Isaiah 63

Siku Ya Mungu Ya Kisasi Na Ukombozi

1Ni nani huyu anayekuja kutoka Edomu,
kutoka Bosra, mwenye mavazi
yaliyotiwa madoa mekundu?
Ni nani huyu, aliyevikwa joho la kifahari,
anayetembea kwa ukuu wa nguvu zake?
“Mimi ndimi, nisemaye katika haki,
mwenye nguvu wa kuokoa.”
2Kwa nini mavazi yako ni mekundu,
kama ya yule akanyagaye shinikizo la zabibu?
3“Nimekanyaga shinikizo la zabibu peke yangu;
kutoka katika mataifa
hakuna mtu awaye yote
aliyekuwa pamoja nami.
Nimewaponda mataifa kwa miguu katika hasira yangu
na kuwakanyaga chini
katika ghadhabu yangu;
damu yao ilitia matone matone kwenye mavazi yangu
na kutia madoa nguo zangu zote.
4Kwa kuwa siku ya kisasi ilikuwa moyoni mwangu,
mwaka wa ukombozi wangu umefika.
5Nilitazama, lakini hakuwepo ye yote wa kunisaidia,
nilishangaa kwa kuwa hakuwepo
ye yote aliyetoa msaada;
hivyo mkono wangu wenyewe ndio ulionifanyia wokovu,
na ghadhabu yangu mwenyewe
ndiyo iliyonitegemeza.
6Nilikanyaga mataifa kwa miguu katika hasira yangu,
katika ghadhabu yangu niliwalewesha
na kumwaga damu yao juu ya ardhi.”

Kusifu Na Kuomba

7Nitasimulia juu ya wema wa BWANA,
kwa ajili ya matendo ambayo
kwayo apaswa kusifiwa,
sawasawa na yote ambayo BWANA
ametenda kwa ajili yetu:
naam, mambo mengi mema aliyoyatenda
kwa ajili ya nyumba ya Israeli,
sawasawa na huruma zake
na wema wake mwingi.
8Alisema, “Hakika wao ni watu wangu,
wana ambao hawatanidanganya”;
kisha akawa Mwokozi wao.
9Katika taabu zao zote naye alitaabika
na malaika wa uso wake akawaokoa.
Katika upendo wake na rehema zake aliwakomboa,
akawainua na kuwachukua siku zote zilizopita.
10Lakini waliasi
na kumhuzunisha Roho Mtakatifu wake.
Hivyo aligeuka na kuwa adui yao
na yeye mwenyewe akapigana dhidi yao.
11Ndipo watu wake wakazikumbuka siku zilizopita,
siku za Mose na watu wake:
yuko wapi yeye aliyewaleta kupitia katikati ya bahari,
pamoja na wachungaji wa kundi lake?
Yuko wapi yule aliyeweka
Roho wake Mtakatifu katikati yao,
12aliyetuma mkono wake uliotukuka wenye nguvu
kuwa katika mkono wa kuume wa Mose,
aliyegawa maji ya bahari mbele yao,
ili kujipatia jina milele,
13aliyewaongoza kupitia kwenye vilindi?
Kama farasi katika nchi iliyo wazi,
wao hawakujikwaa,
14kama ng'ombe washukao bondeni kwenye malisho,
walipewa pumziko na Roho wa BWANA.
Hivi ndivyo ulivyowaongoza watu wako
ili kujipatia mwenyewe jina tukufu.
15Tazama chini kutoka mbinguni ukaone
kutoka katika kiti chako cha enzi
kilichoinuliwa juu, kitakatifu na kitukufu.
Uko wapi wivu wako na uweza wako?
Umetuzuilia wema wako na huruma zako.
16Lakini wewe ni Baba yetu,
ingawa Abrahamu hatufahamu sisi
wala Israeli hatutambui;
wewe, Ee BWANA, ni Baba yetu,
Mkombozi wetu tangu zamani za kale
ndilo jina lako.
17Ee BWANA,, kwa nini unatuacha tuende mbali na njia zako
na kuifanya mioyo yetu migumu
hata hatukukuheshimu?
Rudi kwa ajili ya watumishi wako,
yale makabila ambayo ni urithi wako.
18Kwa maana kwa muda mfupi watu wako walimiliki
mahali pako patakatifu,
lakini sasa adui zetu wamepakanyaga
mahali patakatifu pako.
19Sisi ni watu wako tangu zamani;
lakini tumekuwa kama wale ambao
hujawatawala kamwe,
kama wale ambao
hawajaitwa kwa jina lako.
Copyright information for Neno