Isaiah 4

1Katika siku ile wanawake saba
watamshika mwanaume mmoja
wakisema, “Tutakula chakula chetu wenyewe
na kuvaa nguo zetu wenyewe,
ila wewe uturuhusu tu tuitwe kwa jina lako.
Utuondolee aibu yetu!”

Tawi La BWANA

2Katika siku ile Tawi la BWANA litakuwa zuri na lenye utukufu, nalo tunda la nchi litakuwa fahari na utukufu wa wale Waisraeli watakaonusurika. 3Wale watakaoachwa Sayuni, watakaobaki Yerusalemu, wataitwa watakatifu, wale wote ambao wameorodheshwa miongoni mwa walio hai huko Yerusalemu. 4Bwana atausafisha uchafu wa wanawake wa Sayuni, atatakasa madoa ya damu kutoka Yerusalemu kwa Roho ya hukumu na Roho ya moto. 5Kisha BWANA ataumba juu ya Mlima wote wa Sayuni na juu ya wale wote wanaokusanyika hapo, wingu la moshi wakati wa mchana na kung'aa kwa miali ya moto wakati wa usiku, juu ya huo utukufu wote kutatanda kifuniko cha ulinzi. 6Utakuwa sitara na kivuli kutokana na joto la mchana na kuwa mahali pa kujificha kutokana na dhoruba na mvua.

Copyright information for Neno