Hosea 2

1“Waambie ndugu zako, ‘Watu wangu,’ na pia waambie dada zako, ‘Wapendwa wangu.’

Israeli Aadhibiwa Na Kurudishwa

2“Mkemeeni mama yenu, mkemeeni,
kwa maana yeye si mke wangu,
nami si mume wake.
Aondoe sura ya uzinzi katika uso wake
na uzinzi kati ya matiti yake.
3Kama sivyo nitamvua nguo zake awe uchi
na kumwacha uchi kama siku ile aliyozaliwa.
Nitamfanya kama jangwa,
nitamgeuza awe nchi ya kiu,
nami nitamwua kwa kiu.
4Sitaonyesha upendo wangu kwa watoto wake,
kwa sababu ni watoto wa uzinzi.
5Mama yao amekosa uaminifu
na amewachukua mimba katika aibu.
Gomeri alisema, ‘Nitawaendea wapenzi wangu,
ambao hunipa chakula changu
na maji yangu,
sufu yangu na kitani yangu, mafuta yangu
na kinywaji changu.’
6Kwa hiyo mimi Mungu nitaizuia njia yake
kwa vichaka vya miiba,
nitamjengea ukuta ili kwamba
asiweze kutoka.
7Gomeri atawafuatia wapenzi wake lakini hatawapata;
atawatafuta lakini hatawapata.
Kisha atasema,
‘Nitarudi kwa mume wangu kama kwanza,
kwa maana nilikuwa na hali njema zaidi
kuliko sasa.’
8Gomeri hajakubali kuwa mimi ndiye
niliyempa nafaka, divai mpya na mafuta,
niliyemwongezea fedha na dhahabu waliyoitumia
kwa kumtumikia Baali.
9“Kwa hiyo nitachukua nafaka yangu wakati itakapokomaa
na divai yangu mpya wakati itakapokuwa tayari.
Nitamnyang'anya sufu yangu na kitani yangu
iliyokusudiwa kufunika uchi wake.
10Basi sasa nitaufunua ufisadi wake
mbele ya wapenzi wake;
hakuna ye yote atakayemtoa
mikononi mwangu.
11Nitakomesha furaha na macheko yake yote:
sikukuu zake za mwaka,
sikukuu za Miandamo ya Mwezi,
siku zake za Sabato,
sikukuu zake zote zilizoamuriwa.
12Nitaiharibu mizabibu yake na mitini yake,
ambayo alisema yalikuwa malipo yake
kutoka kwa wapenzi wake;
nitaifanya kuwa kichaka,
nao wanyama pori wataila.
13Nitamwadhibu kwa ajili ya siku
alizowafukizia uvumba Mabaali;
alipojipamba kwa pete
na kwa vito vya thamani,
na kuwaendea wapenzi wake,
lakini mimi alinisahau,”
asema BWANA.

14“Kwa hiyo sasa nitamshawishi;
nitamwongoza hadi jangwani
na kuzungumza naye kwa upole.
15Huko nitamrudishia mashamba yake ya mizabibu,
nami nitalifanya Bonde la Akori
2.15 Akori maana yake ni Taabu

mlango wa matumaini.
Huko ataimba kama alivyofanya katika siku za ujana wake,
kama siku zile alizotoka Misri.
16“Katika siku ile,” asema BWANA,
“utaniita mimi ‘Mume wangu’;
hutaniita tena mimi ‘Bwana wangu.’
17Nitaondoa majina ya Mabaali kutoka midomoni mwake,
wala hataomba tena kwa majina yao.
18Katika siku ile nitafanya Agano kwa ajili yao
na wanyama wa kondeni, na ndege wa angani,
na viumbe vile vitambaavyo ardhini.
Upinde, upanga na vita,
nitaondolea mbali katika nchi,
ili kwamba wote waweze kukaa salama.
19Nitakuposa uwe wangu milele;
nitakuposa kwa uadilifu na haki,
kwa upendo na huruma.
20Nitakuposa kwa uaminifu,
nawe utamkubali BWANA.
21“Katika siku ile nitajibu,”
asema BWANA,
“nitajibu kwa anga,
nazo anga zitajibu kwa nchi;
22nayo nchi itajibu kwa nafaka,
divai mpya na mafuta,
navyo vitajibu kwa Yezreeli.
23Nitampanda katika nchi kwa ajili yangu mwenyewe;
nami nitaonyesha pendo langu kwake
yule ambaye nilimwita, ‘Si mpenzi wangu
2:23 Kiebrania ni Lo-Ruhama
,’
Nitawaambia wale walioitwa, ‘Sio watu wangu
2:23 Kiebrania ni Lo-Ami
,’
‘Ninyi ni watu wangu’
nao watasema, ‘Wewe ndiwe Mungu wangu.’ ”
Copyright information for Neno