Isaiah 55

Mwaliko Kwa Wenye Kiu

“Njoni, ninyi nyote wenye kiu,
njoni kwenye maji;
nanyi ambao hamna fedha,
njoni, nunueni na mle!
Njoni, nunueni divai na maziwa
bila fedha na bila gharama.
Kwa nini kutumia fedha kwa kitu ambacho si chakula,
na kutaabikia kitu kisichoshibisha?
Sikilizeni, nisikilizeni mimi na mle kilicho kizuri,
nazo nafsi zenu zitafurahia utajiri wa unono.
Tegeni sikio mje kwangu,
nisikieni mimi, ili nafsi zenu zipate kuishi.
Nitafanya Agano la milele nanyi,
pendo la uaminifu nililomwahidi Daudi.
Tazama, nimemfanya kuwa shahidi wa mataifa,
kiongozi na jemadari wa mataifa.
Hakika utaita mataifa usiyoyajua,
nayo mataifa yale yasiyokujua yataharakisha kukujia,
kwa sababu ya BWANA Mungu wako,
yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli,
kwa maana amekutukuza.”
Mtafuteni BWANA maadamu anapatikana;
mwiteni maadamu yu karibu.
Mtu mwovu na aiache njia yake
na mtu mbaya na ayaache mawazo yake.
Yeye na amrudie BWANA, naye atamrehemu,
arudi kwa Mungu wetu,
kwa kuwa atamsamehe bure kabisa.
“Kwa kuwa mawazo yangu si mawazo yenu,
wala njia zenu si njia zangu,”
asema BWANA.

“Kama vile mbingu zilivyo juu kuliko dunia,
ndivyo njia zangu zilivyo juu kuliko njia zenu
na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.
10 Kama vile mvua na theluji
ishukavyo kutoka mbinguni,
nayo hairudi tena huko
bila kunywesha dunia
na kuichipusha na kuistawisha,
hivyo hutoa mbegu kwa mpanzi
na mkate kwa mlaji,
11 ndivyo lilivyo neno langu lile litokalo kinywani mwangu:
Halitanirudia tupu,
bali litatimiliza lile nililokusudia
na litafanikiwa katika kusudi
lile nililolituma.
12 Mtatoka nje kwa furaha
na kuongozwa kwa amani;
milima na vilima
vitapaza sauti kwa nyimbo mbele yenu,
nayo miti yote ya shambani
itapiga makofi.
13 Badala ya kichaka cha miiba
itaota miti ya misunobari,
na badala ya michongoma
utaota mhadasi
55.13 Mhadasi ni aina ya mti ambao huota milimani karibu na Yerusalemu, hutoa harufu nzuri itumikayo kutengeneza manukato; kwa Kiebrania ni "hadas", na ilikuwa inatumika kujenga vibanda wakati wa Sikukuu ya Vibanda (ona pia Neh 8:15)
.
Hili litakuwa jambo la kumpatia BWANA jina,
kwa ajili ya ishara ya milele,
ambayo haitaharibiwa.”
Copyright information for Neno