Jeremiah 10

Mungu Na Sanamu

1Sikieni lile ambalo BWANA, anena nanyi Ee nyumba ya Israeli. 2Hili ndilo asemalo BWANA: “Usijifunze njia za mataifa
wala usitishwe na ishara katika anga,
ingawa mataifa yanatishwa nazo.
3Kwa maana desturi za mataifa hazina maana,
wanakata mti kutoka msituni
na fundi anauchonga kwa patasi.
4Wanaparemba kwa fedha na dhahabu,
wanakikaza kwa nyundo
na misumari ili kisitikisike.
5Sanamu zao ni kama sanamu
iliyowekwa shambani kutishia ndege
kwenye shamba la matango,
nazo haziwezi kuongea; sharti zibebwe
kwa sababu haziwezi kutembea.
Usiziogope; haziwezi kudhuru
wala kutenda lo lote jema.”
6Hakuna aliye kama wewe, Ee BWANA;
wewe ni mkuu,
jina lako ni lenye nguvu katika uweza.
7Ni nani ambaye haimpasi kukuheshimu wewe,
Ee mfalme wa mataifa?
Hii ni stahili yako.
Miongoni mwa watu wote wenye hekima
katika mataifa na katika falme zao zote,
hakuna aliye kama wewe.
8Wote hawana akili tena ni wapumbavu,
wanafundishwa na sanamu za miti
zisizofaa lo lote.
9Huleta fedha iliyofuliwa kutoka Tarshishi
na dhahabu kutoka Ufazi.
Kile ambacho fundi na sonara wametengeneza
huvikwa mavazi ya rangi
ya samawi na urujuani:
vyote vikiwa vimetengenezwa
na mafundi stadi.
10Lakini BWANA ni Mungu wa kweli,
yeye ndiye Mungu aliye hai,
Mfalme wa milele.
Akiwa amekasirika, dunia hutetemeka,
mataifa hayawezi kustahimili hasira yake.11“Waambie hivi: ‘Miungu hii, ambayo haikuumba mbingu na dunia, itaangamia kutoka duniani na kutoka chini ya mbingu.’ ” 12Lakini Mungu aliiumba dunia kwa uweza wake,
akaufanya ulimwengu kwa hekima yake
na kwa ufahamu wake akazitandaza mbingu.
13Atoapo sauti yake, maji yaliyo katika mbingu hunguruma;
huyafanya mawingu yainuke
kutoka miisho ya dunia.
Hupeleka umeme wa radi pamoja na mvua
naye huleta upepo kutoka katika ghala zake.
14Kila mmoja ni mjinga na hana maarifa,
kila sonara ameaibishwa na sanamu zake.
Vinyago vyake ni madanganyo,
wala havina pumzi ndani yake.
15Havina maana, ni vitu vya mzaha tu,
hukumu yao itakapokuja, wataangamia.
16Yeye aliye Fungu la Yakobo si kama hivi,
kwani ndiye Muumba wa vitu vyote,
pamoja na Israeli, kabila la urithi wake:
BWANA Mwenye Nguvu Zote ndilo jina lake.


Maangamizi Yajayo

17Kusanyeni mali na vitu vyenu muondoke katika nchi hii,
enyi mnaoishi katika hali ya kuzingirwa na jeshi.
18Kwa kuwa hili ndilo asemalo BWANA:
“Wakati huu, nitawatupa nje kwa nguvu
wote waishio katika nchi hii;
nitawataabisha ili waweze kutekwa.”
19Ole wangu mimi kwa ajili ya kuumia kwangu!
Jeraha langu ni kubwa!
Lakini nilisema,
“Kweli hii ni adhabu yangu,
nami sharti nistahimili.”
20Hema langu limeangamizwa;
kamba zake zote zimekatwa.
Wana wangu wametekwa
na hawapo tena;
hakuna hata mmoja aliyebaki
kulisimika hema langu
wala wa kusimamisha kibanda changu.
21Wachungaji hawana akili
wala hawamulizi BWANA,
hivyo hawastawi
na kundi lao lote la kondoo
na mbuzi limetawanyika.
22Sikilizeni! Taarifa inakuja:
ghasia kubwa kutoka nchi ya kaskazini!
Hii itafanya miji ya Yuda kuwa ukiwa,
makao ya mbweha.

Maombi Ya Yeremia

23Ninajua, Ee BWANA, kwamba maisha ya mwanadamu
si yake mwenyewe;
hawezi kuziongoza hatua zake mwenyewe.
24Unirudi, Ee BWANA,
lakini kwa kipimo cha haki:
si katika hasira yako,
usije ukaniangamiza.
25Umwage ghadhabu yako juu ya mataifa
yale wasiokujua wewe,
juu ya mataifa yale wasioliitia jina lako.
Kwa kuwa wamemwangamiza Yakobo;
wamemwangamiza kabisa
na kuiharibu nchi yake.
Copyright information for Neno