Isaiah 56

Wokovu Kwa Ajili Ya Wengine

Hili ndilo asemalo BWANA: “Dumisheni haki
na mkatende lile lililo sawa,
kwa maana wokovu wangu u karibu
na haki yangu itafunuliwa upesi.
Amebarikiwa mtu yule atendaye hili,
mtu yule alishikaye kwa uthabiti,
yeye ashikaye Sabato bila kuinajisi,
auzuiaye mkono wake
usifanye uovu wo wote.”
Usimwache mgeni aambatanaye na BWANA aseme,
“Hakika BWANA atanitenga na watu wake.”
Usimwache towashi ye yote alalamike akisema,
“Mimi ni mti mkavu tu.”Kwa kuwa hili ndilo asemalo BWANA: “Kwa matowashi washikao Sabato zangu,
ambao huchagua kile kinachonipendeza
na kulishika sana Agano langu,
hao nitawapa ndani ya Hekalu langu na kuta zake
kumbukumbu na jina bora kuliko kuwa
na watoto wa kiume na wa kike:
Nitawapa jina lidumulo milele
ambalo halitakatiliwa mbali.
Wageni wanaoambatana na BWANA
kumtumikia,
kulipenda jina la BWANA,
na kumwabudu yeye,
wote washikao Sabato bila kuinajisi
na ambao hushika sana Agano langu
hawa nitawaleta kwenye mlima wangu mtakatifu
na kuwapa furaha
ndani ya nyumba yangu ya sala.
Sadaka zao za kuteketeza na dhabihu zao
zitakubalika juu ya madhabahu yangu,
kwa maana nyumba yangu itaitwa
nyumba ya sala kwa mataifa yote.”
BWANA Mwenyezi asema, yeye awakusanyaye
Waisraeli waliohamishwa:
“Bado nitawakusanya na wengine kwao zaidi ya hao
ambao wameshakusanywa tayari.”


Mashtaka Ya Mungu Dhidi Ya Waovu

Njoni, enyi wanyama wote wa kondeni,
njoni mle, ninyi wanyama wote wa mwituni!
10 Walinzi wa Israeli ni vipofu,
wote wamepungukiwa na maarifa;
wote ni mbwa walio bubu
hawawezi kubweka;
hulala na kuota ndoto,
hupenda kulala.
11 Ni mbwa wenye tamaa kubwa,
kamwe hawatosheki.
Wao ni wachungaji waliopungukiwa na ufahamu;
wote wamegeukia njia yao wenyewe,
kila mmoja hutafuta faida yake mwenyewe.
12 Kila mmoja hulia, “Njoni, tupate mvinyo!
Tunywe kileo sana!
Kesho itakuwa kama leo,
au hata bora zaidi.”
Copyright information for Neno