Jeremiah 17

Dhambi Ya Yuda Na Adhabu yake

1“Dhambi ya Yuda imechorwa kwa kalamu ya chuma,
imeandikwa kwa ncha ya almasi,
kwenye vibao vya mioyo yao
na kwenye pembe za madhabahu zao.
2Hata watoto wao wanakumbuka madhabahu zao
na nguzo za Ashera
17.2 Ashera ni mungu mke aliyekuwa anaabudiwa na Wakaanani

kandokando ya miti iliyotanda
na juu ya vilima virefu.
3Mlima wangu katika nchi pamoja na utajiri
na hazina zako zote
nitazitoa ziwe nyara,
pamoja na mahali pako pa juu pa kuabudia miungu
kwa sababu ya dhambi katika nchi yako yote.
4Kwa kosa lako mwenyewe utaupoteza
urithi niliokupa.
Nitakufanya mtumwa wa adui zako
katika nchi usiyoijua,
kwa kuwa umeiwasha hasira yangu,
nayo itawaka milele.”
5

Hili ndilo asemalo BWANA: “Amelaaniwa yeye amtegemeaye mwanadamu,
ategemeaye mwenye mwili
kwa ajili ya nguvu zake,
ambaye moyo wake
umemwacha BWANA.
6Atakuwa kama kichaka cha jangwani;
hataona mafanikio yatakapokuja.
Ataishi katika sehemu zisizo na maji,
katika nchi ya chumvi ambapo
hakuna ye yote aishiye humo.
7“Lakini amebarikiwa mtu ambaye tumaini lake ni katika BWANA,
ambaye matumaini yake ni katika BWANA.
8Atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji
uenezao mizizi yake
karibu na kijito cha maji.
Hauogopi wakati wa joto ujapo;
majani yake ni mabichi daima.
Hauna hofu katika mwaka wa ukame
na hautaacha kuzaa matunda.”
9Moyo ni mdanganyifu kuliko vitu vyote,
ni mwovu kupita kiasi.
Ni nani awezaye kuujua?
10“Mimi BWANA huchunguza moyo
na kuzijaribu nia,
kumlipa mtu kwa kadiri ya mwenendo wake,
kwa kadiri ya matendo yake yanavyostahili.”
11Kama kware aanguaye mayai asiyoyataga,
ndivyo alivyo mtu apataye mali
kwa njia zisizo za haki.
Maisha yake yafikapo katikati, siku zitamwacha,
na mwishoni atabainika kuwa mpumbavu.
12Kiti cha enzi kilichotukuzwa, kilichoinuliwa tangu mwanzo,
ndiyo sehemu yetu ya mahali patakatifu.
13Ee BWANA, uliye tumaini la Israeli,
wote wakuachao wataaibika.
Wale wanaogeukia mbali nawe wataandikwa mavumbini
kwa sababu wamemwacha BWANA,
chemchemi ya maji yaliyo hai.
14Uniponye, Ee BWANA, nami nitaponyeka;
uniokoe nami nitaokoka,
kwa maana wewe ndiwe ninayekusifu.
15Wao huendelea kuniambia,
“Liko wapi neno la BWANA?
Sasa na litimie!”
16Sijakukimbia na kuacha kuwa mchungaji wako;
unajua sijaitamani siku ya kukata tamaa.
Kile kipitacho midomoni mwangu
ki wazi mbele yako.
17Usiwe kwangu kitu cha kunitia hofu kuu;
wewe ndiwe kimbilio langu katika siku ya maafa.
18Watesi wangu na waaibishwe,
lakini nilinde mimi nisiaibike;
wao na watiwe hofu kuu,
lakini unilinde mimi na hofu kuu.
Uwaletee siku ya maafa;
waangamize kwa maangamizi maradufu.


Kuiadhimisha Sabato

19Hili ndilo BWANA aliloniambia: “Nenda ukasimame kwenye lango la watu, mahali ambako wafalme wa Yuda huingilia na kutokea, simama pia kwenye malango mengine yote ya Yerusalemu. 20Waambie, ‘Sikieni neno la BWANA, Enyi wafalme wa Yuda nanyi watu wote wa Yuda na kila mmoja aishiye Yerusalemu apitaye katika malango haya. 21Hili ndilo asemalo BWANA: Jihadharini msije mkabeba mzigo siku ya Sabato, wala kuingiza mzigo kupitia malango ya Yerusalemu. 22Msitoe mizigo nje ya nyumba zenu wala kufanya kazi yo yote wakati wa Sabato, lakini itakaseni siku ya Sabato, kama nilivyowaamuru baba zenu. 23Hata hivyo hawakusikiliza wala kujali, walishupaza shingo zao na hawakutaka kusikia wala kukubali marudi. 24Lakini mkiwa waangalifu katika kunitii, asema BWANA, nanyi msipoleta mzigo wo wote kupitia malango ya mji huu wakati wa Sabato, lakini mkaitakasa siku ya Sabato kwa kutofanya kazi siku hiyo, 25ndipo wafalme wakaao juu ya kiti cha enzi cha Daudi, wataingia kupitia malango ya mji huu pamoja na maafisa wao. Wao na maafisa wao watakuja wakiwa wamepanda magari na farasi, wakiandamana na watu wa Yuda na wale waishio Yerusalemu, nao mji huu utakaliwa na watu daima. 26Watu watakuja kutoka miji ya Yuda na vijiji vinavyoizunguka Yerusalemu, kutoka nchi ya Benyamini na chini ya vilima vya magharibi, kutoka nchi ya vilima na Negebu, wakileta sadaka za kuteketezwa na dhabihu, sadaka za nafaka, uvumba na sadaka za shukrani kwenye nyumba ya BWANA. 27Lakini ikiwa hamtanitii mimi kwa kuitakasa Sabato na kwa kutochukua mzigo wo wote mnapoingia katika malango ya Yerusalemu wakati wa Sabato, basi nitawasha moto usiozimika katika malango ya Yerusalemu utakaoteketeza ngome zake.’ ”

Copyright information for Neno