Isaiah 59

Dhambi, Toba Na Ukombozi

1Hakika mkono wa BWANA si mfupi hata usiweze kuokoa,
wala sikio lake si zito hata lisiweze kusikia.
2Lakini maovu yenu yamewatenga ninyi
na Mungu wenu,
dhambi zenu zimewaficha ninyi uso wake,
ili asisikie.
3Kwa maana mikono yenu imetiwa mawaa kwa damu
na vidole vyenu kwa hatia.
Midomo yenu imenena uongo,
nazo ndimi zenu zimenong'ona mambo maovu.
4Hakuna hata mmoja anayedai kwa haki;
hakuna hata mmoja
anayetetea shauri lake kwa haki.
Wanategemea mabishano matupu na kusema uongo,
huchukua mimba ya magomvi na kuzaa uovu.
5Huangua mayai ya nyoka wenye sumu kali
na kutanda wavu wa buibui.
Ye yote alaye mayai yao atakufa,
na wakati moja lianguliwapo,
nyoka mwenye sumu kali hutoka humo.
6Utando wao wa buibui haufai kwa nguo;
hawawezi kujifunika
kwa kile walichokitengeneza.
Matendo yao ni matendo maovu,
vitendo vya jeuri vipo mikononi mwao.
7Miguu yao hukimbilia kwenye dhambi,
ni myepesi kumwaga damu isiyo na hatia.
Mawazo yao ni mawazo mabaya;
uharibifu na maangamizi
huweka alama njia zao.
8Hawajui njia ya amani,
hakuna haki katika mapito yao.
Wamezigeuza kuwa njia za upotovu,
hakuna ye yote apitaye katika njia hizo
atakayeifahamu amani.
9Hivyo uadilifu uko mbali nasi,
nayo haki haitufikii.
Tunatazamia nuru, kumbe! yote ni giza,
tunatazamia mwanga,
lakini tunatembea katika giza kuu.
10Tunapapasa ukuta kama kipofu,
tunapapasa katika njia zetu
kama watu wasio na macho.
Adhuhuri tunajikwaa kama wakati wa gizagiza,
katikati ya wenye nguvu, tuko kama wafu.
11Wote tunanguruma kama dubu;
tunalia kwa uchungu
kwa maombolezo kama hua.
Tunatafuta haki, kumbe hakuna kabisa;
tunatafuta wokovu, lakini uko mbali.
12Kwa sababu makosa yetu ni mengi machoni pako,
na dhambi zetu zinashuhudia dhidi yetu.
Makosa yetu yako pamoja nasi daima,
nasi tunayatambua maovu yetu:
13Uasi na udanganyifu dhidi ya BWANA,
kumgeuzia Mungu wetu kisogo,
tukichochea udhalimu na maasi,
tukinena uongo ambao mioyo yetu imeuhifadhi.
14Hivyo uadilifu umerudishwa nyuma,
nayo haki inasimama mbali,
kweli imejikwaa njiani,
uaminifu hauwezi kuingia.
15Kweli haipatikani po pote,
na ye yote aepukaye uovu huwa mawindo.
BWANA alitazama naye akachukizwa
kwamba hapakuwepo haki.
16Aliona kuwa hakuwepo hata mtu mmoja,
akashangaa kwamba hakuwepo
hata mmoja wa kuingilia kati;
hivyo mkono wake mwenyewe
ndio uliomfanyia wokovu,
nayo haki yake mwenyewe
ndiyo iliyomtegemeza.
17Alivaa haki kama dirii kifuani mwake,
na chapeo ya wokovu kichwani mwake,
alivaa mavazi ya kisasi
naye akajifunga wivu kama joho.
18Kulingana na kile walichokuwa wametenda,
ndivyo atakavyolipa
ghadhabu kwa watesi wake
na kisasi kwa adui zake,
atavilipa tena visiwa sawa na wanavyostahili.
19Kuanzia magharibi, watu wataliogopa jina la BWANA
na kuanzia maawio ya jua,
watauheshimu utukufu wake.
Wakati adui atakapokuja kama mafuriko,
Roho wa BWANA atainua kiwango dhidi yake
na kumshinda kumfukuza.
20“Mkombozi atakuja Sayuni,
kwa wale wa uzao wa Yakobo
wanaozitubia dhambi zao,”
asema BWANA.

21

“Kwa habari yangu mimi, hili ni Agano langu nao,” asema BWANA. “Roho wangu, aliyeko juu yenu na maneno yangu ambayo nimeyaweka katika vinywa vyenu hayataondoka vinywani mwenu, wala kutoka vinywani mwa watoto wenu, wala kutoka vinywani mwa wazao wao kuanzia sasa na hata milele,” asema BWANA.

Copyright information for Neno