Job 16

Hotuba Ya Tano Ya Ayubu

Ayubu Anathibitisha Tena Hali Yake Ya Kutokuwa Na Hatia

1Kisha Ayubu akajibu: 2“Nimepata kusikia mambo mengi kama haya,
nanyi nyote ni wafariji wenye kutaabisha!
3Je, maneno yenu mengi yasiyo na maana hayana mwisho?
Mna nini hata mwendelee kushindana kwa maneno?
4Mimi pia ningeweza kuzungumza kama ninyi,
kama mngekuwa katika hali yangu;
ningeweza kutoa hotuba nzuri dhidi yenu
na kuwatikisia ninyi kichwa changu.
5Lakini kinywa changu kingewatia moyo;
faraja kutoka midomoni mwangu, ingewaletea nafuu.
6“Lakini kama nikisema, maumivu yangu bado hayatulizwi,
nami kama nikijizuia, wala hayaondoki.
7Ee Mungu, hakika umenichakaza;
umewaangamiza kabisa
watu wa nyumbani mwangu wote.
8Umenikunjakunja, nalo limekuwa ushahidi;
nako kukonda kwangu kumeongezeka sana
na kushuhudia dhidi yangu.
9Mungu amenishambulia na kunirarua katika hasira yake
na kunisagia meno yake;
adui yangu hunikazia macho yake makali.
10Watu wamenifumbulia vinywa vyao kunidhihaki,
hunipiga shavuni mwangu kwa dharau,
na kuungana pamoja dhidi yangu.
11Mungu amenigeuzia kwa watu wabaya
na kunitupa katika makucha ya waovu.
12Mambo yote yalikuwa mazuri, lakini alinivunjavunja,
amenikamata shingo na kuniponda.
Amenifanya mimi kuwa shabaha yake;
13wapiga upinde wake wananizunguka.
Bila huruma, huchoma figo zangu
na kuimwaga nyongo yangu juu ya nchi.
14Huniponda tena na tena,
hunishambulia kama shujaa wa vita.
15“Nimejishonea nguo ya gunia juu ya mwili wangu
nami nimekizika kipaji cha uso wangu kwenye vumbi.
16Uso wangu umekuwa mwekundu kwa kulia,
macho yangu yamepigwa na giza kuu,
17hata hivyo mikono yangu haijafanya jeuri
na maombi yangu ni safi.
18“Ee nchi, usiifunike damu yangu,
nacho kilio changu kisinyamazishwe kamwe.
19Hata sasa shahidi wangu yuko mbinguni;
wakili wangu yuko juu.
20Mwombezi wangu ni rafiki yangu
macho yangu yamwagapo machozi kwa Mungu;
21kwa niaba ya mtu anamsihi Mungu
kama mtu anavyosihi kwa ajili ya rafiki yake.
22“Ni miaka michache tu itapita
kabla sijaenda safari ambayo sitarudi.


Copyright information for Neno