Isaiah 34

Hukumu Dhidi Ya Mataifa

1Njoni karibu, enyi mataifa, nanyi msikilize;
sikilizeni kwa makini,
enyi kabila za watu!
Dunia na isikie, navyo vyote vilivyo ndani yake,
ulimwengu na vyote vitokavyo ndani yake!
2BWANA ameyakasirikia mataifa yote;
ghadhabu yake ni juu ya majeshi yao yote.
Atawaangamiza kabisa,
atawatia mikononi mwa wachinjaji.
3Waliouawa watatupwa nje,
maiti zao zitatoa uvundo,
milima itatota kwa damu zao.
4Nyota zote za mbinguni zitayeyuka
na anga litasokotwa kama kitabu,
jeshi lote la angani litaanguka
kama majani yaliyonyauka kutoka kwenye mzabibu,
kama tini iliyonyauka kutoka kwenye mtini.
5Upanga wangu umekunywa na kushiba huko mbinguni,
tazama, unashuka katika hukumu juu ya Edomu,
wale watu ambao nimeshawahukumu,
kuwaangamiza kabisa.
6Upanga wa BWANA umeoga katika damu,
umefunikwa na mafuta ya nyama:
damu ya kondoo na mbuzi,
mafuta kutoka katika figo za kondoo waume.
Kwa maana BWANA ana dhabihu huko Bosra
na machinjo makuu huko Edomu.
7Nyati wataanguka pamoja nao,
ndama waume na mafahali wakubwa.
Nchi yao italowana kwa damu,
nayo mavumbi yataloa mafuta ya nyama.
8Kwa sababu BWANA anayo siku ya kulipiza kisasi,
mwaka wa malipo,
siku ya kushindania shauri la Sayuni.
9Vijito vya Edomu vitageuka kuwa lami,
mavumbi yake yatakuwa kiberiti kiunguzacho,
nchi yake itakuwa lami iwakayo!
10Haitazimishwa usiku wala mchana,
moshi wake utapaa juu milele.
Kutoka kizazi hadi kizazi itakuwa ukiwa,
hakuna mtu ye yote atakayepita huko tena.
11Bundi wa jangwani na bundi mwenye sauti nyembamba wataimiliki,
bundi wakubwa na kunguru wataweka viota humo.
Mungu atanyosha juu ya Edomu
kamba ya kupimia ya machafuko matupu
na timazi ya ukiwa.
12Watu wake wa kuheshimiwa hawatakuwa na cho chote
huko kitakachoitwa ufalme,
wana wao wa kifalme wote watatoweka.
13Miiba itaenea katika ngome za ndani,
viwawi na michongoma itaota
kwenye ngome zake.
Itakuwa maskani ya mbweha,
makao ya bundi.
14Viumbe vya jangwani vitakutana na fisi,
nao mbuzi-mwitu watalia wakiitana;
huko viumbe vya usiku vitastarehe pia
na kujitafutia mahali pa kupumzika.
15Bundi wataweka viota huko na kutaga mayai,
atayaangua na kutunza makinda yake
chini ya uvuli wa mbawa zake;
pia huko vipanga watakusanyika,
kila mmoja na mwenzi wake.
16

Angalieni katika gombo la BWANA na msome: Hakuna hata mmoja katika hawa atakayekosekana,
hakuna hata mmoja atakayemkosa mwenzi wake.
Kwa kuwa ni kinywa chake Mungu kimeagiza,
na Roho wake atawakusanya pamoja.
17Huwagawia sehemu zao,
mkono wake huwagawanyia kwa kipimo.
Wataimiliki hata milele
na kuishi humo kutoka kizazi hadi kizazi.


Copyright information for Neno