Hosea 11

Upendo Wa Mungu Kwa Israeli

1“Wakati Israeli alipokuwa mtoto, nilimpenda,
nilimwita mwanangu kutoka Misri.
2Lakini kadiri nilivyomwita Israeli,
ndivyo walivyokwenda mbali nami.
Walitoa dhabihu kwa Mabaali
na kufukiza uvumba kwa vinyago.
3Mimi ndiye niliyemfundisha Efraimu kutembea,
nikiwashika mikono;
lakini hawakutambua
kuwa ni mimi niliyewaponya.
4Niliwaongoza kwa kamba za huruma ya kibinadamu,
kwa vifungo vya upendo;
niliondoa nira shingoni mwao
nami nikainama kuwalisha.
5“Je, hawatarudi Misri,
nayo Ashuru haitawatawala
kwa sababu wamekataa kutubu?
6Panga zitametameta katika miji yao,
zitaharibu makomeo ya malango yao
na kukomesha mipango yao.
7Watu wangu wamedhamiria kuniacha.
Hata kama wakimwita Yeye Aliye Juu Sana,
kwa vyo vyote hatawainua.
8“Efraimu, ninawezaje kukuacha?
Ee Israeli, ninawezaje kukutoa?
Nitawezaje kukutendea kama Adma?
Nitawezaje kukufanya kama Seboimu?
Moyo wangu umegeuka ndani yangu,
huruma zangu zote zimeamshwa.
9Sitatimiza hasira yangu kali,
wala sitageuka na kumharibu Efraimu.
Kwa kuwa mimi ndimi Mungu,
wala si mwanadamu,
Mtakatifu pekee miongoni mwenu.
Sitakuja kwa ghadhabu.
10Watamfuata BWANA;
atanguruma kama simba.
Wakati angurumapo,
watoto wake watakuja wakitetemeka
kutoka magharibi.
11Watakuja wakitetemeka
kama ndege wakitoka Misri,
kama hua wakitoka Ashuru.
Nitawakalisha katika nyumba zao,”
asema BWANA.

Dhambi Ya Israeli

12Efraimu amenizunguka kwa uongo,
nyumba ya Israeli kwa udanganyifu.
Naye Yuda ni mkaidi dhidi ya Mungu,
hata kinyume cha yeye
aliye mwaminifu Mtakatifu Pekee.
Copyright information for Neno