Job 21

Hotuba Ya Saba Ya Ayubu

Ayubu Anajibu: Waovu Mara Nyingi Huenda Bila Kuadhibiwa

Ndipo Ayubu akajibu: “Yasikilizeni maneno yangu kwa makini,
hii na iwe faraja mnayonipa mimi.
Nivumilieni ninapozungumza,
nami nikishazungumza,
endeleeni kunidhihaki.
“Je, kwani malalamiko yangu
yanaelekezwa kwa mwanadamu?
Kwa nini nisikose subira?
Niangalieni mkastaajabu;
mkaweke mkono juu ya vinywa vyenu.
Ninapowaza juu ya hili, ninaogopa,
nao mwili wangu unatetemeka.
Kwa nini waovu wanaendelea kuishi,
wakifikia umri wa uzee na kuendelea
kuongezeka kuwa na nguvu?
Huwaona watoto wao wakithibitika
wakiwa wamewazunguka,
wazao wao mbele za macho yao.
Nyumba zao zi salama wala hakuna hofu,
fimbo ya Mungu haiko juu yao.
10 Madume yao ya ng'ombe huvyaza bila kushindwa kamwe;
ng'ombe wao huzaa wala hawaharibu mimba.
11 Huwatoa watoto wao nje kama kundi la kondoo na mbuzi,
wadogo wao huchezacheza.
12 Huimba nyimbo kwa matari na kwa kinubi,
nao huifurahia sauti ya filimbi.
13 Huitumia miaka yao katika mafanikio
nao hushuka kaburini kwa amani.
14 Lakini humwambia Mungu, ‘Tuache sisi!’
Hatuna haja ya kufahamu njia zako.
15 Mwenyezi ni nani hata tumtumikie?
Tutapata faida gani kumwomba?
16 Lakini kufanikiwa kwao hakupo mikononi mwao wenyewe,
hivyo najitenga mbali na shauri la waovu.
17 “Lakini ni mara ngapi taa ya waovu huzimwa?
Ni mara ngapi maafa huwajia,
yale yawapatayo ambayo Mungu
huwapangia katika hasira yake?
18 Ni mara ngapi huwa kama majani makavu mbele ya upepo,
kama makapi yachukuliwayo na dhoruba?
19 Imesemekana, ‘Mungu huiweka akiba adhabu ya mtu
kwa ajili ya wanawe.’
Mungu na amlipe mtu mwenyewe,
ili apate kulijua!
20 Macho yake mwenyewe na yaone maangamizi yake,
yeye na ainywe ghadhabu ya Mwenyezi.
21 Kwani anajali nini kuhusu jamaa anayoiacha nyuma,
miezi yake aliyopangiwa ifikapo mwisho?
22 “Je, yuko mtu ye yote awezaye kumfundisha Mungu maarifa,
iwapo yeye ndiye ahukumuye hata walio juu ya wote?
23 Mtu mmoja hufa akiwa na nguvu zake kamili,
akiwa salama na mwenye raha kamili,
24 mwili wake ukiwa umenawiri,
nayo mifupa yake ikiwa imejaa mafuta ndani yake.
25 Mtu mwingine hufa katika uchungu wa nafsi,
akiwa hajafurahia kamwe jambo lolote zuri.
26 Hao wote hulala mavumbini,
nao mabuu huwafunika wote.
27 “Ninayajua kikamilifu yale mnayoyafikiri,
mipango ambayo kwayo mngenitendea mabaya.
28 Mwasema, ‘Iko wapi sasa nyumba ya huyo mtu mkuu,
mahema ambayo watu waovu walikaa yako wapi?’
29 Je, hamkuwahi kuwauliza hao wanaosafiri?
Je, hamkutafakari taarifa zao:
30 kwamba mtu mwovu huepushwa kutoka katika siku ya maafa,
kwamba huokolewa kutoka katika siku ya ghadhabu?
31 Ni nani hulaumu matendo yake mbele ya uso wake?
Ni nani ampatilizaye kwa yale aliyoyatenda?
32 Hupelekwa kaburini,
nao ulinzi ukawekwa kwenye kaburi lake.
33 Udongo ulio bondeni ni mtamu kwake;
watu wote watamfuata,
nao umati wa watu usiohesabika umemtangulia.
34 “Hivyo ninyi mnawezaje kunifariji kwa upuzi wenu?
Hakuna kilichosalia cha majibu yenu isipokuwa uongo!”


Copyright information for Neno