Jeremiah 19

Gudulia La Udongo Lililovunjika

1Hili ndilo asemalo BWANA: “Nenda ukanunue gudulia la udongo kutoka kwa mfinyanzi. Wachukue baadhi ya wazee wa watu na wa makuhani 2na mtoke mwende mpaka kwenye Bonde la Ben-Hinomu, karibu na ingilio la Lango la Vigae. Huko tangaza maneno ninayokuambia, 3nawe useme, ‘Sikieni neno la BWANA, enyi wafalme wa Yuda na watu wa Yerusalemu. Hili ndilo BWANA Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli asemalo: Sikilizeni! Nitaleta maafa mahali hapa ambayo yatafanya masikio ya kila mmoja atakayesikia habari zake yawashe. 4Kwa kuwa wameniacha na kupafanya mahali hapa kuwa pa miungu ya kigeni, wameiteketezea sadaka miungu ambayo wao wala baba zao wala wafalme wa Yuda kamwe hawakuijua, nao wamelijaza eneo hili kwa damu isiyo na hatia. 5Wamejenga mahali pa juu pa kuabudia miungu pa Baali ili kuteketeza wana wao katika moto kama sadaka kwa Baali, kitu ambacho sikukiamuru wala kukitaja, wala hakikuingia akilini mwangu. 6Hivyo jihadharini, siku zinakuja, asema BWANA, wakati watu hawatapaita tena mahali hapa Tofethi ama Bonde la Ben-Hinomu, bali Bonde la Machinjo.

7“ ‘Nitaiharibu mipango ya Yuda na Yerusalemu mahali hapa. Nitawafanya waanguke kwa upanga mbele ya adui zao, katika mikono ya wale watafutao uhai wao, nami nitaitoa mizoga yao kuwa chakula cha ndege wa angani na wanyama wa nchi. 8Nitauharibu mji huu na kuufanya kitu cha kudharauliwa, wote wapitao karibu watashangaa na wataudhihaki kwa ajili ya majeraha yake yote. 9Nitawafanya wao kula nyama ya wana wao na binti zao, kila mmoja atakula nyama ya mwenzake wakati wa dhiki ya kuzungukwa na jeshi lililowekwa juu yao na adui wanaotafuta uhai wao.’

10“Kisha livunje lile gudulia wakati wale walio pamoja nawe wakiwa wanaangalia, 11uwaambie, ‘Hili ndilo BWANA Mwenye Nguvu Zote asemalo: Nitalivunja taifa hili na mji huu kama gudulia hili la mfinyanzi lilivyovunjwa, nalo haliwezi kutengenezeka tena. Watawazika waliokufa huko Tofethi hata isiwepo nafasi zaidi. 12Hivi ndivyo nitakavyopafanya mahali hapa na kwa wale waishio ndani yake, asema BWANA. Nitaufanya mji huu kama Tofethi. 13Nyumba zilizoko Yerusalemu na zile za wafalme wa Yuda zitatiwa unajisi kama mahali hapa, yaani, Tofethi. Nyumba zote ambazo walifukiza uvumba juu ya mapaa yake kwa jeshi lote la angani na kumimina dhabihu ya kinywaji kwa miungu mingine.’ ”

14Kisha Yeremia akarudi kutoka Tofethi, mahali ambapo BWANA alikuwa amemtuma kutoa unabii, akasimama katika ua wa Hekalu la BWANA na kuwaambia watu wote, 15“Hili ndilo BWANA Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Sikilizeni! Nitaleta juu ya mji huu pamoja na vijiji vinavyouzunguka kila maafa niliyosema dhidi yake, kwa sababu wamekuwa na shingo ngumu na hawakuyasikiliza maneno yangu.’ ”

Copyright information for Neno