Isaiah 17

Neno Dhidi Ya Dameski

Neno kuhusu Dameski: “Tazama, Dameski haitakuwa tena mji
bali itakuwa lundo la magofu.
Miji ya Aroeri itaachwa na itaachiwa makundi ya kondoo na mbuzi,
ambayo yatalala huko,
bila ye yote wa kuyaogopesha.
Mji wenye ngome utatoweka kutoka Efraimu,
nao uweza wa kifalme kutoka Dameski;
mabaki ya Aramu yatakuwa
kama utukufu wa Waisraeli,”
asema BWANA Mwenye Nguvu Zote.

“Katika siku ile utukufu wa Yakobo utafifia,
unene wa mwili wake utadhoofika.
Itakuwa kama mvunaji akusanyavyo nafaka
na kuvuna nafaka kwa mikono yake,
kama wakati mtu aokotapo masazo ya masuke ya nafaka
katika Bonde la Warefai.
Hata hivyo baadhi ya masazo yatabaki,
kama vile mti wa mzeituni unavyopigwa,
kukiachwa zeituni mbili au tatu juu ya matawi ya kileleni,
nne au tano katika matawi yazaayo sana,”
asema BWANA, Mungu wa Israeli.

Katika siku ile watu watamwangalia Muumba wao
na kuelekeza macho yao kwa huyo Aliye Mtakatifu wa Israeli.
Hawataziangalia tena madhabahu,
kazi za mikono yao,
nao hawatathamini nguzo za Ashera
17.8 Ashera hapa maana yake ni mungu mke aliyekuwa akiabudiwa pamoja na Baali

na madhabahu za kufukizia uvumba
zilizofanywa kwa mikono yao.

Katika siku ile miji yao iliyo imara, ambayo waliihama kwa sababu ya Waisraeli, itakuwa kama mahali palipoachwa pa vichaka na magugu. Nayo yote itakuwa ukiwa.
10 Mmemsahau Mungu Mwokozi wenu,
hamkumkumbuka Mwamba aliye ngome yenu.
Kwa hiyo, hata ingawa mlipandikiza mimea iliyo mizuri sana
na kuotesha mizabibu ya kigeni,
11 hata kama siku ile unapoipandikiza, unaifanya iote
na asubuhi ile ile unayoipanda,
unaifanya ichipue,
hata hivyo mavuno yatakuwa kama si kitu
katika siku ile ya ugonjwa
na maumivu yasiyoponyeka.
12 Lo! Ghadhabu ya mataifa mengi,
wanaghadhibika kama bahari iliyochafuka!
Lo! Makelele ya mataifa
wanavuma kama ngurumo za maji mengi!
13 Ingawa mataifa yanavuma kama ngurumo
za maji yanayofanya mawimbi,
wakati anapoyakemea yanakimbia mbali,
yanafukuzwa mbele ya upepo kama makapi juu ya milima,
kama jani livingirishwapo na dhoruba.
14 Wakati wa jioni, hofu ya ghafula!
Kabla ya asubuhi, wametoweka!
Hili ndilo fungu la wale wanaotupora,
fungu la wale wanaotunyang'anya mali zetu.


Copyright information for Neno