Jeremiah 37

Yeremia Gerezani

1Sedekia mwana wa Yosia akafanywa kuwa mfalme wa Yuda na Nebukadneza mfalme wa Babeli, akatawala mahali pa Yehoyakini
37.1 Yehoyakini ni jina jingine la Yekonia au Konia
mwana wa Yehoyakimu.
2Lakini si Sedekia wala watumishi wake wala watu wa nchi waliosikiliza maneno ya BWANA aliyonena kupitia kwa nabii Yeremia.

3Hata hivyo, Mfalme Sedekia, akamtuma Yehukali mwana wa Shelemia pamoja na kuhani Sefania mwana wa Maaseya kwa nabii Yeremia wakiwa na ujumbe huu: “Tafadhali utuombee kwa BWANA, Mungu wetu.”

4Wakati huu Yeremia alikuwa huru kuingia na kutoka katikati ya watu, kwa sababu alikuwa bado hajatiwa gerezani. 5Jeshi la Farao lilikuwa limetoka Misri, nao Wakaldayo ambao walikuwa wameuzunguka Yerusalemu kwa majeshi waliposikia taarifa kuhusu jeshi hilo walijiondoa Yerusalemu.

6Ndipo neno la BWANA likamjia nabii Yeremia kusema: 7“Hili ndilo asemalo BWANA, Mungu wa Israeli: Mwambie mfalme wa Yuda aliyekutuma uniulize mimi, ‘Jeshi la Farao lililotoka kuja kukusaidia litarudi katika nchi yake yenyewe, yaani Misri. 8Kisha Wakaldayo watarudi na kushambulia mji huu, watauteka na kuuchoma moto.’

9“Hili ndilo BWANA asemalo: Msijidanganye wenyewe mkifikiri kwamba, ‘Hakika Wakaldayo watatuacha na kwenda zao.’ Hakika hawatawashambulia! 10Hata kama mngelishinda jeshi lote la Wakaldayo linalowashambulia ninyi na wakawa ni watu waliojeruhiwa tu waliobaki kwenye mahema yao, wangetoka na kuuchoma mji huu moto.”

11Baada ya jeshi la Wakaldayo kujiondoa kutoka Yerusalemu kwa sababu ya jeshi la Farao, 12Yeremia akaanza kuondoka mjini ili kwenda kwenye nchi ya Benyamini ili akapate sehemu yake ya milki miongoni mwa watu huko. 13Lakini alipofika kwenye Lango la Benyamini, mkuu wa walinzi, ambaye jina lake lilikuwa Iriya mwana wa Shelemia, mwana wa Hanania, akamkamata na kusema, “Wewe unakwenda kujiunga na Wakaldayo!”

14Yeremia akasema, “Hiyo si kweli, mimi sijiungi na Wakaldayo.” Lakini Iriya hakumsikiliza; badala yake, akamkamata Yeremia na kumpeleka kwa maafisa. 15Wakamkasirikia Yeremia, wakaruhusu apigwe na akafungwa katika nyumba ya Yonathani mwandishi waliyokuwa wameifanya gereza.

16Yeremia akawekwa kwenye chumba kilichofukuliwa chini kilichojengwa kwa zege ndani ya gereza chini ya ngome, akakaa huko kwa muda mrefu. 17Kisha Mfalme Sedekia akatuma aletwe katika jumba la kifalme, mahali alipomwuliza kwa siri, “Je, kuna neno lo lote kutoka kwa BWANA?”

Yeremia akajibu, “Ndiyo, utatiwa mikononi mwa mfalme wa Babeli.”

18Kisha Yeremia akamwambia Mfalme Sedekia, “Nimefanya kosa gani dhidi yako na maafisa wako au watu hawa, hata ukanitia gerezani? 19Wako wapi manabii wako waliokutabiria wakisema, ‘Mfalme wa Babeli hatakushambulia wewe wala nchi hii?’ 20Lakini sasa, bwana wangu mfalme, tafadhali sikiliza. Niruhusu nilete maombi yangu mbele yako, usinirudishe kwenye nyumba ya Yonathani mwandishi nisije nikafa humo.”

21Ndipo Mfalme Sedekia akatoa maagizo Yeremia awekwe katika ua wa walinzi na apewe mkate kutoka mitaa ya waokaji kila siku mpaka mikate yote katika mji itakapokwisha. Kwa hiyo Yeremia akabaki katika ua wa walinzi.

Copyright information for Neno