Job 23

Hotuba Ya Nane Ya Ayubu

Ayubu Anajibu: Kulalamika Kwangu Ni Uchungu

1Ndipo Ayubu akajibu: 2“Hata leo malalamiko yangu ni uchungu,
mkono wake ni mzito juu yangu
pamoja na kulia kwangu kwa uchungu.
3Laiti ningefahamu mahali pa kumwona,
laiti ningeweza kwenda mahali akaapo!
4Ningeliweka shauri langu mbele zake
na kukijaza kinywa changu na hoja.
5Ningejua kwamba angenijibu nini
na kuelewa lile ambalo angelisema.
6Je, angenipinga kwa nguvu nyingi?
La, asingenigandamiza, bali angenisikiliza.
7Hapo mtu mwadilifu angeweka shauri lake mbele zake,
nami ningeokolewa milele na mhukumu wangu.
8“Lakini nikienda mashariki, hayupo,
nikienda magharibi, simpati.
9Anapokuwa kazini pande za kaskazini, simwoni,
akigeukia kusini, nako simwoni hata kidogo.
10Lakini anaijua njia niiendeayo,
akiisha kunijaribu, nitatoka kama dhahabu.
11Nyayo zangu zimefuata hatua zake kwa karibu,
nimeishika njia yake bila kukengeuka.
12Sijaziacha amri zilizotoka midomoni mwake,
bali nimeyathamini maneno ya kinywa chake
kuliko chakula changu cha kila siku.
13“Lakini yeye ndiye aamuaye peke yake,
ni nani awezaye kumpinga?
Yeye hufanya lo lote alitakalo.
14Hutimiliza maagizo yake dhidi yangu,
na bado anayo mipango mingi kama hiyo
ambayo ameiweka akiba.
15Hiyo ndiyo sababu ninaingiwa na hofu mbele zake,
nifikiriapo haya yote ninamwogopa.
16Mungu ameufanya moyo wangu kuzimia,
yeye Mwenyezi amenitia hofu.
17Hata hivyo sikunyamazishwa na giza,
wala kwa giza nene linalofunika uso wangu.


Copyright information for Neno