Isaiah 30

Ole Wa Taifa Kaidi

1BWANA asema,
“Ole wa watoto wakaidi,
kwa wale wanaotimiza mipango ambayo si yangu,
wakifanya umoja, lakini si kwa Roho wangu,
wakilundika dhambi juu ya dhambi,
2wale washukao kwenda Misri
bila kutaka shauri langu,
wanaotafuta msaada wa ulinzi wa Farao,
watafutao kivuli cha Misri kwa ajili ya kimbilio.
3Lakini ulinzi wa Farao utakuwa kwa aibu yenu,
kivuli cha Misri kitawaletea fedheha.
4Ingawa wana maafisa katika Soani
na wajumbe wamewasili katika Hanesi,
5kila mmoja ataaibishwa
kwa sababu ya taifa lisilowafaa kitu,
ambalo haliwaletei msaada wala faida,
bali aibu tu na fedheha.”
6

Neno kuhusu wanyama wa Negebu: Katika nchi ya taabu na shida,
ya simba waume na wake,
ya nyoka mwenye sumu kali na nyoka warukao,
wajumbe huchukua utajiri wao juu ya migongo ya punda,
hazina zao juu ya nundu za ngamia,
kwa lile taifa lisilokuwa na faida,
7kuvipeleka Misri,
ambaye msaada wake haufai kabisa.
Kwa hiyo nimemwita “Rahabu, yaani, yeye aketiye
kimya bila kufanya cho chote.”
8Nenda sasa, liandike neno hili juu ya kibao kwa ajili yao,
liandike kwenye kitabu,
ili kwa ajili ya siku zijazo
liweze kuwa shahidi milele.
9Hawa ni watu waasi, watoto wadanganyifu,
watoto ambao hawataki
kusikiliza mafundisho ya BWANA.
10Wanawaambia waonaji,
“Msione maono tena!”
Nako kwa manabii wanasema,
“Msiendelee kutupatia maono
ambayo ni ya kweli!
Tuambieni mambo ya kupendeza,
tabirini mambo ya uongo.
11Acheni njia hii,
ondokeni katika mapito haya,
nanyi acheni kutukabili pamoja
na yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli!”12Kwa hiyo, hili ndilo asemalo yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli: “Kwa sababu mmekataa ujumbe huu,
mkategemea uonevu na kutumainia udanganyifu,
13dhambi hii itakuwa kwenu
kama ukuta mrefu,
wenye ufa na wenye kubetuka,
ambao unaanguka ghafula,
kwa mara moja.
14Utavunjika vipande vipande kama chombo cha udongo
ukipasuka pasipo huruma
ambapo katika vipande vyake
hakuna kipande kitakachopatikana
kwa kuukulia makaa kutoka mekoni
au kuchotea maji kisimani.”15Hili ndilo BWANA Mwenyezi, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, asemalo: “Katika kutubu na kupumzika ndio wokovu wenu,
katika kutulia na kutumaini ndizo nguvu zenu,
lakini hamkutaka.
16Mlisema, ‘Hapana, tutakimbia kwa farasi.’
Kwa hiyo mtakimbia!
Mlisema, ‘Tutakimbia kwa farasi waendao kasi.’
Kwa hiyo wanaowafukuza watakwenda kasi!
17Watu 1,000 watakimbia
kwa ajili ya kitisho cha mtu mmoja,
kwa vitishio vya watu watano
wote mtakimbia,
hadi mtakapoachwa
kama mlingoti wa bendera
juu ya kilele cha mlima,
kama bendera juu ya kilima.”
18Hata hivyo BWANA anatamani kutupatia neema,
anainuka ili kuwaonyesha huruma.
Kwa kuwa BWANA ni Mungu wa haki.
Wamebarikiwa wote wanaomngojea yeye!19Enyi watu wa Sayuni, mnaoishi Yerusalemu, hamtalia tena. Tazama jinsi atakavyokuwa na huruma mtakapolia kwa kumwomba msaada! Mara asikiapo, atawajibu. 20Ingawa Bwana huwapa chakula cha shida na maji ya taabu, walimu wenu hawatafichwa tena, kwa macho yenu wenyewe mtawaona. 21Kwamba mtageuka kuume au kushoto, masikio yenu yatasikia sauti nyuma yenu, ikisema, “Hii ndiyo njia, ifuateni.” 22Kisha mtanajisi sanamu zenu zilizofunikwa kwa fedha na vinyago vyenu vilivyofunikwa kwa dhahabu, mtazitupilia mbali kama vitambaa vya wakati wa hedhi na kuziambia, “Haya, tokeni hapa!”23Pia atawapa mvua kwa ajili ya mbegu mnazootesha ardhini, chakula kinachotoka ardhini kitakuwa kizuri sana tena kwa wingi. Katika siku ile ng'ombe wenu watalisha katika shamba pana la majani. 24Maksai na punda walimao watakula majani makavu na vyakula vilivyotengenezwa, vinavyotandazwa kwa uma na sepeto. 25Katika siku ile ya mauaji makuu, wakati minara itakapoanguka, vijito vya maji vitatiririka juu ya kila milima mirefu na kila kilima kilichoinuka sana. 26Mwezi utaangaza kama jua, nao mwanga wa jua utang'aa mara saba zaidi, kama nuru ya siku saba, wakati BWANA atakapoyafunga majeraha ya watu wake na kuwaponya vidonda alivyowatia. 27

Tazama, hilo Jina la BWANA linakuja kutoka mbali,
likiwa na hasira kali inayowaka
pamoja na wingu zito la moshi,
midomo yake imejaa ghadhabu
na ulimi wake ni moto ulao.
28Pumzi yake ni kama mkondo wa maji yaendayo kasi,
yakipanda hadi shingoni.
Hutikisa mataifa katika chekecheke ya uharibifu,
huweka lijamu katika mataya ya mataifa
ambayo huwaongoza upotevuni.
29Nanyi mtaimba kama usiku mnaoadhimisha
sikukuu takatifu,
mioyo yenu itashangilia
kama vile watu wanapokwea na filimbi
kwenye mlima wa BWANA,
kwa Mwamba wa Israeli.
30BWANA atawasababisha watu waisikie sauti yake ya utukufu,
naye atawafanya wauone mkono wake ukishuka
pamoja na hasira yake kali na moto ulao,
kukiwa na tufani ya mvua,
ngurumo za radi na mvua ya mawe.
31Sauti ya BWANA itaivunjavunja Ashuru,
kwa fimbo yake ya utawala atawapiga.
32Kila pigo BWANA atakaloliweka juu yao
kwa fimbo yake ya kuadhibu,
litakuwa kwa wimbo wa matari na vinubi,
anapopigana nao katika vita
kwa mapigo ya mkono wake.
33Tofethi imeandaliwa toka zamani,
imewekwa tayari kwa ajili ya mfalme.
Shimo lake la moto limetengenezwa kwa kina kirefu
na kwa upana mkubwa,
likiwa na moto na kuni tele;
pumzi ya BWANA,
kama kijito cha kiberiti,
huuwasha moto.


Copyright information for Neno