Jeremiah 35

Warekabi Wasifiwa

Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwa BWANA wakati wa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda: “Nenda kwa jamaa ya Warekabi na uwaalike waje kwenye moja ya vyumba vya pembeni vya nyumba ya BWANA na uwape divai wanywe.”

Basi nikaenda kumwita Yaazania mwana wa Yeremia, mwana wa Habazinia, ndugu zake na wanawe wote, yaani jamaa nzima ya Warekabi. Nikawaleta katika nyumba ya BWANA, ndani ya chumba cha wana wa Hanani mwana wa Igdalia mtu wa Mungu. Kilikuwa karibu na chumba cha maafisa, ambacho kilikuwa juu ya kile cha Maaseya mwana wa Shalumu aliyekuwa bawabu. Kisha nikaweka mabakuli yaliyojaa divai na baadhi ya vikombe mbele ya watu wa jamaa ya Warekabi na kuwaambia, “Kunyweni divai.”

Lakini wao wakajibu, “Sisi hatunywi divai, kwa sababu baba yetu Yonadabu mwana wa Rekabu, alitupa agizo hili: ‘Ninyi wala wazao wenu kamwe msinywe divai. Pia msijenge nyumba kamwe, wala kuotesha mbegu au kupanda mashamba ya mizabibu, kamwe msiwe na kitu cho chote katika hivi, lakini siku zote lazima muishi kwenye mahema. Ndipo mtakapoishi kwa muda mrefu katika nchi ambayo ninyi ni wahamiaji.’ Tumetii kila kitu ambacho baba yetu Yonadabu, mwana wa Rekabu, alichotuamuru. Sisi wenyewe wala wake zetu wala wana wetu na binti zetu kamwe hatujanywa divai wala kujenga nyumba za kuishi au kuwa na mashamba ya mizabibu, mashamba au mazao. 10 Tumeishi katika mahema na tumetii kikamilifu kila kitu alichotuamuru baba yetu Yonadabu. 11 Lakini wakati Nebukadneza mfalme wa Babeli alipoivamia nchi hii, tulisema, ‘Njoni, ni lazima twende Yerusalemu ili kukimbia majeshi ya Wakaldayo na ya Washami.’ Kwa hiyo tumeishi Yerusalemu.”

12 Ndipo neno la BWANA likamjia Yeremia kusema: 13 “Hili ndilo BWANA Mwenye Nguvu Zote, aliye Mungu wa Israeli, asemalo: Nenda ukawaambie watu wa Yuda na watu wa Yerusalemu, ‘Je, hamwezi kujifunza kutoka kwa wana wa Rekabu na kuyatii maneno yangu?’ asema BWANA. 14 ‘Yonadabu mwana wa Rekabu aliwaagiza wanawe wasinywe divai na agizo hilo wamelishika mpaka leo hawanywi divai kwa sababu wanatii amri ya baba yao. Lakini nimenena nanyi tena na tena, lakini hamkunitii mimi. 15 Tena na tena nimewatuma watumishi wangu wote manabii kwenu. Wakasema, “Kila mmoja wenu ni lazima ageuke na kuacha njia zake mbaya na kuyatengeneza matendo yake, msifuate miungu mingine ili kuitumikia. Ndipo mtakapoishi katika nchi niliyowapa ninyi na baba zenu.” Lakini hamkujali wala kunisikiliza. 16 Wazao wa Yonadabu mwana wa Rekabu walitimiza amri ambayo baba yao aliwapa, lakini watu hawa hawakunitii mimi.’

17 “Kwa hiyo, hili ndilo BWANA Mungu Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli asemalo: ‘Sikilizeni! Nitaleta juu ya Yuda na juu ya kila mmoja aishiye Yerusalemu kila aina ya maafa niliyotamka dhidi yao. Nilinena nao, lakini hawakusikiliza, niliwaita, lakini hawakujibu.’ ”

18 Kisha Yeremia akaiambia jamaa ya Warekabi, “Hili ndilo asemalo BWANA Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli: ‘Mmetii amri ya baba yenu Yonadabu na mmefuata mafundisho yake yote na mmefanya kila kitu alichowaamuru.’ 19 Kwa hiyo hili ndilo BWANA Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Yonadabu mwana wa Rekabu hatakosa kamwe kumpata mtu wa kunitumikia mimi.’ ”

Copyright information for Neno