Jeremiah 36

Yehoyakimu Achoma Kitabu Cha Yeremia

1Katika mwaka wa nne wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda, neno hili lilimjia nabii Yeremia kutoka kwa BWANA kusema: 2“Chukua kitabu na uandike ndani yake maneno yote niliyonena nawe kuhusu Israeli, Yuda na mataifa mengine yote tangu nilipoanza kunena nawe wakati wa utawala wa Yosia hadi sasa. 3Labda watu wa Yuda watakaposikia juu ya kila maafa ninayokusudia kuwapiga nayo kila mmoja wao atageuka kutoka katika njia zake mbaya, kisha nitasamehe uovu wao na dhambi yao.”

4Hivyo Yeremia akamwita Baruki mwana wa Neria, naye Yeremia alipokuwa akiyakariri maneno yote aliyoyasema BWANA, Baruki akayaandika katika kitabu. 5Kisha Yeremia akamwambia Baruki, “Nimezuiliwa, mimi siwezi kuingia katika Hekalu la BWANA. 6Basi wewe nenda katika nyumba ya BWANA siku ya kufunga na uwasomee watu maneno ya BWANA kutoka katika kitabu hiki yale uliyoyaandika kutoka kinywani mwangu. Wasomee watu wote wa Yuda waliofika kutoka kwenye miji yao. 7Labda wataomba na kusihi mbele za BWANA na kila mmoja atageuka kutoka katika njia zake mbaya, kwa sababu hasira na ghadhabu zilizotamkwa dhidi ya watu hawa na BWANA ni kubwa.”

8Baruki mwana wa Neria akafanya kila kitu nabii Yeremia alichomwambia kufanya, katika Hekalu la BWANA alisoma maneno ya BWANA kutoka katika kile kitabu. 9Katika mwezi wa tisa, mnamo mwaka wa tano wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda, wakati wa kufunga mbele za BWANA ilitangazwa kwa watu wote walioko Yerusalemu na wale wote waliokuwa wamekuja kutoka miji ya Yuda. 10Kutoka katika chumba cha Gemaria mwana wa Shafani mwandishi, kilichokuwa katika ua wa juu kwenye ingilio la Lango Jipya la Hekalu, Baruki akawasomea watu wote waliokuwa katika Hekalu la BWANA maneno ya Yeremia kutoka kwenye kile kitabu.

11Basi Mikaya mwana wa Gemaria, mwana wa Shafani, aliposikia maneno yote ya BWANA kutoka kwenye kile kitabu, 12alishuka kwenye chumba cha mwandishi kwenye jumba la kifalme, mahali walipokuwa wameketi maafisa wote, yaani: Elishama mwandishi, Delaya mwana wa Shemaya, Elnathani mwana wa Akbori, Gemaria mwana wa Shafani, Sedekia mwana wa Hanania na maafisa wengine wote. 13Baada ya Mikaya kuwaambia kila kitu ambacho alikuwa amesikia Baruki akiwasomea watu kutoka kwenye kile kitabu, 14maafisa wote wakamtuma Yehudi mwana wa Nethania, mwana wa Shelemia, mwana wa Kushi, kumwambia Baruki, “Leta hicho kitabu ambacho umewasomea watu nawe mwenyewe uje.” Ndipo Baruki mwana wa Neria akawaendea akiwa na hicho kitabu mkononi mwake. 15Wakamwambia, “Tafadhali, keti na utusomee hicho kitabu.”

Ndipo Baruki akawasomea kile kitabu.
16Walipoyasikia maneno haya yote, wakatazamana wao kwa wao kwa woga na kumwambia Baruki, “Ni lazima tutoe taarifa ya maneno haya yote kwa mfalme.” 17Kisha wakamwuliza Baruki, “Tuambie, uliandikaje haya yote? Je, yalitoka kinywani mwa Yeremia?”

18Baruki akajibu, “Ndiyo, maneno haya yote yalitoka kinywani mwa Yeremia, nami nikayaandika kwa wino katika hiki kitabu.”

19Ndipo wale maafisa wakamwambia Baruki, “Wewe na Yeremia nendeni mkajifiche. Mtu ye yote asijue mahali mlipo.”

20Baada ya kuhifadhi kile kitabu ndani ya chumba cha Elishama mwandishi, wakamwendea mfalme katika ua wa nje na kumwarifu kila kitu. 21Mfalme akamtuma Yehudi akachukue kile kitabu na Yehudi akakileta hicho kitabu kutoka kwenye chumba cha Elishama mwandishi na akakisoma mbele ya mfalme na maafisa wakiwa wamesimama kando ya mfalme. 22Ulikuwa mwezi wa tisa na mfalme alikuwa ameketi chumba cha wakati wa baridi akiota moto. 23Hata ikawa kila wakati Yehudi alipomaliza kusoma kurasa tatu au nne za hicho kitabu, mfalme alizikata kwa kisu cha mwandishi na kuzitupia motoni hadi kitabu chote kikateketea. 24Mfalme na watumishi wake wote waliosikia yote yaliyosomwa hawakuonyesha hofu yo yote wala hawakuyararua mavazi yao. 25Hata ingawa Elnathani, Delaya na Gemaria walimsihi mfalme asikichome kile kitabu lakini hakuwasikiliza. 26Badala yake, mfalme akamwamuru Yerameeli, mwana wa mfalme, Seraya mwana wa Azrieli na Shelemia mwana wa Abdeeli kuwakamata mwandishi Baruki na nabii Yeremia. Lakini BWANA alikuwa amewaficha.

27Baada ya mfalme kuchoma kile kitabu kilichokuwa na yale maneno Baruki aliyokuwa ameyaandika kutoka kinywani mwa Yeremia, neno la BWANA lilimjia Yeremia likisema: 28“Chukua kitabu kingine na uandike juu yake maneno yote yaliyokuwa katika kile kitabu cha kwanza, ambacho Yehoyakimu mfalme wa Yuda amekiteketeza kwa moto. 29Mwambie pia Yehoyakimu mfalme wa Yuda, ‘Hili ndilo asemalo BWANA: Ulikiteketeza kile kitabu ukasema, “Kwa nini uliandika kwenye kitabu kwamba kwa hakika mfalme wa Babeli angekuja na kuangamiza nchi hii na kuwakatilia mbali watu na wanyama kutoka humo?” 30Kwa hiyo, hili ndilo asemalo BWANA kuhusu Yehoyakimu mfalme wa Yuda: Hatakuwa na mtu ye yote atakayekalia kiti cha enzi cha Daudi, maiti yake itatupwa nje kwenye joto wakati wa mchana na kupigwa na baridi wakati wa usiku. 31Nitamwadhibu yeye, watoto wake na watumishi wake kwa ajili ya uovu wao, nitaleta juu yao na wote waishio Yerusalemu na watu wa Yuda kila maafa niliyoyasema dhidi yao, kwa sababu hawajasikiliza.’ ”

32Kisha Yeremia akachukua kitabu kingine na kumpa mwandishi Baruki mwana wa Neria, naye kama Yeremia alivyosema, Baruki akaandika juu yake maneno yote ya kile kitabu ambacho Yehoyakimu mfalme wa Yuda alikuwa amekichoma moto na maneno mengine mengi yanayofanana na hayo yaliyoongezewa humo.

Copyright information for Neno