Isaiah 60

Utukufu Wa Sayuni

“Ondoka, angaza, kwa kuwa nuru yako imekuja
na utukufu wa BWANA umezuka juu yako.
Tazama, giza litaifunika dunia
na giza kuu litayafunika mataifa,
lakini BWANA atazuka juu yako
na utukufu wake utaonekana juu yako.
Mataifa wataijia nuru yako
na wafalme kuujia mwanga
wa mapambazuko yako.
“Inua macho yako na utazame pande zote:
Wote wanakusanyika na kukujia,
wana wako wanakuja toka mbali,
nao binti zako wanabebwa mikononi.
Ndipo utatazama na kutiwa nuru,
moyo wako utasisimka na kujaa furaha,
mali zilizo baharini zitaletwa kwako,
utajiri wa mataifa utakujilia.
Makundi ya ngamia yatajaa katika nchi yako,
ngamia vijana wa Midiani na Efa.
Nao wote watokao Sheba watakuja,
wakichukua dhahabu na uvumba
na kutangaza sifa za BWANA.
Makundi yote ya Kedari yatakusanyika kwako,
kondoo waume wa Nebayothi watakutumikia,
watakubalika kama sadaka juu ya madhabahu yangu,
nami nitalipamba Hekalu langu tukufu.
“Ni nani hawa warukao kama mawingu
kama hua kuelekea kwenye viota vyao?
Hakika visiwa vinanitazama,
merikebu za Tarshishi
60.9 Au: merikebu za biashara (ona pia 1 Fal 10:22; 22:48; 2 Nya 9:21; 20:36; Isa 2:16)
ndizo zinazotangulia,
zikiwaleta wana wenu kutoka mbali,
wakiwa na fedha na dhahabu zao,
kwa heshima ya BWANA, Mungu wenu,
yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli,
kwa maana amekujalia utukufu.
10 “Wageni watazijenga upya kuta zako,
na wafalme wao watakutumikia.
Ingawa katika hasira nilikupiga,
lakini katika upendeleo wangu
nitakuonyesha huruma.
11 Malango yako yatakuwa wazi siku zote,
kamwe hayatafungwa, mchana wala usiku,
ili kwamba watu wapate kukuletea utajiri wa mataifa:
wafalme wao wakiongoza
maandamano ya ushindi.
12 Kwa maana taifa au ufalme ule ambao hautakutumikia utaangamia;
utaharibiwa kabisa.
13 “Utukufu wa Lebanoni utakujilia,
msunobari, mvinje pamoja na mteashuri,
ili kupapamba mahali pangu patakatifu,
nami nitapatukuza mahali pa miguu yangu.
14 Wana wa wale waliokuonea
watakuja wakisujudu mbele yako,
wote wanaokudharau
watasujudu kwenye miguu yako
nao watakuita Mji wa BWANA,
Sayuni wa yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli.
15 “Ingawa umeachwa na kuchukiwa,
bila kuwapo na ye yote anayesafiri ndani yako,
nitakufanya kuwa fahari ya milele
na furaha ya vizazi vyote.
16 Utanyonya maziwa ya mataifa
na kunyonyeshwa matiti ya wafalme.
Ndipo utakapojua kwamba Mimi, BWANA, ni Mwokozi wako,
Mkombozi wako, niliye Mwenye Nguvu wa Yakobo.
17 Badala ya shaba nitakuletea dhahabu
na fedha badala ya chuma.
Badala ya mti nitakuletea shaba,
na chuma badala ya mawe.
Nitafanya amani kuwa mtawala wako
na haki kuwa mfalme wako.
18 Jeuri hazitasikika tena katika nchi yako,
wala maangamizi
au uharibifu ndani ya mipaka yako,
lakini utaita kuta zako Wokovu
na malango yako Sifa.
19 Jua halitakuwa tena nuru yako mchana,
wala mwangaza wa mwezi hautakuangazia,
kwa maana BWANA atakuwa nuru yako ya milele,
naye Mungu wako atakuwa utukufu wako.
20 Jua lako halitazama tena,
nao mwezi wako hautafifia tena;
BWANA atakuwa nuru yako milele,
nazo siku zako za huzuni zitakoma.
21 Ndipo watu wako wote watakuwa waadilifu
nao wataimiliki nchi milele.
Wao ni chipukizi nililolipanda,
kazi ya mikono yangu,
kwa ajili ya kuonyesha utukufu wangu.
22 Aliye mdogo kwenu atakuwa elfu,
mdogo kuliko wote
atakuwa taifa lenye nguvu.
Mimi ndimi BWANA;
katika wakati wake
nitayatimiza haya upesi.”
Copyright information for Neno