Isaiah 11

Tawi Kutoka Kwa Yese

1Chipukizi litatokea kutoka katika shina la Yese,
kutoka mizizi yake Tawi litazaa tunda.
2Roho wa BWANA atakaa juu yake,
Roho wa hekima na wa ufahamu,
Roho wa shauri na uweza,
Roho wa maarifa na wa kumcha BWANA
3naye atafurahia kumcha BWANA.
Hatahukumu kwa yale ayaonayo kwa macho yake,
wala kuamua kwa yale ayasikiayo kwa masikio yake,
4bali kwa adili atahukumu wahitaji,
kwa haki ataamua wanyenyekevu wa dunia.
Ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake,
kwa pumzi ya midomo yake atawaua waovu.
5Haki itakuwa mkanda wake
na uaminifu utakuwa mshipi kiunoni mwake.
6Mbwa mwitu ataishi pamoja na mwana-kondoo,
chui atalala pamoja na mbuzi,
ndama, mwana simba na ng'ombe aliyenona wa mwaka mmoja watalisha pamoja,
naye mtoto mdogo atawaongoza.
7Ng'ombe na dubu watalisha pamoja,
watoto wao watalala pamoja
na simba atakula majani makavu kama maksai.
8Mtoto mchanga atacheza karibu na shimo
la nyoka mwenye sumu kali,
naye mtoto mdogo ataweka mkono wake
kwenye kiota cha nyoka mwenye sumu.
9Hawatadhuru wala kuharibu
juu ya mlima wangu mtakatifu wote,
kwa kuwa dunia itajawa na kumjua BWANA
kama maji yajazavyo bahari.
10

Katika siku hiyo, shina la Yese litasimama kama bendera kwa ajili ya mataifa, mataifa yatamkusanyikia na mahali pake pa kupumzika patatukuka.
11Katika siku hiyo Bwana atanyosha mkono wake mara ya pili kurudisha mabaki ya watu wake waliosalia kutoka Ashuru, Misri, Pathrosi
11.11 Pathrosi ina maana Misri ya Juu
, Kushi, Elamu, Babeli, Hamathi na kutoka visiwa vya baharini.
12

Atainua bendera kwa mataifa
na kuwakusanya Waisraeli walioko uhamishoni;
atawakusanya watu wa Yuda waliotawanyika
katika pembe nne za dunia.
13Wivu wa Efraimu utatoweka
na adui wa Yuda watakatiliwa mbali;
Efraimu hatamwonea Yuda wivu
wala Yuda hatakuwa na uadui na Efraimu.
14Watawashukia katika mitelemko ya Wafilisti
hadi upande wa magharibi,
kwa pamoja watawateka watu nyara
hadi upande wa mashariki.
Watawapiga Edomu na Moabu,
na Waamoni watatawaliwa nao.
15BWANA atakausha
ghuba ya Bahari ya Misri;
kwa upepo mkavu ataupeleka mkono wake
juu ya Mto Eufrati.
Ataugawanya katika vijito saba
ili watu waweze kuuvuka
wakiwa wamevaa viatu.
16Itakuwepo njia kuu kwa mabaki ya watu wake
wale waliosalia kutoka Ashuru,
kama ilivyokuwa kwa Israeli
walipopanda kutoka Misri.


Copyright information for Neno