Job 27

Hotuba Ya Mwisho Ya Ayubu

Ayubu Anadumisha Uadilifu wake

Ndipo Ayubu akaendelea na hoja yake, akasema: “Hakika kama Mungu aishivyo, aliyeninyima haki yangu,
Mwenyezi ambaye amenifanya
nionje uchungu wa nafsi,
kwa muda wote nitakaokuwa na uhai ndani yangu,
nayo pumzi ya Mungu ikiwa puani mwangu,
midomo yangu haitanena uovu,
wala ulimi wangu hautatamka udanganyifu.
Sitakubaliana nanyi kabisa kuwa mko sahihi,
hadi nife, sitakana uadilifu wangu.
Nitadumisha haki yangu wala sitaiacha;
dhamiri yangu haitanisuta muda wote ninaoishi.
“Watesi wangu wawe kama waovu,
nao adui zangu wawe kama wasio haki!
Kwa maana mtu asiyemcha Mungu
analo tegemeo gani anapokatiliwa mbali,
Mungu anapouondoa uhai wake?
Je, Mungu husikiliza kilio chake,
shida zimjiapo?
10 Je, anaweza kumfurahia Mwenyezi?
Je, atamwita Mungu nyakati zote?
11 “Nitawafundisha juu ya uweza wa Mungu,
njia za Mwenyezi sitazificha.
12 Ninyi nyote mmeona hili wenyewe.
Ni ya nini basi mazungumzo haya yasiyo na maana?
13 “Hili ndilo fungu ambalo Mungu humpa mtu mwovu,
urithi wa mtu mdhalimu
anaopokea kutoka kwa Mwenyezi:
14 Hata kama watoto wake watakuwa wengi kiasi gani,
fungu lao ni kuuawa kwa upanga,
wazao wake hawatakuwa kamwe
na chakula cha kuwatosha.
15 Tauni itawazika wale watakaonusurika miongoni mwao,
nao wajane wao hawatawaombolezea.
16 Ajapokusanya fedha nyingi kama mavumbi
na mavazi kama malundo ya udongo wa mfinyanzi,
17 yale yote mtu mwovu aliyojiwekea akiba,
mwenye haki ndiye atakayevaa,
naye asiye na hatia ndiye atakayeigawanya fedha yake.
18 Nyumba aijengayo ni kama utando wa buibui,
kama kibanda alichotengeneza mlinzi.
19 Yeye hulala akiwa tajiri, lakini ndiyo mara ya mwisho,
afunguapo macho yake, yote yametoweka.
20 Vitisho humjia kama mafuriko,
dhoruba humkumba ghafula usiku.
21 Upepo mkali wa mashariki humchukua, naye hutoweka,
humzoa kutoka mahali pake.
22 Humvurumisha bila huruma,
huku akikimbia kasi kukwepa nguvu zake.
23 Upepo humpigia makofi kwa dharau
na kumfukuza atoke mahali pake.


Copyright information for Neno