Isaiah 21

Unabii Dhidi Ya Babeli

Neno kuhusu Jangwa kando ya Bahari:
Kama upepo wa kisulisuli unaopita katika nchi hadi kusini,
mshambuliaji anakuja kutoka jangwani,
kutoka katika nchi inayotisha.
Nimeonyeshwa maono ya kutisha:
Msaliti anasaliti, mteka nyara anateka nyara.
Elamu, shambulia Umedi!
Izunguke kwa jeshi!
Nitakomesha huzuni zote alizosababisha.
Katika hili mwili wangu umeteswa na maumivu,
maumivu makali ya ghafula yamenishika,
kama yale ya mwanamke mwenye utungu wa kuzaa,
nimeduwazwa na lile ninalolisikia,
nimeshangazwa na lile ninaloliona.
Moyo wangu unababaika,
woga unanifanya nitetemeke,
gizagiza la jioni nililolitamani sana,
limekuwa hofu kuu kwangu.
Wanaandaa meza,
wanatandaza mazulia,
wanakula, wanakunywa!
Amkeni, enyi maafisa,
zitieni ngao mafuta!

Hili ndilo Bwana analoniambia: “Nenda, weka mlinzi,
na mtake atoe taarifa ya kile anachokiona.
Anapoona magari ya vita
pamoja na kundi la farasi,
wapanda punda au wapanda ngamia,
na awe macho, awe macho kikamilifu.”Naye mlinzi alipaza sauti, “Mchana baada ya mchana, bwana wangu,
ninasimama katika mnara wa ulinzi,
kila usiku ninakaa mahali pangu nilipoamriwa.
Tazama, yuaja mtu anayepanda gari la vita
pamoja na kundi la farasi.
Naye akajibu:
‘Babeli ameanguka,
ameanguka!
Vinyago vyote vya miungu yake
vimelala chini vikiwa vimevunjwavunjwa!’ ”
10 Ee watu wangu, mliopondwapondwa kwenye sakafu ya kupuria,
ninawaambia kile nilichokisikia
kutoka kwa BWANA Mwenye Nguvu Zote,
kutoka kwa Mungu wa Israeli.


Unabii Dhidi Ya Edomu

11 Neno kuhusu Duma: Mtu fulani ananiita kutoka Seiri,
“Mlinzi, ni muda gani uliobaki kupambazuke?
Mlinzi, usiku utaisha lini?”
12 Mlinzi akajibu,
“Asubuhi inakuja, lakini pia usiku.
Kama ungeliuliza, basi uliza;
bado na urudi tena.”


Unabii Dhidi Ya Arabia

13 Neno kuhusu Arabia: Enyi misafara ya Wadedani,
Mnaopiga kambi katika vichaka vya Arabia,
14 Leteni maji kwa wenye kiu,
ninyi mnaoishi Tema,
leteni chakula kwa ajili ya wakimbizi.
15 Wanaukimbia upanga,
kutoka upanga uliochomolewa alani,
kutoka upinde uliopindwa
na kutoka kwenye joto la vita.16 Hili ndilo Bwana analoniambia: “Katika muda wa mwaka mmoja, kama vile mtumishi aliyefungwa na mkataba angeihesabu, majivuno yote ya Kedari yatafikia mwisho. 17 Wanaume wavutao pinde walionusurika, mashujaa wa Kedari, watakuwa wachache.” BWANA, Mungu wa Israeli, amesema.

Copyright information for Neno