Isaiah 1

1Maono kuhusu Yuda na Yerusalemu ambayo Isaya mwana wa Amozi aliyaona wakati wa utawala wa Uzia, Yothamu, Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda.

Taifa Asi

2Sikieni, enyi mbingu! Sikilizeni, enyi dunia!
Kwa maana BWANA amesema:
“Nimewalisha watoto na kuwalea,
lakini wameniasi mimi.
3Ng'ombe anamjua bwana wake,
naye punda anajua hori la mmiliki wake,
lakini Israeli hajui,
watu wangu hawaelewi.”
4Lo! Taifa lenye dhambi,
watu waliolemewa na uovu,
uzao wa watenda mabaya,
watoto waliozoelea upotovu!
Wamemwacha BWANA,
Wamemkataa kwa dharau
yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli
na kumgeuzia kisogo.
5Kwa nini mzidi kupigwa?
Kwa nini kudumu katika uasi?
Kichwa chako chote kimejeruhiwa,
moyo wako wote ni mgonjwa.
6Kutoka wayo wako wa mguu
hadi kwenye utosi wa kichwa chako
hakuna uzima:
ni majeraha matupu na makovu
na vidonda vitokavyo damu,
havikusafishwa au kufungwa
wala kulainishwa kwa mafuta.
7Nchi yenu imekuwa ukiwa,
miji yenu imeteketezwa kwa moto;
nchi yenu imeachwa tupu na wageni
mbele ya macho yenu,
imeharibiwa kama vile imepinduliwa na wageni.
8Binti Sayuni ameachwa kama kipenu
katika shamba la mizabibu,
kama kibanda katika shamba la matikitimaji,
kama mji uliohusuriwa.
9Kama BWANA Mungu Mwenye Nguvu Zote
1.9 Bwana Mwenye Nguvu Zote hapa ni jina la Kiebrania Jehova Sabaoth (yaani Bwana wa Majeshi; pia War 9:29 na Yak 5:4)

asingelituachia walionusurika,
tungelikuwa kama Sodoma,
tungelifanana na Gomora.
10Sikieni neno la BWANA,
ninyi watawala wa Sodoma;
sikilizeni sheria ya Mungu wetu,
enyi watu wa Gomora!
11BWANA anasema, “Wingi wa sadaka zenu,
ni kitu gani kwangu?
Ninazo sadaka za kuteketezwa nyingi kupita kiasi,
za kondoo waume
na mafuta ya wanyama walionona,
Sipendezwi na damu za mafahali
wala za wana-kondoo na mbuzi.
12Mnapokuja kujihudhurisha mbele zangu,
ni nani aliyewataka ninyi mfanye hivyo,
huku kuzikanyaga nyua zangu?
13Acheni kuniletea sadaka zisizokuwa na maana!
Uvumba wenu ni chukizo kwangu.
Miandamo ya Mwezi, Sabato na makusanyiko ya ibada:
siwezi kuvumilia makusanyiko yenu maovu.
14Sikukuu zenu za Miandamo ya Mwezi
na sikukuu zenu zilizoamriwa
moyo wangu unazichukia.
Zimekuwa mzigo kwangu,
nimechoka kuzivumilia.
15Mnaponyosha mikono yenu katika kuomba,
nitaficha macho yangu nisiwaone;
hata mkiomba maombi mengi
sitasikiliza.
Mikono yenu imejaa damu;
16jiosheni na mkajitakase.
Yaondoeni matendo yenu maovu
mbele zangu!
Acheni kutenda mabaya,
17jifunzeni kutenda mema!
Tafuteni haki,
watieni moyo walioonewa.
Teteeni shauri la yatima,
wateteeni wajane.
18“Njoni basi na tuhojiane,”
asema BWANA.
“Ingawa dhambi zenu ni kama rangi nyekundu,
zitakuwa nyeupe kama theluji;
ingawa ni nyekundu sana kama damu,
zitakuwa nyeupe kama sufu.
19Kama mkikubali na kutii,
mtakula mema ya nchi,
20lakini kama mkikataa na kuasi,
mtaangamizwa kwa upanga.”
Kwa kuwa kinywa cha BWANA kimenena.

21Tazama jinsi ambavyo mji uliokuwa mwaminifu
umekuwa kahaba!
Mwanzoni ulikuwa umejaa unyofu,
haki ilikuwa inakaa ndani yake,
lakini sasa ni wauaji!
22Fedha yenu imekuwa takataka,
divai yenu nzuri imechanganywa na maji.
23Watawala wenu ni waasi,
rafiki wa wevi,
wote wanapenda rushwa
na kukimbilia hongo.
Hawatetei yatima,
shauri la mjane haliletwi mbele yao likasikilizwa.
24Kwa hiyo Bwana, BWANA Mwenye Nguvu Zote,
Mwenye Nguvu wa Israeli, asema hivi:
“Lo, nitapata faraja kutoka kwa adui zangu
na kujilipizia kisasi juu ya watesi wangu.
25Nitauelekeza mkono wangu dhidi yenu,
nitawasafisha takataka yenu yote
na kuwaondolea unajisi wenu wote.
26Nitawarudishieni waamuzi wenu
kama ilivyokuwa siku za zamani,
nao washauri wenu kama ilivyokuwa mwanzoni.
Baadaye utaitwa,
Mji wa Haki,
Mji Mwaminifu.”
27Sayuni itakombolewa kwa haki,
wale waliomo ndani yake waliotubu kwa uaminifu.
28Lakini waasi na wenye dhambi wote wataangamizwa,
nao wanaomwacha BWANA wataangamia.
29“Mtaaibika kwa sababu ya hiyo mialoni mliyoipenda
mkaifanya mahali pa kuabudia sanamu,
mtafadhaika kwa sababu ya bustani
mlizozichagua.
30Mtakuwa kama mwaloni wenye majani yanayonyauka,
kama bustani isiyokuwa na maji.
31Mtu mwenye nguvu atatoweka
kama majani makavu yawakayo moto
na kazi yake kama cheche ya moto;
vyote vitaungua pamoja,
wala hakuna wa kuuzima huo moto.”
Copyright information for Neno