James 5

Onyo Kwa Matajiri

1Basi sikilizeni, ninyi matajiri, lieni na kuomboleza kwa ajili ya hali mbaya sana inayowajia. 2Utajiri wenu umeoza na mavazi yenu yameliwa na nondo. 3Dhahabu yenu na fedha yenu vimeliwa na kutu. Kutu yake itashuhudia dhidi yenu nayo itaila miili yenu kama vile moto. Mmejiwekea hazina kwa ajili ya siku za mwisho. 4Angalieni! Ule ujira wa vibarua waliolima mashamba yenu mliouzuia kwa hila unapiga kelele dhidi yenu na vilio vya wavunaji vimefika masikioni mwa Bwana Mwenye Nguvu Zote.
5.4 Bwana Mwenye Nguvu Zote hapa ni jina la Kiebrania Jehova Sabaoth (yaani Bwana wa Majeshi; pia Isa 1:9 na War 9:29)
5Mmeishi duniani kwa anasa na kwa starehe, mmejinenepesha tayari kwa siku ya kuchinjwa. 6Mmewahukumu na kuwaua watu wenye haki, ambao walikuwa hawapingani nanyi.

Uvumilivu Katika Mateso

7Kwa hiyo, ndugu zangu, vumilieni hadi kuja kwake Bwana. Angalieni jinsi mkulima angojavyo ardhi itoe mavuno yake yaliyo ya thamani na jinsi anavyovumilia kwa ajili ya kupata mvua za kwanza na za mwisho. 8Ninyi nanyi vumilieni tena simameni imara, kwa sababu kuja kwa Bwana kumekaribia. 9Ndugu zangu, msinung'unikiane msije mkahukumiwa. Hakimu amesimama mlangoni!

10Ndugu zangu, waangalieni manabii walionena kwa Jina la Bwana, ili kuwa mfano wa uvumilivu katika kukabiliana na mateso. 11Kama mnavyojua, tunawahesabu kuwa wamebarikiwa wale waliovumilia. Mmesikia habari za uvumilivu wake Ayubu na mmeona kile ambacho hatimaye Bwana alimtendea. Bwana ni mwingi wa huruma naye amejaa rehema.

12Zaidi ya yote, ndugu zangu, msiape, ama kwa mbingu, au kwa dunia au kwa kitu kingine cho chote. “Ndiyo” yenu na iwe ndiyo, na “Hapana” yenu iwe hapana, la sivyo mtahukumiwa.

Maombi Ya Imani

13Je, mtu ye yote miongoni mwenu amepatwa na taabu? Basi inampasa aombe. Je, kuna ye yote mwenye furaha? Basi na aimbe nyimbo za kusifu. 14Je, kuna ye yote miongoni mwenu aliye mgonjwa? Basi inampasa awaite wazee wa kanisa wamwombee na kumpaka mafuta kwa Jina la Bwana. 15Kule kuomba kwa imani kutamwokoa huyo mgonjwa, naye Bwana atamwinua na kama ametenda dhambi, atasamehewa. 16Kwa hiyo ungamianeni makosa yenu ninyi kwa ninyi na kuombeana ili mpate kuponywa. Maombi ya mwenye haki yana nguvu tena yanafaa sana.

17Eliya alikuwa mwanadamu kama sisi. Akaomba kwa bidii kwamba mvua isinyeshe nayo haikunyesha juu ya nchi kwa muda wa miaka mitatu na miezi sita. 18Kisha akaomba tena, mbingu zikatoa mvua nayo ardhi ikatoa mazao yake.

19Ndugu zangu, ye yote miongoni mwenu akipotoka na kuicha kweli, naye akarejezwa na mtu mwingine, 20hamna budi kujua kwamba ye yote amrejezaye mwenye dhambi kutoka katika upotovu wake, ataiokoa roho ya huyo mwenye dhambi kutoka katika mauti na kusitiri wingi wa dhambi.

Copyright information for Neno