Isaiah 57

Ibada Ya Sanamu Ya Israeli Iliyo Batili

1Mwenye haki hupotea,
wala hakuna hata mmoja
awazaye hilo moyoni mwake;
watu wanaomcha Mungu huondolewa,
wala hakuna hata mmoja anayeelewa
kuwa wenye haki wameondolewa
wasipatikane na maovu.
2Wale waendao kwa unyofu
huwa na amani;
hupata pumziko walalapo mautini.
3“Lakini ninyi, njoni hapa, ninyi wana wa wachawi,
ninyi wazao wa wazinzi na makahaba!
4Mnamdhihaki nani?
Ni nani mnayemcheka kwa dharau
na kumtolea ndimi zenu?
Je, ninyi si watoto wa waasi,
Uzao wa waongo?
5Mnawaka tamaa katikati ya mialoni
na chini ya kila mti uliotanda matawi;
mnawatoa kafara watoto wenu kwenye mabonde
na chini ya majabali yenye mianya.
6“Sanamu zilizoko katikati ya mawe laini ya mabondeni
ndiyo fungu lenu;
hizo ndizo sehemu yenu.
Naam, kwa hizo mmemimina sadaka za vinywaji,
na kutoa sadaka za nafaka.
Kwa ajili ya haya yote,
niendelee kuona huruma?
7Umeweka kitanda chako juu kwenye kilima kirefu kilichoinuka,
huko ulikwenda kutoa dhabihu zako.
8Nyuma ya milango yako na miimo yako
umeweka alama zako za kipagani.
Kwa kuniacha mimi, ulifunua kitanda chako,
umepanda juu yake
na kukipanua sana;
ulifanya patano na wale ambao unapenda vitanda vyao,
nawe uliangalia uchi wao.
9Ulikwenda kwa Moleki
57.9 Moleki alikuwa mungu aliyekuwa anaabudiwa na Waamoni; pia alijulikana kama Malkomu, Maloki au Kemoshi wa Moabu
ukiwa na mafuta ya zeituni
na ukaongeza manukato yako.
Ukawatuma wajumbe wako mbali sana,
ukashuka kwenye kaburi
57.9 Kaburi hapa maana yake ni Kuzimu, kwa Kiebrania ni Sheol
lenyewe!
10Ulikuwa umechoshwa na njia zako zote,
lakini usingeliweza kusema,
‘Hakuna tumaini.’
Ulipata uhuisho wa nguvu zako,
kwa sababu hiyo hukuzimia.
11“Ni nani uliyemhofu hivyo na kumwogopa
hata ukaniambia uongo,
wala hukunikumbuka
au kutafakari hili moyoni mwako?
Si kwa sababu nimekuwa kimya muda mrefu
kwamba huniogopi?
12Nitaifunua haki yako na matendo yako,
nayo hayatakufaidia.
13Utakapolia kwa kuhitaji msaada,
sanamu zako ulizojikusanyia na zikuokoe!
Upepo utazipeperusha zote,
pumzi peke yake itazipeperusha,
Lakini mtu atakayenifanya kimbilio lake,
atairithi nchi
na kuumiliki mlima wangu mtakatifu.”

Faraja Kwa Wenye Majuto

14Tena itasemwa: “Jengeni, jengeni, itengenezeni njia!
Ondoeni vikwazo katika njia ya watu wangu.”
15Kwa maana hili ndilo asemalo Aliye juu,
yeye aliyeinuliwa sana,
yeye aishiye milele,
ambaye jina lake ni Mtakatifu:
“Ninaishi mimi mahali palipoinuka
tena palipo patakatifu,
tena pamoja na yeye aliye na roho iliyotubu
na mwenye roho ya unyenyekevu,
ili kuzihuisha roho za wanyenyekevu
na kuihuisha mioyo yao waliotubu.
16Sitaendelea kulaumu milele,
wala sitakasirika siku zote,
kwa kuwa roho ya mwanadamu
ingezimia mbele zangu:
yaani pumzi ya mwanadamu niliyemwumba.
17Nilighadhibika na tamaa yake ya dhambi;
nilimwadhibu, nikauficha uso wangu kwa hasira,
yeye bado aliendelea katika njia zake za tamaa.
18Nimeziona njia zake, lakini nitamponya,
nitamwongoza na kumrudishia upya faraja,
19nikiumba sifa katika midomo ya waombolezaji
katika Israeli.
Amani, amani, kwa wale walio mbali
na kwa wale walio karibu,”
asema BWANA. “Nami nitawaponya.”
20Bali waovu ni kama bahari ichafukayo,
ambayo haiwezi kutulia,
mawimbi yake hutupa takataka na matope.
21Mungu wangu asema,
“Hakuna amani kwa waovu.”


Copyright information for Neno