Genesis 30

1Raheli alipoona hamzalii Yakobo watoto, akamwonea ndugu yake wivu. Hivyo akamwambia Yakobo, “Nipe watoto, la sivyo nitakufa!”

2Yakobo akamkasirikia, akamwambia, “Je, mimi ni badala ya Mungu, ambaye amekuzuia usizae watoto?”

3Ndipo Raheli akamwambia, “Hapa yupo Bilha, mtumishi wangu wa kike. Kutana naye kimwili ili aweze kunizalia watoto na kwa kupitia yeye mimi pia niweze kuwa na uzao.”

4Hivyo Raheli akampa Yakobo Bilha awe mke wake. Yakobo akakutana naye kimwili, 5akapata mimba, naye akamzalia mwana. 6Ndipo Raheli akasema, “Mungu amenipatia haki yangu, amesikiliza maombi yangu na kunipa mwana.” Kwa sababu hiyo akamwita Dani
30.6Dani maana yake Anahukumu, yaani Mungu amenipatia haki yangu
.

7Bilha mtumishi wa kike wa Raheli akapata mimba tena akamzalia Yakobo mwana wa pili. 8Ndipo Raheli akasema, “Nilikuwa na mashindano makubwa na ndugu yangu, nami nimeshinda.” Kwa hiyo akamwita Naftali
30.8Naftali maana yake Nimeshindana nami nimeshinda
.

9Lea alipoona kuwa amekoma kuzaa watoto, alimchukua mtumishi wake wa kike Zilpa naye akampa Yakobo awe mke wake. 10Mtumishi wa Lea yaani Zilpa, akamzalia Yakobo mwana. 11Ndipo Lea akasema, “Hii ni bahati nzuri iliyoje!” Kwa hiyo akamwita Gadi.

12Mtumishi wa kike wa Lea akamzalia Yakobo mwana wa pili. 13Ndipo Lea aliposema, “Jinsi gani nilivyo na furaha! Wanawake wataniita furaha.” Kwa hiyo akamwita Asheri
30.13Asheri maana yake Nimefurahi, yaani Mungu amenifurahisha
.

14Wakati wa kuvuna ngano, Reubeni akaenda shambani akakuta tunguja, ambazo alizileta kwa Lea mama yake. Raheli akamwambia Lea, “Tafadhali nakuomba unipe baadhi ya tunguja za mwanao.”

15Lakini Lea akamwambia, “Haikukutosha kumtwaa mume wangu? Je, utachukua na tunguja za mwanangu pia?”

Raheli akasema, “Vema sana! Yakobo atakutana nawe kimwili leo usiku, kwa malipo ya tunguja za mwanao.”

16Kwa hiyo Yakobo alipokuja kutoka shambani jioni ile, Lea akaenda kumlaki, akamwambia, “Lazima ukutane nami kimwili. Nimekukodisha kwa tunguja za mwanangu.” Kwa hiyo akakutana naye kimwili usiku ule.

17Mungu akamsikiliza Lea, naye akapata mimba akamzalia Yakobo mwana wa tano. 18Ndipo Lea akasema, “Mungu amenizawadia kwa kumpa mume wangu mtumishi wangu wa kike.” Kwa hiyo akamwita Isakari
30.18Isakari maana yake Zawadi, yaani Mungu amenizawadia
.

19Lea akapata mimba tena akamzalia Yakobo mwana wa sita. 20Ndipo Lea aliposema, “Mungu amenizawadia kwa zawadi ya thamani sana. Wakati huu mume wangu ataniheshimu kwa sababu nimemzalia wana sita.” Kwa hiyo akamwita Zabuloni
30.20Zabuloni maana yake Heshima
.

21Baadaye akamzaa mtoto wa kike akamwita Dina
30.21Dina maana yake Tetea haki, yaani Mungu amenitetea katika mashindano yangu
.

22Ndipo Mungu akamkumbuka Raheli, akasikia maombi yake na akafungua tumbo lake. 23Akapata mimba na akamzaa mwana na kusema, “Mungu ameniondolea aibu yangu.”

24Akamwita Yosefu
30.24Yosefu maana yake Yeye na aongeze, yaani Mungu na aniongezee
na kusema, “BWANA na anipe mwana mwingine.”

Makundi Ya Yakobo Yaongezeka

25Baada ya Raheli kumzaa Yosefu, Yakobo akamwambia Labani, “Nipe ruhusa nirudi katika nchi yangu. 26Nipe wake zangu na watoto, ambao nimetumika kuwapata, nami niende zangu. Unajua ni kazi kiasi gani ambayo nimekufanyia.”

27Lakini Labani akamwambia, “Ikiwa nimepata kibali machoni pako, tafadhali ukae. Nimegundua kwa njia ya uaguzi kwamba BWANA amenibariki kwa sababu yako.” 28Akaongeza kumwambia, “Taja ujira wako nami nitakulipa.”

29Yakobo akamwambia, “Unajua jinsi ambavyo nimekutumikia na jinsi ambavyo wanyama wako walivyolishwa vizuri chini ya uangalizi wangu. 30Kidogo ulichokuwa nacho kabla sijaja kimeongezeka sana, naye BWANA amekubariki po pote nilipokuwa. Lakini sasa, ni lini nitashughulikia mambo ya nyumba yangu mwenyewe?”

31Labani akamwuliza, “Nikupe nini?”

Yakobo akamjibu, “Usinipe cho chote lakini kama utanifanyia jambo hili moja, nitaendelea kuchunga na kuyaangalia makundi yako.
32Niruhusu nipite katika makundi yako yote leo niondoe humo kila kondoo mwenye mabakabaka au madoadoa, kila mwana-kondoo mweusi na kila mbuzi mwenye madoadoa au mabakabaka. Hawa watakuwa ujira wangu. 33Uadilifu wangu utanishuhudia siku zijazo, kila utakapochunguza ujira ambao umenilipa mimi. Mbuzi ye yote wangu ambaye hana mabakabaka wala madoadoa, au mwana-kondoo ambaye si mweusi, atahesabika ameibwa.”

34Labani akasema, “Ninakubali na iwe kama ulivyosema.” 35Siku ile ile Yakobo akawaondoa beberu wote waliokuwa na mistari au madoadoa na mbuzi wake wote waliokuwa na mistari au madoadoa (wote waliokuwa na alama nyeupe juu yao) na wana-kondoo weusi wote, akawaweka chini ya uangalizi wa wanawe. 36Kisha Labani akamwacha Yakobo kwa mwendo wa safari ya siku tatu kati yake na Yakobo, wakati Yakobo akiendelea kuchunga lile kundi la Labani lililobaki.

37Hata hivyo, Yakobo, akachukua fito mbichi zilizokatwa wakati huo huo za miti ya mlubna, mlozi na mwaramoni akazibambua ili mistari myeupe ionekane katika fito hizo. 38Kisha akaweka fito alizozibambua kwenye mabirika yote ya kunyweshea mifugo, ili ziwe mbele ya makundi walipokuja kunywa maji. Wanyama walipokuja kunywa maji, hali wakiwa wanahitaji mbegu, 39wakapandwa hizo fito zikiwa mbele yao, wanyama waliopata mimba mbele ya hizo fito, walizaa wanyama wenye mistari, madoadoa na mabakabaka. 40Yakobo akawatenga wadogo wa kundi peke yao, lakini akazielekeza nyuso za hao waliobaki kwenye wale wenye mistari na weusi waliokuwa mali ya Labani. Hivyo akatenga makundi yake mwenyewe na wala hakuwachanganya na wanyama wa Labani. 41Kila mara wanyama wenye nguvu walipohitaji mbegu, Yakobo aliweka zile fito kwenye mabirika mbele ya hao wanyama, ili wapandwe karibu na hizo fito, 42lakini ikiwa wanyama walikuwa wadhaifu hakuziweka hizo fito. Hivyo wanyama dhaifu wakawa wa Labani, na wanyama wenye nguvu wakawa wa Yakobo. 43Kwa njia hii Yakobo akastawi sana, tena akawa na makundi makubwa, watumishi wa kike na wa kiume na ngamia na punda.

Copyright information for Neno