Isaiah 36

Senakeribu Anatishia Yerusalemu

Katika mwaka wa kumi na nne wa kutawala kwa Mfalme Hezekia, Mfalme Senakeribu wa Ashuru alishambulia miji yote ya Yuda yenye maboma na kuiteka. Kisha mfalme wa Ashuru akamtuma Amirijeshi kutoka Lakishi hadi kwa Mfalme Hezekia huko Yerusalemu, pamoja na jeshi kubwa. Amirijeshi aliposimama kwenye mfereji wa Bwawa la Juu lililojengwa, katika njia iendayo kwenye uwanda wa Dobi, Eliakimu mwana wa Hilkia aliyekuwa msimamizi wa jumba la kifalme, Shebna aliyekuwa katibu na Yoa mwana wa Asafu mwandishi wakamwendea.

Amirijeshi akawaambia, “Mwambieni Hezekia,

“ ‘Hili ndilo asemalo mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru: Ni wapi ulikoweka hili tumaini lako?
Unasema mnayo mikakati na nguvu za kijeshi, lakini unasema maneno matupu tu. Je, wewe unamtegemea nani, hata kwamba unaniasi mimi? Tazama sasa, unaitegemea Misri, fimbo ile ya mwanzi uliopasuka, ambayo huutoboa na kuujeruhi mkono wa mtu akiiegemea! Hivyo ndivyo alivyo Farao mfalme wa Misri, kwa wote wanaomtegemea. Kama ukiniambia, “Tunamtumainia BWANA, Mungu wetu,” si ni yeye ambaye mahali pake pa juu na madhabahu zake Hezekia ameziondoa, akiwaambia Yuda na Yerusalemu, “Ni lazima msujudu mbele ya madhabahu hii”?

“ ‘Njoni sasa, fanyeni patano na bwana wangu, mfalme wa Ashuru: Nitakupa farasi 2,000, kama wewe unaweza kuwapandisha watu juu yao! Wawezaje basi kurudisha nyuma mmoja wa maafisa wangu wadogo wa bwana wangu, hata kama unaitegemea Misri kwa ajili ya magari ya vita na wapanda farasi? 10 Zaidi ya hayo, je, nimekuja kushambulia na kuangamiza nchi hii bila BWANA? BWANA mwenyewe aliniambia niingie niishambulie nchi hii na kuiangamiza.’ ”



11 Ndipo Eliakimu, Shebna na Yoa wakamwambia Amirijeshi, “Tafadhali, zungumza na watumishi wako kwa lugha ya Kiaramu, kwa kuwa tunaifahamu. Usiseme nasi kwa Kiebrania watu walioko juu ya ukuta wakiwa wanasikia.”

12 Lakini Amirijeshi akajibu, “Kwani ni kwa bwana wenu na ninyi peke yenu ambao bwana wangu amenituma kusema mambo haya, wala si kwa watu walioketi juu ya ukuta, ambao, kama ninyi, itawapasa kula mavi yao na kunywa mkojo wao wenyewe?”

13 Ndipo Amirijeshi akasimama na kuita kwa lugha ya Kiebrania, “Sikilizeni maneno ya mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru! 14 Hili ndilo mfalme asemalo: Msikubali Hezekia awadanganye. Hawezi kuwaokoa! 15 Msikubali Hezekia awashawishi kumtumaini BWANA wakati anaposema, ‘Hakika BWANA atatuokoa sisi, mji huu hautatiwa mikononi mwa mfalme wa Ashuru.’

16 “Msimsikilize Hezekia. Hili ndilo mfalme wa Ashuru asemalo: Fanyeni amani nami na mje kwangu. Kisha kila mmoja wenu atakula kutoka katika mzabibu wake na mtini wake mwenyewe na kunywa maji kutoka katika kisima chake mwenyewe, 17 mpaka nije nikawachukue mwende kwenye nchi iliyo kama nchi yenu wenyewe, nchi ya nafaka na divai mpya, nchi ya mkate na ya mashamba ya mizabibu.

18 “Msikubali Hezekia awapotoshe wakati asemapo, ‘BWANA atatuokoa.’ Je, mungu wa taifa lo lote ameshawahi kuokoa nchi yake kutoka katika mkono wa mfalme wa Ashuru? 19 Wako wapi miungu ya Hamathi na ya Arpadi? Wako wapi miungu ya Sefarvaimu? Je, wameokoa Samaria kutoka katika mkono wangu? 20 Ni yupi miongoni mwa miungu yote ya nchi hizi aliyeweza kuokoa nchi yake kutoka kwangu? Inawezekanaje basi BWANA kuiokoa Yerusalemu kutoka katika mkono wangu?”

21 Lakini watu wakakaa kimya wala hawakujibu lo lote, kwa kuwa mfalme aliamuru kuwa, “Msimjibu.”

22 Kisha Eliakimu mwana wa Hilkia kiongozi wa jumba la kifalme, Shebna katibu na Yoa mwana wa Asafu, mwandishi wakamwendea Hezekia, nguo zao zikiwa zimeraruliwa na kumwambia yale Amirijeshi aliyosema.

Copyright information for Neno