Isaiah 50

Dhambi Ya Israeli Na Utii Wa Mtumishi

1Hili ndilo asemalo BWANA: “Iko wapi hati ya talaka ya mama yako
ambayo kwayo niliachana naye?
Au nimewauza ninyi kwa nani
miongoni mwa watu wanaonidai?
Kwa ajili ya dhambi zenu mliuzwa,
kwa sababu ya makosa mama yenu aliachwa.
2Nilipokuja, kwa nini hakuwepo hata mmoja?
Nilipoita, kwa nini hakuwepo hata mmoja wa kujibu?
Je, mkono wangu ni mfupi mno hata nisiweze kuwakomboa?
Je, mimi sina nguvu za kukuokoa?
Kwa kukemea tu naikausha bahari,
naigeuza mito ya maji kuwa jangwa;
samaki wake wanaoza kwa kukosa maji
na kufa kwa ajili ya kiu.
3Ninalivika anga weusi na kufanya nguo ya gunia
kuwa kifuniko chake.”
4BWANA Mwenyezi amenipa ulimi uliofundishwa,
ili kujua neno lile limtegemezalo aliyechoka.
Huniamsha asubuhi kwa asubuhi,
huamsha sikio langu lisikie kama mtu afundishwaye.
5BWANA Mwenyezi amezibua masikio yangu,
nami sikuwa mwasi,
wala sikurudi nyuma.
6Niliwapa mgongo wangu wale wanipigao,
mashavu yangu wale wang'oao ndevu zangu;
sikuuficha uso wangu kutokana na fedheha
na kutemewa mate.
7Kwa sababu BWANA Mwenyezi ananisaidia,
sitatahayarika.
Kwa hiyo nimekaza uso wangu kama jiwe la gumegume,
nami ninajua sitaaibika.
8Yeye anipatiaye haki yangu yu karibu.
Ni nani basi atakayeleta mashtaka dhidi yangu?
Tukabiliane uso kwa uso!
Mshitaki wangu ni nani?
Ni nani aliye mshitaki wangu?
9Ni BWANA Mwenyezi ndiye anisaidiaye mimi.
Ni nani huyo atakayenihukumu?
Wote watachakaa kama vazi,
nondo atawala awamalize.
10Ni nani miongoni mwenu amchaye BWANA
na kulitii neno la mtumishi wake?
Yeye atembeaye gizani,
yeye asiye na nuru,
na alitumainie jina la BWANA
na amtegemee Mungu wake.
11Lakini sasa, ninyi nyote mnaowasha mioto
na kupeana ninyi kwa ninyi mienge iwakayo,
nendeni, tembeeni katika nuru ya moto wenu
na ya mienge mliyoiwasha.
Hili ndilo mtakalolipokea kutoka mkononi mwangu:
Mtalala chini kwa mateso makali.


Copyright information for Neno