Jeremiah 26

Yeremia

Mwanzoni mwa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda, neno hili lilikuja kutoka kwa BWANA: “Hili ndilo BWANA asemalo: Simama katika ua wa nyumba ya BWANA na useme na watu wote wa miji ya Yuda wanaokuja kuabudu katika nyumba ya BWANA. Waambie kila kitu nitakachokuamuru, usipunguze neno. Huenda watasikiliza na kila mmoja akageuka kutoka katika njia yake mbaya. Kisha nitawahurumia na kuacha kuwaletea maafa niliyokuwa ninapanga kwa sababu ya maovu waliyofanya. Waambie, ‘Hili ndilo asemalo BWANA: Ikiwa hamtanisikiliza na kuifuata sheria yangu ambayo nimeiweka mbele yenu, nanyi ikiwa hamtayasikiliza maneno ya watumishi wangu manabii, ambao nimewatuma kwenu tena na tena (ijapokuwa hamkuwasikiliza), ndipo nitaifanya nyumba hii kama Shilo na mji huu kuwa kitu cha kulaaniwa na mataifa yote ya dunia.’ ”

Makuhani, manabii na watu wote wakamsikia Yeremia akiyasema maneno haya ndani ya nyumba ya BWANA. Lakini mara tu Yeremia alipomaliza kuwaambia watu kila kitu BWANA alichomwamuru kukisema, makuhani, manabii na watu wote walimkamata wakisema, “Ni lazima ufe! Kwa nini unatoa unabii katika jina la BWANA kwamba nyumba hii itakuwa kama Shilo na mji huu utakuwa ukiwa na kuachwa tupu?” Nao watu wote wakamkusanyikia na kumzunguka Yeremia ndani ya nyumba ya BWANA.

10 Maafisa wa Yuda waliposikia kuhusu mambo haya, wakapanda kutoka katika jumba la kifalme wakaenda katika nyumba ya BWANA na kushika nafasi zao kwenye ingilio la Lango Jipya la nyumba ya BWANA. 11 Kisha makuhani na manabii wakawaambia maafisa pamoja na watu wote, “Mtu huyu anastahili ahukumiwe kifo kwa sababu ametoa unabii mabaya dhidi ya mji huu. Mmesikia kwa masikio yenu wenyewe!”

12 Kisha Yeremia akawaambia maafisa wote na watu wote: “BWANA amenituma kutoa unabii dhidi ya nyumba hii na mji huu mambo yote mliyoyasikia. 13 Sasa tengenezeni njia zenu na matendo yenu na kumtii BWANA Mungu wenu. Ndipo BWANA atawahurumia na kuacha kuleta maafa aliyokuwa ameyatamka dhidi yenu. 14 Lakini kwa habari yangu mimi, niko mikononi mwenu, nifanyieni lo lote mnaloona kuwa ni jema na la haki. 15 Hata hivyo, jueni kwa hakika, ikiwa mtaniua, mtakuwa mmejipatia dhambi kwa damu isiyo na hatia juu yenu wenyewe na juu ya mji huu na wote wanaoishi ndani yake, kwa maana ni kweli BWANA amenituma kwenu ili niseme maneno haya yote masikioni mwenu.”

16 Kisha maafisa na watu wote wakawaambia makuhani na manabii, “Mtu huyu asihukumiwe kifo! Amesema nasi katika jina la BWANA, Mungu wetu.”

17 Baadhi ya wazee wa nchi wakasogea mbele wakaliambia kusanyiko lote la watu, 18 “Mika wa Moreshethi alitoa unabii katika siku za Hezekia mfalme wa Yuda. Akawaambia watu wote wa Yuda, ‘Hili ndilo asemalo BWANA Mwenye Nguvu Zote: “ ‘Mji wa Sayuni utalimwa kama shamba,
Yerusalemu utakuwa lundo
la kifusi cha changarawe,
kilima cha Hekalu kitakuwa kichuguu
kilichoota vichaka.’


19 Je, Hezekia mfalme wa Yuda au mtu mwingine ye yote katika Yuda alimhukumu Mika kufa? Je, Hezekia hakumcha BWANA na kuhitaji msaada wake? Je, BWANA hakuwahurumia na akaacha kuleta maafa aliyokuwa ametamka dhidi yao? Tunakaribia sana kujiletea maangamizo ya kutisha sisi wenyewe!”

20 (Wakati huu, Uria mwana wa Shemaya kutoka mji wa Kiriath-Yearimu alikuwa mtu mwingine aliyetoa unabii kwa jina la BWANA; alitoa unabii juu ya mambo yaliyofanana na haya dhidi ya mji huu na nchi hii kama alivyofanya Yeremia. 21 Mfalme Yehoyakimu na wakuu wake wote na maafisa waliposikia maneno yake, mfalme alitafuta kumwua. Lakini Uria alipata habari na kwa kuogopa akakimbilia Misri. 22 Hata hivyo, Mfalme Yehoyakimu alimtuma Elnathani mwana wa Akbori huko Misri, pamoja na watu wengine ili kwenda kumkamata Uria. 23 Wakamrudisha Uria kutoka Misri na kumpeleka kwa Mfalme Yehoyakimu, ambaye alimwua kwa upanga na mwili wake kutupwa kwenye eneo la makaburi ya watu wasio na cheo.)

24 Zaidi ya hayo, Ahikamu mwana wa Shefani akamuunga mkono Yeremia, kwa hiyo hakutiwa tena mikononi mwa watu ili auawe.

Copyright information for Neno