Isaiah 2

Mlima Wa BWANA

1Hili ndilo aliloliona Isaya mwana wa Amozi kuhusu Yuda na Yerusalemu:

2Katika siku za mwisho mlima wa Hekalu la BWANA utaimarishwa
kama mlima mkuu miongoni mwa milima,
utainuliwa juu kupita vilima
na mataifa yote yatamiminika huko.



3Mataifa mengi yatakuja na kusema, “Njoni na tuupande mlima wa BWANA,
kwenye nyumba ya Mungu wa Yakobo.
Atatufundisha njia zake,
ili tuweze kuenenda katika mapito yake.”
Sheria itatoka Sayuni,
neno la BWANA kutoka Yerusalemu.
4Atahukumu kati ya mataifa
na ataamua magomvi ya mataifa mengi.
Watafua panga zao kuwa majembe
na mikuki yao kuwa miundu ya kukata matawi.
Taifa halitainua upanga dhidi ya taifa jingine,
wala hayatafanya mazoezi ya vita tena.
5Njoni, Enyi nyumba ya Yakobo,
sisi na tutembee katika nuru ya BWANA


Siku Ya BWANA

6Umewatelekeza watu wako,
nyumba ya Yakobo.
Wamejaa ushirikina utokao Mashariki,
wanapiga ramli kama Wafilisti
na wanashikana mikono na wapagani.
7Nchi yao imejaa fedha na dhahabu,
hakuna mwisho wa hazina zao.
Nchi yao imejaa farasi,
hakuna mwisho wa magari yao.
8Nchi yao imejaa sanamu,
wanasujudia kazi za mikono yao,
vitu vile ambavyo vidole vyao vimevitengeneza.
9Kwa hiyo mwanadamu atashushwa
na binadamu atanyenyekezwa,
usiwasamehe.
10Ingieni kwenye miamba,
jificheni ardhini
kutokana na utisho wa BWANA
na utukufu wa enzi yake!
11Macho ya mtu mwenye majivuno yatanyenyekezwa
na kiburi cha wanadamu kitashushwa,
BWANA peke yake ndiye atakayetukuzwa siku hiyo.
12BWANA Mwenye Nguvu Zote anayo siku aliyoiweka akiba
kwa wote wenye kujivuna na wenye kiburi,
kwa wote wanaojikweza
(nao watanyenyekezwa),
13kwa mierezi yote ya Lebanoni,
iliyo mirefu sana,
nayo mialoni yote ya Bashani,
14kwa milima yote mirefu
na vilima vyote vilivyoinuka,
15kwa kila mnara ulio mrefu sana
na kila ukuta wenye ngome,
16kwa kila meli ya biashara ya Tarshishi
2:16 Ona pia 1 Fal 10:22; 22:48; 2 Nya 9:21; 20:36; Isa 60:9

na kila chombo cha baharini cha fahari.
17Majivuno ya mwanadamu yatashushwa
na kiburi cha wanadamu kitanyenyekezwa,
BWANA peke yake ndiye atatukuzwa siku hiyo,
18nazo sanamu zitatoweka kabisa.
19Watu watakimbilia kwenye mapango ndani ya miamba
na kwenye mahandaki ardhini
kutokana na utisho wa BWANA
na utukufu wa enzi yake,
ainukapo kuitikisa dunia.
20Katika siku ile watu watawatupia
panya na popo
vinyago vyao vya fedha na vya dhahabu,
walivyovitengeneza ili waviabudu.
21Watakimbilia kwenye mapango miambani
na kwenye nyufa za miamba
kutokana na utisho wa BWANA
na utukufu wa enzi yake,
ainukapo kuitikisa dunia.
22Acheni kumtumainia mwanadamu,
ambaye hana kitu ila pumzi katika pua zake.
Yeye ana thamani gani?
Copyright information for Neno