Isaiah 39

Wajumbe Kutoka Babeli

Wakati huo Merodaki-Baladani mwana wa Baladani mfalme wa Babeli alimpelekea Hezekia barua na zawadi, kwa kuwa alikuwa amesikia habari za kuugua na kupona kwake. Hezekia akawapokea wajumbe hao kwa furaha na kuwaonyesha kile kilichokuwa ndani ya ghala zake: Fedha, dhahabu, vikolezo, mafuta safi, silaha zake zote za vita na kila kitu kilichopo katika hazina zake. Hapakuwepo kitu cho chote katika jumba lake la kifalme au katika ufalme wake wote ambacho Hezekia hakuwaonyesha.

Ndipo nabii Isaya akaenda kwa Mfalme Hezekia na kumwuliza, “Watu wale walisema nini, nao wametoka wapi?”

Hezekia akajibu, “Kutoka nchi ya mbali. Walikuja kwangu kutoka Babeli.”

Nabii akauliza, “Waliona nini katika jumba lako la kifalme?”

Hezekia akajibu, “Waliona kila kitu katika jumba langu la kifalme. Hakuna kitu cho chote katika hazina yangu ambacho sikuwaonyesha.”

Ndipo Isaya akamwambia Hezekia, “Sikia neno la BWANA Mwenye Nguvu Zote: Hakika wakati unakuja ambapo kila kitu katika jumba lako la kifalme, navyo vyote ambavyo baba zako waliweka akiba mpaka siku hii, vitachukuliwa kwenda Babeli. Hakuna cho chote kitakachosalia, asema BWANA. Tena baadhi ya wazao wako, watu wa nyama na damu yako mwenyewe watakaozaliwa kwako, watachukuliwa, nao watakuwa matowashi katika jumba la kifalme la mfalme wa Babeli.”

Hezekia akajibu, “Neno la BWANA ulilosema ni jema.” Kwa kuwa alifikiri, “Patakuwepo amani na salama katika siku za maisha yangu.”

Copyright information for Neno