Jeremiah 31

Kurudi Kwa Watu Wa Uhamishoni Kwa Shangwe

1“Wakati huo, nitakuwa Mungu wa koo zote za Israeli nao watakuwa watu wangu,” asema BWANA.

2Hili ndilo asemalo BWANA: “Watu watakaopona upanga
watapata upendeleo jangwani,
nitakuja niwape Israeli pumziko.”3BWANA alitutokea wakati uliopita akisema: “Nimekupenda kwa upendo wa milele,
nimekuvuta kwa wema.
4Nitakujenga tena nawe utajengeka upya,
Ewe Bikira Israeli.
Utachukua tena matari yako
na kwenda kucheza na wenye furaha.
5Utapanda tena shamba la mizabibu
juu ya vilima vya Samaria,
wakulima watapanda
na kufurahia matunda yake.
6Itakuja siku wakati walinzi watakapowapigia kelele
juu ya vilima vya Efraimu wakisema,
‘Njoni, twendeni juu Sayuni,
kwake BWANA Mungu wetu.’ ”7Hili ndilo asemalo BWANA: “Mwimbieni Yakobo kwa furaha,
mpigieni kelele aliye mkuu wa mataifa.
Zifanyeni sifa zenu zisikike, nanyi mseme,
‘Ee BWANA, okoa watu wako,
mabaki ya Israeli.’
8Tazama, nitawaleta kutoka nchi ya kaskazini
na kuwakusanya kutoka miisho ya dunia.
Miongoni mwao watakuwepo vipofu na viwete,
mama wajawazito na wenye utungu wa kuzaa,
umati mkubwa wa watu utarudi.
9Watakuja wakilia;
wataomba wakati nikiwarudisha.
Nitawaongoza kando ya vijito vya maji
katika mapito yaliyo tambarare
ambapo hawatajikwaa,
kwa sababu mimi ndimi baba wa Israeli,
naye Efraimu ni mwanangu,
mzaliwa wangu wa kwanza.
10“Sikieni neno la BWANA, Enyi mataifa,
litangazeni katika nchi za pwani ya mbali:
‘yeye aliyewatawanya Israeli atawakusanya
na atalichunga kundi lake la kondoo
kama mchungaji.’
11Kwa kuwa BWANA atamlipia fidia Yakobo
na kuwakomboa kutoka mkononi mwao
walio na nguvu kuliko wao.
12Watakuja na kupiga kelele kwa furaha katika miinuko ya Sayuni;
watashangilia ukarimu wa BWANA:
nafaka, divai mpya na mafuta,
wana-kondoo wachanga
na ndama wa makundi ya ng'ombe nitakaowapa.
Watakuwa kama bustani iliyonyeshewa vizuri,
wala hawatahuzunika tena.
13Kisha wanawali watacheza na kufurahi,
vijana waume na wazee pia.
Nitageuza maombolezo yao kuwa furaha,
nitawapa faraja na furaha badala ya huzuni.
14Nitawashibisha makuhani kwa wingi,
nao watu wangu watajazwa kwa ukarimu wangu,”
asema BWANA.15Hili ndilo asemalo BWANA: “Sauti imesikika huko Rama,
maombolezo na kilio kikubwa,
Raheli akiwalilia watoto wake
na anakataa kufarijiwa,
kwa sababu watoto wake hawako tena.”16Hili ndilo asemalo BWANA: “Izuie sauti yako kulia
na macho yako yasitoe machozi,
kwa kuwa kazi yako itapata thawabu,”
asema BWANA.

“Watarudi kutoka nchi ya adui.
17Kwa hiyo kuna tumaini kwa ajili yako
katika siku zijazo,”
asema BWANA.

“Watoto wako watarudi
katika nchi yao yenyewe.
18“Hakika nimeyasikia maombolezo ya Efraimu:
‘Ulinirudi kama ndama mkaidi,
nami nimekubali kutii.
Unirudishe, nami nitarudi,
kwa sababu wewe ndiwe BWANA, Mungu wangu.
19Baada ya kupotea,
nilitubu;
baada ya kuelewa,
nilijipiga kifua.
Niliaibika na kuona haya
kwa sababu niliibeba aibu ya ujana wangu.’
20Je, Efraimu si mwanangu mpendwa,
mtoto ninayependezwa naye?
Ingawa mara kwa mara ninanena dhidi yake,
bado ninamkumbuka.
Kwa hiyo moyo wangu unamwonea shauku,
nina huruma kubwa kwa ajili yake,”
asema BWANA.

21“Weka alama za barabara,
weka vibao vya kuelekeza.
Zingatia vyema njia kuu,
barabara ile unayoipita.
Rudi, Ee Bikira Israeli,
rudi kwenye miji yako.
22Utatangatanga hata lini,
Ee binti usiye mwaminifu?
BWANA ameumba kitu kipya duniani,
mwanamke atamlinda mwanaume.”23Hili ndilo BWANA Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo, “Nitakapowarudisha toka nchi ya kutekwa kwenu, watu walio katika nchi ya Yuda na miji yake kwa mara nyingine tena watatumia maneno haya: ‘BWANA akubariki, Ee makao ya haki, Ee mlima mtakatifu.’ 24Watu wataishi pamoja katika Yuda na miji yake yote, wakulima na wote wanaohamahama na mifugo yao. 25Nitawaburudisha waliochoka na kuwatuliza walio na huzuni.”

26Kwa jambo hili niliamka na kuangalia pande zote. Usingizi wangu ulikuwa mtamu kwangu.

27BWANA asema, “Siku zinakuja, nitakapoongeza idadi ya watu na kuzidisha hesabu ya mifugo katika nyumba ya Israeli na nyumba ya Yuda. 28Kama vile nilivyowaangalia ili kuwang'oa na kubomoa, kuharibu, kuangamiza na kuleta maafa juu yao, vivyo hivyo nitawaangalia ili kujenga na kupanda,” asema BWANA. 29“Katika siku hizo watu hawatasema tena, “ ‘Baba wamekula zabibu chachu,
nayo meno ya watoto yakatiwa ganzi.’30Badala yake, kila mmoja atakufa kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe; ye yote alaye zabibu chachu, meno yake mwenyewe yatatiwa ganzi. 31

“Wakati unakuja,” asema BWANA,
“nitakapofanya Agano jipya
na nyumba ya Israeli
na nyumba ya Yuda.
32Halitafanana na Agano
nililofanya na baba zao
wakati nilipowashika mkono
na kuwaongoza watoke Misri,
kwa sababu walivunja Agano langu,
ijapokuwa nilikuwa mume kwao,”
asema BWANA.

33“Hili ndilo Agano nitakalofanya na nyumba ya Israeli,
baada ya wakati ule,” asema BWANA.
“Nitaweka sheria yangu ndani yao
na kuiandika katika mioyo yao.
Nitakuwa Mungu wao,
nao watakuwa watu wangu.
34Mtu hatamfundisha tena jirani yake,
au mtu kumfundisha ndugu yake akisema, ‘Umjue BWANA Mungu,’
kwa sababu wote watanijua mimi,
kuanzia aliye mdogo kabisa kwao hata aliye mkuu sana,”
asema BWANA.

“Kwa sababu nitausamehe uovu wao
na sitazikumbuka dhambi zao tena.”35Hili ndilo asemalo BWANA, yeye aliyeweka jua
liwake mchana,
yeye anayeamuru mwezi na nyota
kung'ara usiku,
yeye aichafuaye bahari
ili mawimbi yake yangurume;
BWANA Mwenye Nguvu Zote ndilo jina lake:
36“Ikiwa amri hizi zitaondoka machoni pangu,”
asema BWANA,
“ndipo wazao wa Israeli watakoma
kuwa taifa mbele yangu daima.”37Hili ndilo asemalo BWANA: “Ikiwa mbingu zilizo juu zitaweza kupimika
na misingi ya dunia chini
ikaweza kuchunguzwa,
ndipo nitakapowakataa wazao wote wa Israeli
kwa sababu ya yote waliyoyatenda,”
asema BWANA.38“Siku zinakuja,” asema BWANA, “wakati mji huu utakapojengwa kwa upya kwa ajili yangu kuanzia mnara wa Hananeli hadi Lango la Pembeni. 39Kamba ya kupimia itaanzia hapo kunyooka mpaka kwenye kilima cha Garebu na kisha kugeuka kuelekea Goa. 40Bonde lote watupwapo maiti na majivu pia na matuta yote kutoka Bonde la Kidroni upande wa mashariki mpaka kwenye pembe ya Lango la Farasi, itakuwa takatifu kwa BWANA. Kamwe mji huu hautang'olewa tena wala kubomolewa.”

Copyright information for Neno