Job 20

Sofari Anasema: Uovu Hupokea Malipo Ya Haki

1Ndipo Sofari, Mnaamathi akajibu na kusema: 2“Mawazo yanayonisumbua yananisukuma kujibu,
kwa sababu nimehangaika sana.
3Ninasikia makaripio ambayo yananivunjia heshima,
nao ufahamu wangu unanisukuma kujibu.
4“Hakika unajua jinsi ilivyokuwa tangu zamani,
tangu zamani mwanadamu alipowekwa duniani,
5macheko ya mtu mwovu ni ya muda mfupi,
nayo furaha ya wasiomcha Mungu
hudumu kwa kitambo tu.
6Ingawa kujikweza kwake hufikia mbinguni
na kichwa chake hugusa mawingu,
7ataangamia milele kama mavi yake mwenyewe,
wale waliomwona watauliza, ‘Yuko wapi?’
8Kama ndoto hutoweka, wala hapatikani tena,
amefukuziwa mbali kama maono ya usiku.
9Jicho lililomwona halitamwona tena,
mahali pake hapatamwona tena.
10Watoto wake watalipa yote baba yao aliyowadhulumu maskini,
nayo mikono yake itarudisha mali yote aliyonyang'anya watu.
11Nguvu za ujana zilizoijaza mifupa yake,
zitalala naye mavumbini.
12“Ingawa uovu ni mtamu kinywani mwake
naye huuficha chini ya ulimi wake,
13ingawa hawezi kukubali kuuachia uende,
lakini huuweka kinywani mwake,
14hata hivyo chakula chake kitakuwa kichungu tumboni mwake,
nacho kitakuwa sumu kali ya nyoka ndani yake.
15Atatema mali alizozimeza,
Mungu atalifanya tumbo lake kuzitapika.
16Atanyonya sumu za majoka,
meno ya nyoka mwenye sumu kali yatamwua.
17Hatafurahia vijito,
mito inayotiririsha asali na siagi.
18Vile alivyovitaabikia atavirudisha bila kuvila,
hatafurahia faida itokanayo na biashara yake.
19Kwa kuwa aliwaonea maskini na kuwaacha pasipo kitu,
amenyang'anya kwa nguvu nyumba asizozijenga.
20“Hakika hatakuwa na raha katika kutamani kwake sana,
hawezi kujiokoa mwenyewe kwa hazina zake.
21Hakuna cho chote kitakachosalia kwa ajili yake ili ale,
kufanikiwa kwake hakutadumu.
22Katikati ya wingi wa ustawi wake, dhiki itampata,
taabu itamjia kwa nguvu zote.
23Wakati atakapokuwa amelijaza tumbo lake,
Mungu ataionyesha ghadhabu kali dhidi yake
na kumnyeshea mapigo yake juu yake.
24Ijapokuwa aikimbia silaha ya chuma,
mshale wa shaba utamchoma.
25Atauchomoa katika mgongo wake,
ncha ing'aayo kutoka katika ini lake.
Vitisho vitakuja juu yake,
26giza nene linavizia hazina zake.
Moto usiopepewa na mtu utamteketeza
na kuangamiza yaliyosalia nyumbani mwake.
27Mbingu zitaweka wazi hatia yake,
nayo nchi itainuka kinyume chake.
28Mafuriko yataichukua nyumba yake,
mali za nyumbani mwake zitachukuliwa na maji yaendayo kasi
katika siku ya ghadhabu ya Mungu.
29Hili ndilo fungu Mungu alilowagawia waovu,
urithi uliowekwa kwa ajili yao na Mungu.”


Copyright information for Neno