Jeremiah 41

Katika mwezi wa saba, Ishmaeli mwana wa Nethania, mwana wa Elishama, ambaye alikuwa wa uzao wa kifalme na pia alikuwa mmoja wa maafisa wa mfalme, akaja pamoja na watu kumi kwa Gedalia mwana wa Ahikamu huko Mizpa. Walipokuwa wakila pamoja huko, Ishmaeli mwana wa Nethania pamoja na wale watu kumi waliokuwa pamoja naye waliinuka na kumwua Gedalia mwana wa Ahikamu, mwana wa Shafani kwa upanga, wakamwua yule ambaye mfalme wa Babeli alikuwa amemweka awe mtawala juu ya nchi. Ishmaeli akawaua pia Wayahudi wote waliokuwa na Gedalia huko Mizpa, pamoja na askari wa Kikaldayo waliokuwa huko.

Siku moja baada ya kuuawa kwa siri kwa Gedalia, kabla mtu ye yote hajafahamu juu ya jambo hilo, watu themanini waliokuwa wamenyoa ndevu zao, waliorarua nguo zao na kujikatakata walikuja kutoka Shekemu, Shilo na Samaria wakileta sadaka za nafaka na uvumba katika nyumba ya BWANA. Ishmaeli mwana wa Nethania akaondoka Mizpa ili kwenda kuwalaki, huku akilia alipokuwa akienda. Alipokutana nao, akasema, “Karibuni kwa Gedalia mwana wa Ahikamu,” Walipoingia mjini, Ishmaeli mwana wa Nethania na wale watu waliokuwa pamoja naye wakawachinja na kuwatupa ndani ya kisima. Lakini watu kumi miongoni mwao wakamwambia Ishmaeli, “Sisi usituue! Tuna ngano na shayiri, mafuta na asali, vilivyofichwa katika shamba.” Kwa hiyo akawaacha na hakuwaua pamoja na wale wengine. Basi kile kisima ambacho alitupa zile maiti za watu aliowaua pamoja na Gedalia kilikuwa ni kile kisima ambacho Mfalme Asa alikifanya sehemu ya ulinzi wake dhidi ya Baasha mfalme wa Israeli. Ishmaeli mwana wa Nethania akakijaza kisima hicho kwa maiti.

10 Ishmaeli akawafanya mateka watu wote ambao Nebuzaradani kiongozi wa walinzi wa kifalme alikuwa amewaacha huko Mizpa na kumweka Gedalia mwana wa Ahikamu juu yao, ambao ni binti za mfalme pamoja na watu wote aliokuwa amewaacha huko. Ishmaeli mwana wa Nethania akawachukua mateka na kuondoka nao akavuka kwenda kwa Waamoni.

11 Ikawa Yohanani mwana wa Karea na maafisa wote wa jeshi waliokuwa pamoja naye waliposikia juu ya uhalifu wote ambao Ishmaeli mwana wa Nethania alikuwa ameufanya, 12 waliwachukua watu wao wote kwenda kupigana na Ishmaeli mwana wa Nethania. Wakakutana naye karibu na bwawa kubwa huko Gibeoni. 13 Ikawa watu wote waliokuwa na Ishmaeli walipomwona Yohanani mwana wa Karea pamoja na maafisa wa jeshi waliokuwa pamoja naye, wakafurahi. 14 Watu wote ambao Ishmaeli alikuwa amewachukua mateka huko Mizpa wakageuka na kumfuata Yohanani mwana wa Karea. 15 Lakini Ishmaeli mwana wa Nethania pamoja na watu wake wanane wakamtoroka Yohanani na kukimbilia kwa Waamoni.

Kukimbilia Misri

16 Ndipo Yohanani mwana wa Karea pamoja na maafisa wote wa jeshi waliokuwa pamoja naye wakawaongoza wote walionusurika waliotoka Mizpa ambao walipona kutoka mikononi mwa Ishmaeli mwana wa Nethania baada ya kumwua Gedalia mwana wa Ahikamu, yaani askari, wanawake, watoto na matowashi aliowaleta kutoka Gibeoni. 17 Kisha wakaenda mbele na kutua Geruth Kimhamu karibu na Bethlehemu wakiwa njiani kwenda Misri 18 ili kuwatoroka Wakaldayo. Waliwaogopa kwa sababu Ishmaeli mwana wa Nethania alikuwa amemwua Gedalia mwana wa Ahikamu, ambaye alikuwa amewekwa na mfalme wa Babeli kuwa mtawala wa nchi.

Copyright information for Neno