Jeremiah 15

Adhabu Isiyoepukika

Kisha BWANA akaniambia: “Hata kama Mose na Samweli wangesimama mbele zangu, moyo wangu usingewaelekea watu hawa. Waondoe mbele za macho yangu! Waache waende! Nao kama wakikuuliza, ‘Tuende wapi?’ Waambie, ‘Hili ndilo BWANA asemalo: “ ‘Wale waliowekwa kwa ajili ya kufa, wakafe;
waliowekwa kwa ajili ya upanga, kwa upanga;
waliowekwa kwa ajili ya njaa, kwa njaa:
waliowekwa kwa ajili ya kutekwa, watekwe.’ ”BWANA asema, “Nitatuma aina nne ya waharabu dhidi yao, upanga ili kuua na mbwa ili wakokote mbali, ndege wa angani na wanyama wa nchi ili kula na kuangamiza. Nitawafanya wawe machukizo kwa falme zote za dunia kwa sababu ya kile alichofanya Manase mwana wa Hezekia mfalme wa Yuda huko Yerusalemu. “Ni nani atakayekuhurumia, Ee Yerusalemu?
Ni nani atakayeomboleza kwa ajili yako?
Ni nani atakayesimama ili kuuliza
kuhusu hali yako?
Umenikataa mimi,” asema BWANA.
“Unazidi kukengeuka.
Hivyo nitanyosha mkono wangu juu yako na kukuangamiza,
siwezi kuendelea kukuonea huruma.
Nitawapepeta kwa uma wa kupepetea
kwenye malango ya miji katika nchi.
Nitaleta msiba na maangamizi juu ya watu wangu,
kwa maana hawajabadili njia zao.
Nitawafanya wajane wao kuwa wengi
kuliko mchanga wa bahari.
Wakati wa adhuhuri nitamleta mharabu
dhidi ya mama wa vijana wao waume;
kwa ghafula nitaleta juu yao
maumivu makuu na hofu kuu.
Mama mwenye watoto saba atazimia
na kupumua pumzi yake ya mwisho.
Jua lake litatua kungali bado mchana,
atatahayarika na kufedheheka.
Wale wote waliobaki nitawaua kwa upanga
mbele ya adui zao,”
asema BWANA.

10 Ole wangu, mama yangu, kwamba ulinizaa,
mtu ambaye ulimwengu wote
unashindana na kugombana naye!
Sikukopa wala sikukopesha,
lakini kila mmoja ananilaani.11 BWANA akasema, “Hakika nitakuokoa kwa kusudi jema,
hakika nitawafanya adui zako wakuombe msaada
nyakati za maafa na nyakati za dhiki.
12 “Je, mtu aweza kuvunja chuma,
chuma kitokacho kaskazini na shaba?
13 Utajiri wako na hazina zako nitavitoa kuwa nyara,
bila gharama,
kwa sababu ya dhambi zako zote
katika nchi yako yote.
14 Nitakufanya uwe mtumwa wa adui zako
katika nchi usiyoijua,
kwa kuwa katika hasira yangu moto umewashwa
utakaowaka juu yako daima.”
15 Wewe unajua, Ee BWANA,
unikumbuke na unitunze mimi.
Lipiza kisasi juu ya watesi wangu.
Kwa uvumilivu wako usiniondolee mbali;
kumbuka jinsi ninavyoshutumiwa.
16 Maneno yako yalipokuja, niliyala;
yakawa shangwe yangu
na furaha ya moyo wangu,
kwa kuwa nimeitwa kwa jina lako,
Ee BWANA Mungu Mwenye Nguvu Zote.
17 Kamwe sikuketi katika kundi la wafanyao sherehe,
wala kamwe sikujifurahisha pamoja nao;
niliketi peke yangu kwa sababu mkono wako
ulikuwa juu yangu
na wewe ulikuwa umenijaza hasira.
18 Kwa nini maumivu yangu hayakomi
na jeraha langu ni la kuhuzunisha
wala haliponyeki?
Je, utakuwa kwangu kama kijito cha udanganyifu,
kama chemchemi iliyokauka?19 Kwa hiyo hili ndilo asemalo BWANA: “Kama ukitubu, nitakurejeza
ili uweze kunitumikia;
kama ukinena maneno yenye maana,
wala si ya upuzi,
utakuwa mnenaji wangu.
Watu hawa ndio watakaokugeukia,
wala si wewe utakayewageukia wao.
20 Nitakufanya wewe uwe ukuta kwa watu hawa,
ngome ya ukuta wa shaba;
watapigana nawe
lakini hawatakushinda,
kwa maana mimi niko pamoja nawe
kukuponya na kukuokoa,”
asema BWANA.

21 “Nitakuokoa kutoka katika mikono ya waovu,
na kukukomboa kutoka katika makucha ya watu wakatili.”


Copyright information for Neno