni alama ya Agano kati yangu na ninyi. 12 Kwa vizazi vijavyo, kila mwanaume miongoni mwenu mwenye siku nane ni lazima atahiriwe, pamoja na watakaozaliwa nyumbani mwako au walionunuliwa kwa fedha kutoka kwa mgeni, wale ambao sio watoto wako. 13 Awe amezaliwa nyumbani mwako au amenunuliwa kwa fedha yako, ni lazima watahiriwe. Agano langu katika mwili wako litakuwa ni Agano la milele. 14 Kila mwanaume asiyetahiriwa, ambaye hajapata tohara ya mwilini, atatengwa na watu wake, amelivunja Agano langu.”

15 Pia BWANA akamwambia Abrahamu, “Kwa upande wa Sarai mkeo, hutamwita tena Sarai bali jina lake litakuwa Sara. 16 Nitambariki na hakika nitakupatia mwana kwake. Nitambariki na kwamba atakuwa mama wa mataifa, wafalme wa mataifa watatoka kwake.”

17 Abrahamu akaanguka kifudifudi, akacheka na kusema moyoni mwake, “Je, mtu wa miaka mia moja aweza kuzaa mwana? Je, Sara atazaa mtoto katika umri wa miaka tisini?” 18 Abrahamu akamwambia Mungu, “Laiti Ishmaeli naye angeshiriki baraka yako!”

19 Ndipo Mungu akasema, “Ndiyo, lakini mkeo Sara atakuzalia wewe mwana, nawe utamwita jina lake Isaki
17.19Isaki maana yake Kucheka
. Nitalithibitisha Agano langu naye kama Agano la milele kwa ajili yake na wazao wake baada yake.
20 Kwa upande wa Ishmaeli, nimekusikia: hakika nitambariki, nitamfanya awe na uzao mwingi na nitaongeza sana idadi yake. Atakuwa baba wa watawala kumi na wawili, nami nitamfanya awe taifa kubwa. 21 Lakini Agano langu nitalithibitisha kwa Isaki, ambaye Sara atakuzalia mwaka ujao majira kama haya.” 22 Wakati alipomaliza kuzungumza na Abrahamu, Mungu akapanda juu akaondoka kwa Abrahamu.

23 Siku ile ile, Abrahamu akamchukua Ishmaeli mwanawe na wote waliozaliwa nyumbani mwake pamoja na walionunuliwa kwa fedha zake, kila mwanaume wa nyumbani mwake, akawatahiri, kama Mungu alivyomwagiza. 24 Abrahamu alikuwa na umri wa miaka tisini na tisa alipotahiriwa, 25 naye Ishmaeli mwanawe alitahiriwa akiwa na umri wa miaka kumi na mitatu. 26 Abrahamu na Ishmaeli mwanawe walitahiriwa siku ile ile, 27 Kila mwanaume nyumbani mwa Abrahamu, pamoja na wote waliozaliwa nyumbani mwake au aliyenunuliwa kutoka kwa mgeni, alitahiriwa pamoja naye.

Copyright information for Neno