Jeremiah 20

Yeremia Ateswa Na Pashuri

Ikawa kuhani Pashuri mwana wa Imeri, mkuu wa maafisa wa Hekalu la BWANA, alipomsikia Yeremia akitoa unabii juu ya mambo haya, akaamuru Yeremia nabii apigwe na kufungwa katika mkatale katika Lango la Juu la Benyamini katika Hekalu la BWANA. Siku ya pili Pashuri alipomwachia kutoka kwenye mkatale, Yeremia akamwambia, “BWANA hakukuita jina lako kuwa Pashuri bali Magor-Misabibu
20.3 Magor-Misabibu maana yake hapa ni Vitisho pande zote
.
Kwa kuwa hili ndilo asemalo BWANA: ‘Nitakufanya kuwa hofu kuu kwako wewe mwenyewe na rafiki zako wote, kwa macho yako mwenyewe utawaona wakianguka kwa upanga wa adui zao. Nitawatia Wayahudi wote mikononi mwa mfalme wa Babeli, ambaye atawachukua na kuwapeleka Babeli ama awaue kwa upanga. Nitatia utajiri wote wa mji huu kwa adui zao, yaani, mazao yao yote, vitu vyao vyote vya thamani na hazina zote za wafalme wa Yuda. Watavitwaa kwa nyara na kuvipeleka Babeli. Nawe Pashuri pamoja na wote waishio katika nyumba yako mtakwenda uhamishoni Babeli. Mtafia humo na kuzikwa, wewe na rafiki zako wote ambao umewatabiria uongo.’ ”

Malalamiko Ya Yeremia

Ee BWANA, umenidanganya,
nami nikadanganyika;
wewe una nguvu kuliko mimi,
nawe umenishinda.
Ninadharauliwa mchana kutwa,
kila mmoja ananidhihaki.
Kila ninenapo, ninapiga kelele
nikitangaza ukatili na uharibifu.
Kwa hiyo neno la BWANA limeniletea matukano
na mashutumu mchana kutwa.
Lakini kama nikisema, “Sitamtaja
wala kusema tena kwa jina lake,”
neno lake linawaka ndani ya moyo wangu kama moto,
moto uliofungwa ndani ya mifupa yangu.
Nimechoka sana kwa kulizuia ndani mwangu;
kweli, siwezi kujizuia.
10 Ninasikia minong'ono mingi,
“Hofu iko pande zote!
Mshitakini! Twendeni tumshitaki!”
Rafiki zangu wote wananisubiri niteleze,
wakisema,
“Labda atadanganyika;
kisha tutamshinda
na kulipiza kisasi juu yake.”
11 Lakini BWANA yu pamoja nami
kama shujaa mwenye nguvu;
hivyo washitaki wangu watajikwaa
na kamwe hawatashinda.
Watashindwa, nao wataaibika kabisa;
kukosa adabu kwao hakutasahauliwa.
12 Ee BWANA Mwenye Nguvu Zote,
wewe umjaribuye mwenye haki
na kupima moyo na nia,
na nione ukilipiza kisasi juu yao,
kwa maana kwako
nimeliweka shauri langu.
13 Mwimbieni BWANA!
Mpeni BWANA sifa!
Huokoa uhai wa mhitaji
kutoka mikononi mwa waovu.
14 Ilaaniwe siku niliyozaliwa!
Nayo isibarikiwe ile siku
mama yangu aliyonizaa!
15 Alaaniwe mtu yule aliyemletea baba yangu habari,
yule aliyemfanya afurahi sana, akisema,
“Mtoto amezaliwa kwako,
tena mtoto wa kiume!”
16 Mtu huyo na awe kama miji ile
ambayo BWANA Mungu
aliiangamiza bila huruma.
Yeye na asikie maombolezo asubuhi
na kilio cha vita wakati wa adhuhuri.
17 Kwa sababu hakuniua nikiwa tumboni,
hivyo mama yangu angekuwa kaburi langu,
nalo tumbo lake la uzazi
lingebaki kuwa kubwa daima.
18 Kwa nini basi nilitoka tumboni
ili kuona taabu na huzuni
na kuzimaliza siku zangu katika aibu?
Copyright information for Neno