Isaiah 47

Anguko La Babeli

1“Shuka uketi mavumbini,
Ee Bikira Binti Babeli;
keti chini pasipo na kiti cha enzi,
Ee binti wa Wakaldayo.
Hutaitwa tena mwororo wala wa kupendeza.
2Chukua mawe ya kusagia na usage unga,
vua shela yako.
Pandisha mavazi yako, ondoa viatu vyako,
vuka vijito kwa shida.
3Uchi wako utafunuliwa
na aibu yako itaonekana.
Nitalipa kisasi;
sitamhurumia hata mmoja.”
4Mkombozi wetu: BWANA Mwenye Nguvu Zote ndilo jina lake;
ndiye yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli.
5“Keti kimya, ingia gizani,
Binti wa Wakaldayo,
hutaitwa tena malkia wa falme.
6Niliwakasirikia watu wangu
na kuaibisha urithi wangu;
niliwatia mikononi mwako,
nawe hukuwaonea huruma.
Hata juu ya wazee
uliweka nira nzito sana.
7Ukasema, ‘Nitaendelea
kuwa malkia milele!’
Lakini hukutafakari mambo haya
wala hukuwaza juu ya kile ambacho
kingeweza kutokea.
8“Sasa basi, sikiliza, ewe kiumbe mpenda anasa,
ukaaye katika mahali pako pa salama
na kujiambia mwenyewe,
‘Mimi ndiye, wala hakuna mwingine zaidi yangu.
Kamwe sitakuwa mjane
wala sitafiwa na watoto.’
9Haya yote mawili yatakupata kufumba na kufumbua,
katika siku moja:
kufiwa na watoto na ujane.
Vyote hivyo vitakupata kwa kipimo kikamilifu,
ijapokuwa uchawi wako ni mwingi
na uaguzi wako ni mwingi.
10Umeutegemea uovu wako,
nawe umesema, ‘Hakuna ye yote anionaye.’
Hekima yako na maarifa yako vinakupoteza
unapojiambia mwenyewe,
‘Mimi ndiye, wala hakuna mwingine zaidi yangu.’
11Maafa yatakujia,
nawe hutaweza kuyaondoa kwa uaguzi.
Janga litakuangukia
wala hutaweza kulikinga kwa fidia;
msiba mkuu usioweza kuutabiri
utakujia ghafula.
12“Endelea basi na uaguzi wako
na wingi wa uchawi wako,
ambao umeutumikia tangu utoto wako.
Labda utafanikiwa,
labda unaweza ukasababisha hofu kuu.
13Ushauri wote uliopokea umekuchosha bure!
Wanajimu wako na waje mbele,
wale watazamao nyota na watabirio mwezi baada ya mwezi,
wao na wawaokoe na lile linalokuja juu yenu.
14Hakika wako kama mabua makavu,
moto utawateketeza.
Hawawezi hata kujiokoa wao wenyewe
kutokana na nguvu za mwali wa moto.
Hapa hakuna makaa ya kumtia mtu ye yote joto;
hapa hakuna moto wa kuota.
15Hayo ndiyo yote wanayoweza kuwatendea ninyi,
hawa ambao umetaabika nao
na kufanya nao biashara tangu utoto.
Kila mmoja atatoroka;
hakuna ye yote awezaye kukuokoa.
Copyright information for Neno