Isaiah 22

Unabii Kuhusu Yerusalemu

1Neno kuhusu Bonde la Maono: Nini kinachokutaabisha sasa,
kwamba ninyi nyote mmepanda juu ya mapaa?
2Ewe mji uliojaa ghasia,
Ewe mji wa makelele
na karamu za sherehe!
Watu wenu waliokufa hawakuuawa kwa upanga,
wala hawakufa vitani.
3Viongozi wako wote wamekimbia pamoja,
wamekamatwa bila kutumia upinde.
Ninyi nyote mliokamatwa mlichukuliwa wafungwa pamoja,
mlikimbia wakati adui alipokuwa bado mbali.
4Kwa hiyo nilisema, “Geukia mbali nami,
niache nilie kwa uchungu.
Usijaribu kunifariji
juu ya maangamizi ya watu wangu.”
5Bwana, BWANA Mwenye Nguvu Zote, anayo siku
ya ghasia, ya kukanyaga na ya kuogofya
katika Bonde la Maono,
siku ya kuangusha kuta
na ya kupiga kelele mpaka milimani.
6Elamu analichukua podo,
pamoja na waendesha magari ya vita na farasi,
Kiri anaifungua ngao.
7Mabonde yako yaliyo mazuri sana yamejaa magari ya vita,
nao wapanda farasi wamewekwa kwenye malango ya mji;
8ulinzi wa Yuda umeondolewa.
Nawe ulitazama katika siku ile
silaha katika Jumba la Kifalme la Mwituni,
9mkaona kuwa Mji wa Daudi
una matundu mengi katika ulinzi wake,
mkaweka akiba ya maji
kwenye Bwawa la Chini.
10Mlihesabu majengo katika Yerusalemu
nanyi mkabomoa nyumba ili kuimarisha ukuta.
11Mlijenga bwawa la maji katikati ya kuta mbili
kwa ajili ya maji ya Bwawa la Zamani,
lakini hamkumtazama yule aliyelitengeneza,
au kuwa na heshima kwa yule aliyeubuni tangu zamani za kale.
12Bwana, BWANA Mwenye Nguvu Zote,
aliwaita siku ile
ili kulia na kuomboleza,
kung'oa nywele zenu
na kuvaa nguo ya gunia.
13Lakini tazama, kuna furaha na sherehe,
kuchinja ng'ombe na kuchinja kondoo,
kula nyama na kunywa mvinyo!
Mnasema, “Sisi na tule na kunywa,
kwa kuwa kesho tunakufa!”14BWANA Mwenye Nguvu Zote amelifunua hili nikiwa ninasikia: Bwana, BWANA Mwenye Nguvu Zote, asema: “Mpaka siku ya kufa kwenu, dhambi hii haitafanyiwa upatanisho.”15Hili ndilo Bwana, BWANA Mwenye Nguvu Zote, asemalo: “Nenda ukamwambie huyu wakili Shebna,
ambaye ni msimamizi wa jumba la kifalme:
16Unafanya nini hapa na ni nani aliyekupa ruhusa
kujikatia kaburi lako mwenyewe,
ukichonga kaburi lako mahali palipo juu
na kutoboa kwa patasi mahali pako pa kupumzikia katika mwamba?
17“Jihadhari, BWANA yu karibu kukukamata kwa uthabiti
na kukutupa mbali kwa nguvu, Ewe mtu mwenye nguvu.
18Atakuvingirisha uwe kama mpira
na kukutupa katika nchi kubwa.
Huko ndiko utakakofia,
na huko ndiko magari yako ya vita ya fahari yatabakia,
wewe unayeifedhehesha nyumba ya bwana wako!
19Nitakuondoa kutoka katika kazi yako,
nawe utaondoshwa kutoka katika nafasi yako.20“Katika siku ile, nitamwita mtumishi wangu, Eliakimu mwana wa Hilkia. 21Nitamvika joho lako nami nitamfunga mshipi wako kiunoni mwake na kumkabidhi mamlaka yako. Yeye atakuwa baba kwa wale wanaoishi Yerusalemu na kwa nyumba ya Yuda. 22Nitaweka mabegani mwake ufunguo wa nyumba ya Daudi, kile afunguacho hakuna awezaye kufunga na kile afungacho hakuna awezaye kufungua. 23Nitamgongomea kama kigingi kilicho mahali palipo imara, naye atakuwa kiti cha enzi cha heshima kwa ajili ya nyumba ya baba yake. 24Utukufu wote wa jamaa yake utakuwa juu yake: Watoto wa jamaa hiyo na machipukizi yake, vyombo vyake vyote vidogo, tangu bakuli hadi magudulia yote.”

25BWANA Mwenye Nguvu Zote asema, “Katika siku ile, kigingi kilichogongomewa mahali imara kitaachia njia, kitakatwa, nacho kitaanguka na mzigo ulioning'inia juu yake utaanguka chini.” BWANA amesema.

Copyright information for Neno