Jeremiah 50

Ujumbe Kuhusu Babeli

Hili ndilo neno alilosema BWANA kupitia nabii Yeremia kuhusu Babeli na nchi ya Wakaldayo:

“Tangazeni na mhubiri katikati ya mataifa,
twekeni bendera na mkahubiri;
msiache kitu cho chote, bali semeni,
‘Babeli utatekwa;
Beli ataaibishwa,
Merodaki atajazwa na hofu kuu.
Sanamu zake zitaaibishwa
na vinyago vyake vitajazwa hofu kuu.’
Taifa kutoka kaskazini litamshambulia
na kuifanya nchi yake ukiwa.
Hakuna hata mmoja atakayeishi ndani yake,
watu na wanyama wataikimbia.
“Katika siku hizo, wakati huo,”
asema BWANA,
“watu wa Israeli pamoja na watu wa Yuda
wataenda wakilia
ili kumtafuta BWANA Mungu wao.
Wataiuliza njia iendayo Sayuni
na kuelekeza nyuso zao huko.
Watakuja na kuambatana na BWANA
katika Agano la milele
ambalo halitasahaulika.
“Watu wangu wamekuwa kondoo waliopotea;
wachungaji wao wamewapotosha
na kuwasababisha kuzungukazunguka
juu ya milima.
Walitangatanga juu ya mlima na kilima
na kusahau mahali pao wenyewe
pa kupumzikia.
Ye yote aliyewakuta aliwala;
adui zao walisema,
‘Sisi hatuna hatia,
kwa kuwa wao walitenda dhambi dhidi ya BWANA,
malisho yao halisi,
BWANA, aliye tumaini la baba zao.’
“Kimbieni kutoka Babeli;
ondokeni katika nchi ya Wakaldayo
tena iweni kama mbuzi wale waongozao kundi.
Kwa maana nitaamsha na kuleta dhidi ya Babeli
muungano wa mataifa makubwa
kutoka nchi ya kaskazini.
Watashika nafasi zao dhidi yake,
naye kwa kutokea kaskazini atatekwa.
Mishale yao itakuwa kama mishale ya mashujaa walio hodari
ambao hawawezi kurudi mikono mitupu.
10 Kwa hiyo Ukaldayo utatekwa nyara;
wote wamtekao nyara watapata za kutosha,”
asema BWANA.

11 “Kwa sababu hushangilia na kufurahi,
wewe utekaye urithi wangu,
kwa sababu unachezacheza kama mtamba anayepura nafaka
na kulia kama farasi dume asiyehasiwa,
12 mama yako ataaibika mno,
yeye aliyekuzaa atatahayari.
Atakuwa mdogo kuliko mataifa mengine yote,
atakuwa nyika, nchi kame na jangwa.
13 Kwa sababu ya hasira ya BWANA hatakaliwa na mtu,
lakini ataachwa ukiwa kabisa.
Wote watakaopita Babeli watatiwa hofu na kudhihaki
kwa sababu ya majeraha yake yote.
14 “Shikeni nafasi zenu kuzunguka Babeli,
enyi nyote mvutao upinde.
Mpigeni! Msibakize mshale wo wote,
kwa kuwa ametenda dhambi dhidi ya BWANA.
15 Piga kelele dhidi yake kila upande!
Anajisalimisha, minara yake inaanguka,
kuta zake zimebomoka.
Kwa kuwa hiki ni kisasi cha BWANA,
mlipizeni kisasi;
mtendeeni kama alivyowatendea wengine.
16 Katilieni mbali mpanzi kutoka Babeli,
naye mvunaji pamoja na mundu wake akivuna.
Kwa sababu ya upanga wa mdhalimu
kila mmoja na arejee
kwa watu wake mwenyewe,
kila mmoja na akimbilie
kwenye nchi yake mwenyewe.
17 “Israeli ni kundi lililotawanyika
ambalo simba wamelifukuzia mbali.
Wa kwanza kumla alikuwa mfalme wa Ashuru,
wa mwisho kuponda mifupa yake
alikuwa Nebukadneza mfalme wa Babeli.”18 Kwa hiyo hili ndilo BWANA Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: “Nitamwadhibu mfalme wa Babeli na nchi yake
kama nilivyomwadhibu mfalme wa Ashuru.
19 Lakini nitamrudisha Israeli katika malisho yake mwenyewe
naye atalisha huko Karmeli na Bashani;
njaa yake itashibishwa
juu ya vilima vya Efraimu na Gileadi.
20 Katika siku hizo, wakati huo,”
asema BWANA,
“uchunguzi utafanyika kwa ajili ya kosa la Israeli,
lakini halitakuwepo,
kwa ajili ya dhambi za Yuda,
lakini haitapatikana hata moja,
kwa kuwa nitawasamehe
mabaki nitakaowaacha.
21 “Shambulieni nchi ya Merathaimu
na wale waishio huko Pekodi.
Wafuatieni, waueni
na kuwaangamiza kabisa,”
asema BWANA.

“Fanyeni kila kitu nilichowaamuru.
22 Kelele ya vita iko ndani ya nchi,
kelele ya maangamizi makuu!
23 Tazama jinsi nyundo ya dunia yote
ilivyovunjika na kuharibika!
Tazama jinsi Babeli ilivyokuwa ukiwa
miongoni mwa mataifa!
24 Nimetega mtego kwa ajili yako, Ee Babeli,
nawe ukakamatwa kabla haujafahamu;
ulipatikana na ukakamatwa
kwa sababu ulimpinga BWANA.
25 BWANA amefungua ghala lake la silaha
na kuzitoa silaha za ghadhabu yake,
kwa kuwa BWANA Mwenyezi Mwenye Nguvu Zote
anayo kazi ya kufanya
katika nchi ya Wakaldayo.
26 Njoni dhidi yake kutoka mbali.
Zifungueni ghala zake za nafaka;
mlundikeni kama lundo la nafaka.
Mwangamizeni kabisa
na msimwachie mabaki yo yote.
27 Waueni mafahali wake wachanga wote;
waacheni washuke machinjoni!
Ole wao! Kwa kuwa siku yao imewadia,
wakati wao wa kuadhibiwa.
28 Wasikilizeni watoro na wakimbizi kutoka Babeli
wakitangaza katika Sayuni
jinsi BWANA, Mungu wetu alivyolipiza kisasi,
kisasi kwa ajili ya Hekalu lake.
29 “Waiteni wapiga mishale dhidi ya Babeli,
wote wale wavutao upinde.
Pigeni kambi kumzunguka kabisa,
asitoroke mtu ye yote.
Mlipizeni kwa matendo yake;
mtendeeni kama alivyotenda.
Kwa kuwa alimdharau BWANA,
yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli.
30 Kwa hiyo, vijana wake wanaume wataanguka barabarani;
askari wake wote watanyamazishwa siku ile,”
asema BWANA.

31 “Tazama, niko kinyume nawe, Ewe mwenye majivuno,”
asema Bwana, BWANA Mwenye Nguvu Zote,
“kwa kuwa siku yako imewadia,
yaani, wakati wako wa kuadhibiwa.
32 Mwenye majivuno atajikwaa na kuanguka,
wala hakuna ye yote atakayemuinua;
nitawasha moto katika miji yake,
utakaowateketeza wote wanaomzunguka.”33 Hili ndilo asemalo BWANA Mwenye Nguvu Zote: “Watu wa Israeli wameonewa,
nao watu wa Yuda pia.
Wote waliowateka wamewashikilia sana,
wanakataa kuwaachia waende.
34 Lakini Mkombozi wao ana nguvu;
BWANA Mwenye Nguvu Zote ndilo jina lake.
Atatetea kwa nguvu shauri lao
ili kwamba alete raha katika nchi yao,
lakini ataleta msukosuko
kwa wale waishio Babeli.
35 “Upanga dhidi ya Wakaldayo!”
asema BWANA,
“dhidi ya wale waishio Babeli
na dhidi ya maafisa wake
na watu wenye busara!
36 Upanga dhidi ya manabii wake wa uongo!
Watakuwa wapumbavu.
Upanga dhidi ya mashujaa wake!
Watajazwa na hofu kuu
37 Upanga dhidi ya farasi na magari yake ya vita
pamoja na askari wake wote wa kigeni katika safu zake!
Wao watakuwa kama wanawake.
Upanga dhidi ya hazina zake!
Hizo zitatekwa nyara.
38 Ukame juu ya maji yake!
Nayo yatakauka.
Kwa kuwa ni nchi ya sanamu,
wao wanapenda sana sanamu.
39 “Hivyo viumbe vya jangwani na fisi wataishi humo,
nao bundi watakaa humo.
Kamwe haitakaliwa tena
wala watu hawataishi humo
kutoka kizazi hadi kizazi.
40 Kama vile Mungu alivyoangamiza Sodoma na Gomora
pamoja na miji iliyo jirani nayo,”
asema BWANA,

“vivyo hivyo hapatakuwa na mtu ye yote
atakayeishi humo.
Naam, hakuna mtu ye yote
atakayekaa humo.
41 “Tazama! Jeshi linakuja kutoka kaskazini;
taifa kubwa na wafalme wengi
wameamshwa kutoka miisho ya dunia.
42 Wamejifunga pinde na mikuki;
ni wakatili na wasio na huruma.
Wanasikika kama bahari inayonguruma
wanapoendesha farasi zao;
wanakuja kama watu waliojipanga kwa vita
ili kukushambulia, Ee Binti Babeli.
43 Mfalme wa Babeli amesikia habari kuwahusu hao,
nayo mikono yake imelegea.
Uchungu umemshika,
maumivu kama yale ya mwanamke
aliye katika utungu wa kuzaa.
44 Kama simba anayepanda kutoka kwenye vichaka vya Yordani
kuja kwenye nchi ya malisho manono,
nitamfukuza Babeli kutoka nchi yake ghafula.
Ni nani aliye mteule,
nimweke kwa ajili ya jambo hili?
Ni nani aliye kama mimi
na ni nani awezaye kunipinga?
Tena ni mchungaji yupi
awezaye kusimama dhidi yangu?”
45 Kwa hiyo, sikia kile BWANA alichokipanga dhidi ya Babeli,
kile alichokusudia dhidi ya nchi ya Wakaldayo:
Aliye mchanga katika kundi ataburutwa mbali,
ataharibu kabisa malisho yao kwa sababu yao.
46 Kwa kusikika kutekwa kwa Babeli,
dunia itatetemeka;
kilio chake kitaenea pote
miongoni mwa mataifa.


Copyright information for Neno