Isaiah 35

Furaha Ya Waliokombolewa

Jangwa na nchi kame vitafurahi;
nyika itashangilia na kuchanua maua.
Kama waridi,
litachanua maua,
litashangilia sana na kupaza sauti kwa furaha.
Litapewa utukufu wa Lebanoni.
Fahari ya Karmeli na Sharoni;
wataona utukufu wa BWANA,
fahari ya Mungu wetu.
Itieni nguvu mikono iliyo dhaifu,
yafanyeni imara magoti yaliyolegea,
waambieni wale wenye mioyo ya hofu,
“Iweni hodari, msiogope;
tazama, Mungu wenu atakuja,
pamoja na malipo ya Mungu,
atakuja na kuwaokoa ninyi.”
Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa
na masikio ya viziwi yatazibuliwa.
Ndipo kilema atarukaruka kama kulungu,
nao ulimi wa aliye bubu utapaza sauti kwa shangwe.
Maji yatatiririka kwa kasi katika nyika
na vijito katika jangwa.
Mchanga wa moto utakuwa bwawa la maji,
ardhi yenye kiu itabubujika chemchemi.
Maskani ya mbweha walikolala hapo awali
patamea majani, matete na mafunjo
35.7 Majani marefu kama matete yaotayo kwenye bwawa, ziwa au kandokando ya mto
.
Nako kutakuwa na njia kuu,
nayo itaitwa Njia ya Utakatifu.
Wasio safi hawatapita juu yake;
itakuwa kwa ajili ya wale
watembeao katika Njia ile;
yeye asafiriye juu yake,
ajapokuwa mjinga, hatapotea.
Huko hakutakuwepo na simba,
wala mnyama mkali hatapita njia hiyo,
wala hawatapatikana humo.
Ila waliokombolewa tu ndio watakaopita huko,
10 waliokombolewa na BWANA watarudi.
Wataingia Sayuni wakiimba;
furaha ya milele itakuwa juu ya vichwa vyao.
Watapata furaha na shangwe;
huzuni na majonzi vitakimbia.
Copyright information for Neno