Jeremiah 33

Ahadi Ya Kurudishwa

1Wakati Yeremia alipokuwa angali amefungwa kwenye ua wa walinzi, neno la BWANA lilimjia mara ya pili kusema: 2“Hili ndilo BWANA asemalo, yeye aliyeumba dunia, BWANA aliyeifanya na kuithibitisha, BWANA ndilo jina lake: 3‘Niite nami nitakuitika na kukuambia mambo makuu na yasiyochunguzika usiyoyajua.’ 4Kwa maana hili ndilo BWANA, Mungu wa Israeli, asemalo kuhusu nyumba katika mji huu na majumba ya kifalme ya Yuda yaliyobomolewa yatumiwe dhidi ya kule kuzungukwa na jeshi na upanga 5katika kupigana na Wakaldayo: ‘Zitajazwa na maiti za watu nitakaowachinja katika hasira na ghadhabu yangu. Nitauficha uso wangu kwa sababu ya maovu yake yote.

6“ ‘Hata hivyo, nitauletea afya na uponyaji, nitawaponya watu wangu na kuwafanya wafurahie amani tele na salama. 7Nitawarudisha Yuda na Israeli kutoka katika nchi ya kutekwa kwao na kuwajenga tena kama walivyokuwa hapo awali. 8Nitawatakasa dhambi zote walizofanya dhidi yangu na nitawasamehe dhambi zote za uasi dhidi yangu. 9Kisha mji huu utaniletea utukufu, furaha, sifa na heshima mbele ya mataifa yote ya dunia yatakayosikia juu ya mambo yote mazuri ninayoufanyia, nao watashangaa na kutetemeka kwa ajili ya wingi wa mafanikio na amani nitakayoupatia.’

10“Hili ndilo asemalo BWANA: ‘Mnasema kuhusu mahali hapa kwamba, “Ni mahali palipoachwa ukiwa, pasipo na wanadamu wala wanyama.” Lakini katika miji ya Yuda na barabara za Yerusalemu ambazo zimeachwa, ambazo hazikaliwi na wanadamu wala wanyama, huko kutasikika kwa mara nyingine 11sauti za shangwe na furaha, sauti za bibi na BWANA arusi na sauti za wale waletao sadaka za shukrani katika nyumba ya BWANA, wakisema, “ ‘ “Mshukuruni BWANA Mwenye Nguvu Zote,
kwa maana BWANA ni mwema;
upendo wake wadumu milele.”


Kwa kuwa nitairudishia nchi baraka kama zilivyokuwa hapo awali,’ asema BWANA.

12“Hili ndilo asemalo BWANA Mwenye Nguvu Zote: ‘Mahali hapa, ambapo ni ukiwa pasipo na wanadamu wala wanyama, katika miji yake, patakuwepo tena malisho kwa ajili ya wachungaji kupumzisha makundi yao ya kondoo na mbuzi. 13Katika miji ya nchi ya vilima, ya vilima vya magharibi na ya Negebu, katika nchi ya Benyamini, katika vijiji vinavyoizunguka Yerusalemu na katika miji ya Yuda, makundi ya kondoo na mbuzi yatapita tena chini ya mkono wa yeye ayahesabuye,’ asema BWANA.

14“ ‘Siku zinakuja,’ asema BWANA, ‘wakati nitakapotimiza ahadi yangu ya rehema niliyoifanya kwa nyumba ya Israeli na kwa nyumba ya Yuda. 15“ ‘Katika siku hizo na wakati huo nitalifanya Tawi la haki
lichipuke kutoka ukoo wa Daudi,
naye atafanya lile lililo haki na sawa
katika nchi.
16Katika siku hizo, Yuda ataokolewa
na Yerusalemu ataishi salama.
Hili ndilo jina atakaloitwa:
BWANA Ndiye Haki Yetu.’17Kwa maana hili ndilo asemalo BWANA: ‘Daudi kamwe hatakosa mtu wa kukalia kiti cha enzi cha nyumba ya Israeli, 18wala hata makuhani, ambao ni Walawi, kamwe hawatakosa mtu wa kusimama mbele zangu daima ili kutoa sadaka za kuteketezwa, ili kuteketeza sadaka ya nafaka na kutoa dhabihu.’ ”

19Neno la BWANA likamjia Yeremia kusema: 20“Hili ndilo asemalo BWANA: ‘Ikiwa mtaweza kuvunja Agano langu kuhusu mchana na usiku, ili mchana na usiku visiwepo kwa nyakati zake, 21basi Agano langu na Daudi mtumishi wangu na Agano langu na Walawi ambao ni makuhani wanaohudumu mbele zangu, linaweza kuvunjwa na Daudi hatakuwa tena na mzao wa kutawala katika kiti chake cha enzi. 22Nitawafanya wazao wa Daudi mtumishi wangu na Walawi wanaohudumu mbele zangu wasioweza kuhesabika kama nyota za angani, tena wasiopimika kama mchanga wa ufuoni mwa bahari.’ ”

23Neno la BWANA likamjia Yeremia kusema: 24“Je, hujasikia kwamba watu hawa wanasema, ‘BWANA amezikataa zile falme mbili alizozichagua?’ Kwa hiyo wamewadharau watu wangu na hawawaoni tena kama taifa. 25Hili ndilo asemalo BWANA: ‘Kama sijathibitisha Agano langu na mchana na usiku na kuzisimika sheria za mbingu na nchi, 26basi nitawakataa wazao wa Yakobo na Daudi mtumishi wangu na sitachagua mmoja wa wanawe kutawala juu ya wazao wa Abrahamu, Isaki na Yakobo. Kwa maana nitawarudisha kutoka kwenye nchi ya kutekwa kwao na kuwaonea huruma.’ ”

Copyright information for Neno