Hebrews 9

Ibada Katika Hema La Kidunia

1Basi Agano lile la kwanza lilikuwa na kanuni zake za kuabudu na pia patakatifu pake pa kidunia. 2Hema lilitengenezwa, katika sehemu yake ya kwanza kulikuwa na kinara cha taa, meza na mikate iliyowekwa wakfu, hii sehemu iliitwa Mahali Patakatifu. 3Nyuma ya pazia la pili, palikuwa na sehemu iliyoitwa Patakatifu pa Patakatifu, 4ambako ndiko kulikokuwa na ile madhabahu ya dhahabu ya kufukizia uvumba na lile Sanduku la Agano lililofunikwa dhahabu. Sanduku hili lilikuwa na gudulia la dhahabu lenye ile mana, ile fimbo ya Aroni iliyochipuka na vile vibao vya mawe vya Agano. 5Juu ya lile Sanduku kulikuwa na makerubi ya Utukufu yakitilia kivuli kile kifuniko ambacho ndicho kiti cha rehema. Lakini hatuwezi kueleza vitu hivi kwa undani sasa.

6Basi vitu hivi vilikuwa vimepangwa, kwamba makuhani wakiingia daima katika sehemu ya kwanza ya hema ili kufanya taratibu zao za ibada, 7lakini ni Kuhani Mkuu peke yake ndiye aliyeingia ndani ya sehemu ya pili ya hema, tena hii ilikuwa mara moja tu kwa mwaka, lakini si bila kuchukua damu ambayo angetoa kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya watu waliotenda dhambi bila kukusudia. 8Kwa njia hii, Roho Mtakatifu alikuwa anaonyesha kwamba maadamu ile hema ya kwanza ilikuwa bado imesimama, njia ya kuingia Patakatifu pa Patakafifu ilikuwa bado haijafunguliwa. 9Huu ulikuwa mfano kwa ajili ya wakati wa sasa, kuonyesha kwamba sadaka na dhabihu zilizokuwa zikitolewa hazikuweza kusafisha dhamiri ya mtu anayeabudu. 10Lakini hizi zilishughulika tu na vyakula na vinywaji pamoja na taratibu mbalimbali za kunawa kwa nje, kanuni kwa ajili ya mwili zilizowekwa hadi wakati utimie wa matengenezo mapya.

Damu Ya Kristo

11Kristo alipokuja akiwa Kuhani Mkuu wa mambo mema ambayo tayari yameshawasili, alipitia kwenye hema iliyo kuu zaidi na bora zaidi, ambayo haikutengenezwa kwa mikono ya binadamu, hii ni kusema, ambayo si sehemu ya uumbaji huu. 12Hakuingia kwa njia ya damu ya mbuzi na ya ndama, lakini aliingia Patakatifu pa Patakatifu mara moja tu kwa damu yake mwenyewe, akiisha kupata ukombozi wa milele. 13Damu ya mbuzi na ya mafahali na majivu ya mitamba walivyonyunyiziwa wale waliokuwa najisi kwa taratibu za kiibada viliwatakasa hata kuwaondolea uchafu wa nje. 14Basi si zaidi sana damu ya Kristo, ambaye kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na waa kutusafisha dhamiri zetu, kutokana na matendo yaletayo mauti, ili tupate kumtumikia Mungu aliye hai!

15Kwa sababu hii Kristo ni mjumbe wa Agano Jipya, ili kwamba wale walioitwa waweze kupokea ile ahadi ya urithi wa milele, yeye alikufa awe ukombozi wao kutoka katika dhambi walizozitenda chini ya Agano la kwanza.

16Kwa habari ya wosia
9:16 Wosia hapa kwa neno la Kiyunani ni agano
, ni muhimu kuthibitisha kifo cha yule aliyeutoa,
17kwa sababu wosia huwa na nguvu tu wakati mtu akishakufa, kamwe hauwezi kutumika wakati yule aliyeuandika akiwa bado yuko hai. 18Hii ndiyo sababu hata lile Agano la kwanza halikuweza kutekelezwa pasipo damu. 19Wakati Mose alipotangaza kila amri kwa watu wote, alichukua damu ya ndama na ya mbuzi, pamoja na maji, sufu nyekundu na matawi ya mti wa hisopo, akanyunyizia kile kitabu na watu wote. 20Akisema, “Hii ndiyo damu ya Agano, ambalo Mungu amewaamuru kulitii.” 21Vivyo hivyo alinyunyizia damu hiyo kwenye lile hema pamoja na kila kifaa kilichotumika ndani yake kwa taratibu za ibada. 22Kwa kweli sheria hudai kwamba, karibu kila kitu kitakaswe kwa damu, wala pasipo kumwaga damu, hakuna msamaha wa dhambi.

23Kwa hiyo, ilikuwa muhimu kwa nakala za vitu vile vya mbinguni vitakaswe kwa dhabihu hizi, lakini vitu halisi vya mbinguni vilihitaji dhabihu bora kuliko hizi. 24Kwa maana Kristo hakuingia kwenye patakatifu palipofanywa kwa mikono ya mwanadamu, ambao ni mfano wa kile kilicho halisi. Yeye aliingia mbinguni penyewe, ili sasa aonekane mbele za Mungu kwa ajili yetu. 25Wala hakuingia mbinguni ili apate kujitoa mwenyewe mara kwa mara, kama vile Kuhani Mkuu aingiavyo Patakatifu pa Patakatifu kila mwaka kwa damu ambayo si yake mwenyewe. 26Ingelikuwa hivyo, ingelimpasa Kristo kuteswa mara nyingi tangu kuumbwa kwa ulimwengu. Lakini sasa ametokea mara moja tu katika mwisho wa nyakati aiondoe dhambi kwa kujitoa mwenyewe kuwa dhabihu. 27Kama vile mwanadamu alivyowekewa kufa mara moja tu na baada ya kufa akabili hukumu, 28vivyo hivyo Kristo alitolewa mara moja tu kuwa dhabihu ili azichukue dhambi za watu wengi, naye atakuja mara ya pili, si ili kuchukua dhambi, bali kuwaletea wokovu wale wanaomngoja kwa shauku.

Copyright information for Neno