Hebrews 10

Dhabihu Ya Kristo Ni Mara Moja Tu

Kwa maana Torati ni kivuli tu cha mambo mema yajayo, wala si uhalisi wa mambo yenyewe. Kwa sababu hii, haiwezekani kamwe kwa njia ya dhabihu zitolewazo mwaka hadi mwaka, kuwakamilisha wale wanaokaribia ili kuabudu. Kama dhabihu hizo zingeweza kuwakamilisha, hazingeendelea kutolewa tena. Kwa kuwa hao waabuduo wangekuwa wametakaswa mara moja tu, wala wasingejiona tena kuwa na dhambi. Lakini zile dhabihu zilikuwa ukumbusho wa dhambi kila mwaka, kwa sababu haiwezekani damu ya mafahali na mbuzi kuondoa dhambi.

Kwa hiyo, Kristo alipokuja duniani, alisema: “Dhabihu na sadaka hukuzitaka,
bali mwili uliniandalia;
sadaka za kuteketezwa na za dhambi
hukupendezwa nazo.
Ndipo niliposema, ‘Tazama niko hapa,
kama nilivyoandikiwa katika kitabu,
Nimekuja kuyafanya mapenzi yako, Ee Mungu.’ ”Kwanza alisema, “Dhabihu na sadaka, sadaka za kuteketezwa na za dhambi hukuzitaka, wala hukupendezwa nazo” (ingawa sheria iliagiza zitolewe). Kisha akasema “Tazama niko hapa, nimekuja kuyafanya mapenzi yako.” Aondoa lile Agano la kwanza ili kuimarisha la pili. 10 Katika mapenzi hayo sisi tumetakaswa na kufanywa watakatifu kwa njia ya sadaka ya mwili wa Yesu Kristo alioutoa mara moja tu.

11 Kila kuhani husimama siku kwa siku akifanya huduma yake ya ibada na kutoa tena na tena dhabihu zile zile ambazo haziwezi kamwe kuondoa dhambi. 12 Lakini huyu kuhani akiisha kutoa dhabihu moja kwa ajili ya dhambi kwa wakati wote, aliketi mkono wa kuume wa Mungu. 13 Tangu wakati huo anangoja mpaka adui zake wawekwe chini ya miguu yake, 14 kwa sababu kwa dhabihu moja amewafanya kuwa wakamilifu milele wale wote wanaotakaswa.

15 Pia Roho Mtakatifu anatushuhudia kuhusu jambo hili. Kwanza anasema: 16 “Hili ndilo Agano nitakalofanya nao
baada ya siku hizo, asema Bwana.
Nitaziweka sheria zangu mioyoni mwao,
na kuziandika katika nia zao.”17 Kisha aongeza kusema: “Dhambi zao na kutokutii kwao
sitakumbuka tena.”18 Basi haya yakiisha kusamehewa, hakuna tena dhabihu yo yote inayotolewa kwa ajili ya dhambi.

Wito Wa Kuvumilia

19 Kwa hiyo, ndugu zangu, kwa kuwa tunao ujasiri wa kupaingia Patakatifu pa Patakatifu kwa damu ya Yesu, 20 kwa njia mpya iliyo hai tuliyofunguliwa kwa ajili yetu kupitia kwenye lile pazia, yaani, mwili wake, 21 basi kwa kuwa tunaye Kuhani Mkuu juu ya nyumba ya Mungu, 22 sisi na tumkaribie Mungu kwa moyo mnyofu kwa imani timilifu, mioyo yetu ikiwa imenyunyizwa damu ya Kristo na kuwa safi kutokana na dhamiri mbaya nayo miili yetu ikiwa imeoshwa kwa maji safi. 23 Tushike kwa uthabiti lile tumaini la ukiri wetu bila kuyumbayumba, kwa maana yeye aliyeahidi ni mwaminifu. 24 Tuangaliane na kuhimizana sisi kwa sisi katika upendo na katika kutenda mema. 25 Wala tusiache kukutana pamoja, kama wengine walivyo na desturi ya kukutana, tuhimizane sisi kwa sisi kadiri tuonavyo Siku ile inakaribia.

26 Kama tukiendelea kutenda dhambi kwa makusudi baada ya kupokea ufahamu wa ile kweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi. 27 Lakini kinachobaki ni kungoja kwa hofu hukumu ya moto uwakao utakaowaangamiza adui za Mungu. 28 Ye yote aliyeikataa sheria ya Mose alikufa pasipo huruma kwa ushahidi wa watu wawili au watatu. 29 Je, mnadhani ni adhabu kali kiasi gani anayostahili kupewa mtu aliyemkanyaga Mwana wa Mungu chini ya nyayo zake, yeye aliyeifanya damu ya Agano iliyomtakasa kuwa kitu najisi na kumtendea maovu Roho wa neema? 30 Kwa kuwa tunamjua yeye aliyesema, “Kulipiza kisasi ni juu yangu; mimi nitalipiza.” Tena asema, “Bwana atawahukumu watu wake.” 31 Ni jambo la kutisha kuanguka mikononi mwa Mungu aliye hai.

32 Kumbukeni siku zile za kwanza, ambazo mkiisha kutiwa nuru mlistahimili mashindano makali ya maumivu. 33 Wakati mwingine mlitukanwa na kuteswa hadharani, wakati mwingine mlikuwa radhi kuungana na wale waliofanyiwa hivyo. 34 Mliwahurumia wale waliokuwa kifungoni, mkikubali kwa furaha kunyang'anywa mali zenu kwa maana mlijua kwamba mnayo mali iliyo bora zaidi idumuyo.

35 Kwa hiyo msiutupe ujasiri wenu, kwa maana una thawabu kubwa mno. 36 Inawapasa kuvumilia ili mkiisha kufanya mapenzi ya Mungu mpate kile alichoahidi. 37 Kwa kuwa bado kitambo kidogo tu, “Yeye ajaye atakuja wala hatakawia.
38 Lakini mwenye haki wangu
ataishi kwa imani.
Naye kama akisitasita
sina furaha naye.”39 Lakini sisi hatumo miongoni mwa hao wanaositasita na kuangamia, bali tuko miongoni mwa hao wenye imani na hivyo tunaokolewa.

Copyright information for Neno