Jeremiah 29

Barua Kwa Watu Wa Uhamishoni

Haya ndiyo maneno ya ile barua ambayo nabii Yeremia aliituma kutoka Yerusalemu kwenda kwa wazee waliobaki miongoni mwa wale waliohamishwa na kwa makuhani, manabii na watu wengine wote ambao Nebukadneza alikuwa amewachukua kwenda uhamishoni Babeli kutoka Yerusalemu. (Hii ilikuwa ni baada ya Mfalme Yekonia
29:2 Yekonia au Konia ni jina jingine la Yehoyakini
na malkia mamaye, maafisa wa mahakama, viongozi wa Yuda na wa Yerusalemu, mafundi na wahunzi kwenda uhamishoni kutoka Yerusalemu.)
Barua ilikabidhiwa kwa Elasa mwana wa Shafani na Gemaria mwana wa Hilkia, ambao Sedekia mfalme wa Yuda aliwatuma kwa Mfalme Nebukadneza huko Babeli. Barua yenyewe ilisema:

Hili ndilo BWANA Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, awaambialo wale wote niliowapeleka kutoka Yerusalemu kwenda uhamishoni Babeli: “Jengeni nyumba na mstarehe, pandeni bustani na mle mazao yake. Oeni wake na mzae wana na binti, waozeni wana wenu wake nanyi watoeni binti zenu waolewe, ili nao pia wazae wana na binti. Ongezekeni idadi yenu huko, wala msipungue. Pia tafuteni amani na mafanikio ya mji ambamo nimewapeleka uhamishoni. Mwombeni BWANA kwa ajili ya mji kwa sababu ukistawi, ninyi pia mtastawi.”

Naam, hili ndilo BWANA Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: “Msikubali manabii na wabashiri walioko miongoni mwenu wawadanganye. Msisikilize ndoto ambazo mmewatia moyo kuota. Wanawatabiria ninyi uongo kwa Jina langu. Sikuwatuma,” asema BWANA.

10 Hili ndilo asemalo BWANA: “Miaka sabini itakapotimia kwa ajili ya Babeli, nitakuja kwenu na kutimiza ahadi yangu ya rehema ya kuwarudisha mahali hapa. 11 Kwa maana ninajua mipango niliyo nayo kwa ajili yenu,” asema BWANA, “ni mipango ya kuwafanikisha na wala si ya kuwadhuru, ni mipango ya kuwapa tumaini katika siku zijazo. 12 Kisha mtaniita na mtakuja na kuniomba, nami nitawasikiliza. 13 Mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote. 14 Nitaonekana kwenu,” asema BWANA, “nami nitawarudisha watu wenu waliotekwa. Nitawakusanya kutoka katika mataifa yote na mahali pote nilipokuwa nimewafukuzia, nami nitawarudisha mahali ambapo nilikuwa nimewatoa ili wachukuliwe uhamishoni,” asema BWANA.

15 Mnaweza mkasema, “BWANA ameinua manabii kwa ajili yetu huku Babeli,” 16 lakini hili ndilo asemalo BWANA kuhusu mfalme aketiaye kiti cha enzi cha Daudi na watu wa kwenu wote wanaobaki katika mji huu, yaani nchi yenu, watu ambao hawakwenda pamoja nanyi uhamishoni, 17 naam, hili ndilo asemalo BWANA Mwenye Nguvu Zote: “Nitatuma upanga, njaa na tauni dhidi yao nami nitawafanya kuwa kama tini dhaifu zile ambazo ni mbaya sana zisizofaa kuliwa. 18 Nitawafukuza kwa upanga, kwa njaa na kwa tauni nami nitawafanya kitu cha kuchukiza sana kwa falme zote za dunia na kuwa kitu cha laana na cha kuogofya, cha dharau na kukemewa, miongoni mwa mataifa yote nitakakowafukuzia. 19 Kwa kuwa hawakuyasikiliza maneno yangu,” asema BWANA, “maneno ambayo niliwatumia tena na tena kupitia watumishi wangu manabii. Wala ninyi watu wa uhamisho hamkusikiliza pia,” asema BWANA.

20 Kwa hiyo, sikieni neno la BWANA, enyi nyote mlio uhamishoni niliowapeleka Babeli kutoka Yerusalemu. 21 Hili ndilo BWANA Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo kuhusu Ahabu mwana wa Kolaya na Sedekia mwana wa Maaseya, wanaowatabiria uongo kwa Jina langu: “Nitawatia mikononi mwa Nebukadneza mfalme wa Babeli, naye atawaua mbele ya macho yenu hasa. 22 Kwa ajili yao, watu wote wa uhamisho kutoka Yuda walioko Babeli watatumia laana hii: ‘BWANA na akutendee kama Sedekia na Ahabu, ambao mfalme wa Babeli aliwachoma kwa moto.’ 23 Kwa kuwa wamefanya mambo maovu kabisa katika Israeli, wamezini na wake za majirani zao, tena kwa Jina langu wamesema uongo, mambo ambayo sikuwaambia kuyafanya, nami ni shahidi wa jambo hilo,” asema BWANA.

Ujumbe Kwa Shemaya

24 Mwambie Shemaya Mnehelami, 25 “Hili ndilo BWANA Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: Ulituma barua kwa jina lako mwenyewe kwa watu wote wa Yerusalemu, kwa Sefania mwana wa kuhani Maaseya na kwa makuhani wengine wote. Ulimwambia Sefania, 26 ‘BWANA amekuweka wewe uwe kuhani badala ya Yehoyada uwe msimamizi wa nyumba ya BWANA, utamfunga kwa mikatale na mnyororo wa shingoni mwendawazimu ye yote anayejifanya nabii. 27 Kwa nini basi hukumkemea Yeremia wa Anathothi, aliyejifanya kama nabii miongoni mwenu? 28 Ametutumia ujumbe huu huko Babeli: Mtakuwako huko muda mrefu. Kwa hiyo jengeni nyumba mkakae, pandeni mashamba na mle mazao yake.’ ”

29 Kuhani Sefania, hata hivyo, akamsomea nabii Yeremia ile barua. 30 Ndipo neno la BWANA likamjia Yeremia kusema: 31 “Tuma ujumbe huu kwa watu wote walio uhamishoni: ‘Hili ndilo BWANA asemalo kuhusu Shemaya Mnehelami: Kwa sababu Shemaya amewatabiria ninyi, hata ingawa sikumtuma, naye amewafanya kuamini uongo, 32 hili ndilo BWANA asemalo: Hakika nitamwadhibu Shemaya Mnehelami pamoja na uzao wake. Hapatakuwa na ye yote atakayebaki miongoni mwa watu hawa, wala hataona mema nitakayowatendea watu wangu, asema BWANA, kwa sababu ametangaza uasi dhidi yangu.’ ”

Copyright information for Neno