Jeremiah 39

Anguko La Yerusalemu

1Hivi ndivyo Yerusalemu ilivyotwaliwa: Katika mwaka wa tisa wa utawala wa Mfalme Sedekia wa Yuda, katika mwezi wa kumi, Nebukadneza mfalme wa Babeli alilipeleka jeshi lake lote dhidi ya Yerusalemu na akauzunguka. 2Katika siku ya tisa ya mwezi wa nne wa mwaka wa kumi na moja wa utawala wa Sedekia kutawala, ukuta wa mji ulibomolewa. 3Kisha maafisa wote wa mfalme wa Babeli wakaja na kuketi katika viti kwenye Lango la Kati nao ni: Nergal-Shareza wa Samgari, Nebo-Sarsekimu afisa mkuu, Nergal-Shareza afisa mwenye cheo cha juu na maafisa wengine wote wa Mfalme wa Babeli. 4Mfalme Sedekia wa Yuda na askari wote walipowaona, wakakimbia, na kuondoka mjini wakati wa usiku kwa njia ya bustani ya mfalme kupitia lango lililo kati ya kuta mbili na kuelekea Araba
39.4 Au: kuelekea Bonde la Yordani
.

5Lakini jeshi la Wakaldayo liliwafuatia na kumkuta Sedekia kwenye tambarare za Yeriko. Wakamkamata na kumpeleka kwa Nebukadneza mfalme wa Babeli huko Ribla katika nchi ya Hamathi, mahali walipomhukumu. 6Huko Ribla, mfalme wa Babeli aliwachinja wana wa Sedekia mbele ya macho yake na akawaua wakuu wote wa Yuda. 7Kisha akang'oa macho ya Sedekia na kumfunga kwa pingu za shaba, na kumpeleka Babeli.

8Jeshi la Wakaldayo likachoma moto jumba la kifalme, nyumba za watu na kubomoa kuta za Yerusalemu. 9Nebuzaradani kiongozi wa walinzi wa kifalme akawachukua na kuwapeleka uhamishoni Babeli wale watu pamoja na wale waliokuwa wamebaki ndani ya mji, pamoja na wale waliokuwa wamemwendea, na watu wengine wote. 10Lakini Nebuzaradani, kiongozi wa walinzi aliwabakiza baadhi ya watu maskini katika nchi ya Yuda, ambao hawakuwa na kitu, naye kwa wakati ule aliwapa mashamba ya mizabibu na mashamba mengine.

11Basi, Nebukadneza mfalme wa Babeli alikuwa ametoa maagizo kuhusu Yeremia kupitia Nebuzaradani kiongozi wa walinzi wa kifalme akisema: 12“Mchukue umtunze, usimdhuru, lakini umfanyie cho chote anachotaka.” 13Basi Nebuzaradani kiongozi wa walinzi, Nebushazbani afisa mkuu, Nergal-Shareza afisa wa cheo cha juu na maafisa wengine wote wa mfalme wa Babeli 14wakatuma watu kumwondoa Yeremia kutoka katika ua wa walinzi. Wakamkabidhi kwa Gedalia mwana wa Ahikamu, mwana wa Shafani, ili amrudishe nyumbani kwake. Kwa hiyo akabaki miongoni mwa watu wake mwenyewe.

15Wakati Yeremia alipokuwa amezuiliwa katika ua wa walinzi, neno la BWANA lilimjia kusema: 16“Nenda ukamwambie Ebed-Meleki, Mkushi, ‘Hili ndilo BWANA Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: Ninakaribia kutimiza maneno yangu dhidi ya mji huu kwa njia ya maafa, wala si kwa kuwafanikisha. Wakati huo hayo yatatimizwa mbele ya macho yako. 17Lakini siku hiyo nitakuokoa, asema BWANA; hutatiwa mikononi mwa wale unaowaogopa. 18Nitakuokoa; hutaanguka kwa upanga, lakini maisha yako yatakuwa salama, kwa sababu unanitumaini, asema BWANA.’ ”

Copyright information for Neno