Jeremiah 6

Yerusalemu Imezingirwa Na Jeshi

1“Kimbieni kwa usalama wenu, enyi watu wa Benyamini!
Kimbieni kutoka Yerusalemu!
Pigeni tarumbeta katika Tekoa!
Inueni ishara juu ya Beth-Hakeremu!
Kwa kuwa maafa yanaonekana yakitoka kaskazini
na uharibifu wa kutisha.
2Nitamwangamiza Binti Sayuni,
aliye mzuri sana na mororo.
3Wachungaji pamoja na makundi yao ya kondoo
na mbuzi watakuja dhidi yake;
watapiga mahema yao kumzunguka,
kila mmoja akichunga kundi lake mwenyewe.”
4“Jiandaeni kwa vita dhidi yake!
Inukeni na tumshambulie mchana!
Lakini, ole wetu, mchana unaisha
na vivuli vya jioni vinazidi kuwa virefu.
5Kwa hiyo inukeni, tufanye mashambulizi usiku
na kuharibu ngome zake!”
6

Hivi ndivyo asemavyo BWANA Mwenye Nguvu Zote: “Kateni miti mjenge boma
kuzunguka Yerusalemu.
Mji huu ni lazima uadhibiwe,
umejazwa na uonevu.
7Kama vile kisima kinavyomwaga maji yake,
ndivyo anavyomwaga uovu wake.
Ukatili na maangamizi yasikika ndani yake,
ugonjwa wake na majeraha yake
viko mbele yangu daima.
8Pokea onyo, Ee Yerusalemu,
la sivyo nitageukia mbali nawe
na kuifanya nchi yako kuwa ukiwa
asiweze mtu kuishi ndani yake.”9Hivi ndivyo asemavyo BWANA Mwenye Nguvu Zote: “Wao na wayakusanye mabaki ya Israeli
kwa uangalifu kama kwenye mzabibu;
pitisha mkono wako kwenye matawi tena,
kama yeye avunaye zabibu.”
10Niseme na nani na kumpa onyo?
Ni nani atakayenisikiliza mimi?
Masikio yao yameziba
6.10 Masikio yameziba kwa Kiebrania ina maana kwamba masikio yao hayajatahiriwa

kwa hiyo hawawezi kusikia.
Neno la BWANA ni chukizo kwao,
hawalifurahii.
11Lakini nimejaa ghadhabu ya BWANA,
nami siwezi kuizuia.
“Wamwagie watoto walioko barabarani,
na juu ya vijana waume
waliokusanyika pamoja;
mume na mke watakumbwa kwa pamoja ndani yake,
hata nao wazee waliolemewa na miaka.
12Nyumba zao watapewa watu wengine,
pamoja na mashamba yao na wake zao,
nitakapounyosha mkono wangu
dhidi ya wale waishio katika nchi,”
asema BWANA.

13“Kuanzia aliye mdogo kabisa hadi mkubwa kabisa,
wote wanatamani kupata faida isiyo halali;
makuhani na manabii wanafanana,
wote wanafanya udanganyifu.
14Hufunga majeraha ya watu wangu
kama vile hawakuumia sana.
Husema, ‘Amani, amani,’
wakati hakuna amani.
15Je, wanaona aibu kwa ajili ya tabia yao
inayochukiza mno?
Hapana, hawana aibu hata kidogo;
hawajui hata kuona haya.
Kwa hiyo wataanguka miongoni mwa hao walioanguka,
watashushwa nitakapowaadhibu,”
asema BWANA.16Hivi ndivyo asemavyo BWANA: “Simama kwenye njia panda utazame,
ulizia mapito ya zamani,
ulizia wapi ilipo njia nzuri, uifuate hiyo,
nanyi mtapata raha nafsini mwenu.
Lakini ninyi mlisema, ‘Hatutaipita hiyo.’
17Niliweka walinzi juu yenu na kusema,
‘Sikieni sauti ya tarumbeta!’
Lakini mkasema, ‘Hatutasikiliza.’
18Kwa hiyo sikilizeni, Enyi mataifa,
angalieni, Enyi mashahidi,
lile litakalowatokea.
19Sikia Ee nchi:
Ninaleta maafa juu ya watu hawa,
matunda ya mipango yao,
kwa sababu hawakusikiliza maneno yangu
na wameikataa sheria yangu.
20Wanifaa nini uvumba kutoka Sheba
au udi wa harufu nzuri kutoka nchi ya mbali?
Sadaka zako za kuteketezwa hazikubaliki,
dhabihu zako hazinifurahishi mimi.”21Kwa hiyo hivi ndivyo asemavyo BWANA: “Nitawawekea vikwazo mbele ya watu hawa.
Baba na wana wao watajikwaa juu yake,
majirani na marafiki wataangamia.”22Hivi ndivyo asemavyo BWANA: “Tazama, jeshi linakuja
kutoka nchi ya kaskazini,
taifa kubwa linaamshwa
kutoka miisho ya dunia.
23Wamejifunga pinde na mkuki,
ni wakatili na hawana huruma.
Wanatoa sauti kama bahari inayonguruma
wanapokuwa wamepanda farasi zao,
wanakuja kama watu walioandaliwa tayari kwa vita
kukushambulia wewe, Ee Binti Sayuni.”
24Tumesikia taarifa zao,
nayo mikono yetu imelegea.
Uchungu umetushika,
maumivu kama mwanamke
mwenye utungu wa kuzaa.
25Usitoke kwenda mashambani
au kutembea barabarani,
kwa kuwa adui ana upanga
na kuna vitisho kila upande.
26Enyi watu wangu, vaeni magunia
mjivingirishe kwenye majivu,
ombolezeni kwa kilio cha uchungu
kama amliliaye mwana pekee,
kwa maana ghafula
mharabu atatujia.
27“Nimekufanya wewe kuwa kitu cha kujaribu chuma
na watu wangu kama mawe yenye madini,
ili upate kuzijua na kuzijaribu njia zao.
28Wote ni waasi sugu,
wakienda huko na huko kusengenya.
Wao ni shaba na chuma,
wote wanatenda kwa upotovu.
29Mivuo inavuma kwa nguvu,
kinachoungua kwa huo moto ni risasi,
lakini pamoja na kusafisha kote huku ni bure;
waovu hawaondolewi.
30Wanaitwa fedha iliyokataliwa,
kwa sababu BWANA amewakataa.”


Copyright information for Neno